Kutana na mwanamke aliyevuka changamoto tano za Udereva. - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Monday, 10 March 2025

Kutana na mwanamke aliyevuka changamoto tano za Udereva.

 

Mama huyu Amefanya kazi ya udereva kwa miaka 37 akiendesha mabasi makubwa,daladala,mitambo ya kuvunja miamba,magreda na magari ya viongozi.



Amegeukia ujasiliamali akifuga kuku,njiwa na kuzalisha dawa lishe za mmea wa mwani.






Na: Burhani Yakub, Tanga.


maipacarusha20@gmail.com 


Uthubutu, kujituma, tabia njema, ucheshi na umahiri awapo barabarani ni silaha zilizomvusha Zubeda Hajji Mohamed (53) kuvuka changamoto tano alizopitia katika kazi yake ya udereva wa mabasi makubwa ya abiria, mitambo ya kutengeneza barabara kwa kipindi cha miaka 37.

"Kitabu cha "The Bus Driver " nilichokisoma nikiwa kidato cha kwanza kilinifanya niweke azma ya kuja kuwa dereva mkubwa wa mabasi ya abiria, ndoto ambayo niliweza kuitimiza na kuibuka kuwa miongoni mwa wanawake watatu nchini Tanzania walioasisi na kufanya kazi ya udereva Kwa umakini na kuleta heshima Kwa wanawake wote wa Tanzania.

Hayo ni maneno aliyoyatamka Zubeda Hajji Mohamed ambaye alipokuwa akizungumza na Mwandishi wa habari akielezea milima na mabonde aliyopitia wakati akifanya kazi ya udereva kipindi cha miaka 37 na baadaye kuwa mfugaji na mjasiliamali maarufu wa ndani na nje ya Tanzania.

Alianza kwa kueleza historia yake kwamba alizaliwa mwaka 1972 mtaa wa Tangulia kata ya Majengo Soko la mjinga barabara ya 18 Ngamiani jijini Tanga na kuhitimu elimu ya Msingi  shule ya Changa iliyokuwa ikijulikana St Anthony mwaka 1985 ambapo mwaka 1986 alijiunga shule ya Sekondari Jumuiya.

"Sikuendelea na masomo sababu nilipata ujauzito nikiwa kidato cha pili mwaka  1988 nikamzaa mwanangu wa kwanza akiwa na miezi nane nikaomba kusoma udereva pale Tanga Driving School nilipohutimu ikawa ndiyo mwanzo wa kufanya kazi ya udereva"alisema Zubeda.

Alianza kazi ya udereva mwaka 1989 akiajiriwa katika mradi wa barabara. vijijini RRM chini ya Wizara ya Ujenzi akiendesha Toyota Land cruiser ambapo alikuwa akimuendesha mtaalamu raia wa Norway.

"Katika usaili uliofanyika tulikuwa wasailiwa nane aliyekuwa akihitajika kuajiriwa ni mmoja pekee ambaye sikuwa na cheti cha kuhutimu kidato cha nne ni mimi peke yangu... nashukuru Mungu niliweza kupita na kuajiriwa rasmi, cheti cha udereva na majaribio Kwa vitendo vilinibeba"alisema Zubeda.

Alisema baada ya mradi wa RRM kumalizika aliajiriwa na Mamlaka ya Mkonge katika mradi maalumu wa Ngombezi Wilayani Korogwe na baadaye akaajiriwa Wilaya ya Handeni mwenye mradi wa kuondoa jangwa HIAP uliokuwa ukiendeshwa chini ya shirika la ujerumani GIZ.

"Nikiwa RRM namshukuru mkaguzi mkuu wa barabara, George Johnsen aliamuru niendeshe pia maroli makubwa ya kusomba kokoto, magreda na mitambo ya kuvunja miamba, nikafanya Kwa ufanisi wa hali ya juu"alisema Zubeda.

Safari yake ya udereva wa mabasi ilianza Kwa kuendesha daladala za Tanga jiji na baadaye Tanga-Lushoto ikiwa ni mara yake ya kwanza kuwasafirisha abiria wengi.

"Nilisimama kidogo kuendesha magari nikajiingiza kwenye biashara ya kuleta magari nchini Tanzania kutoka Dubai lakini ilipofana nikadhulumiwa mtaji wote nikabaki mtupu ndipo mwaka 1998 nikaanza kazi ya kuendesha mabasi makubwa ya abiria ya kampuni ya Shabiby kati ya Dodoma na Tanga na baadaye nikahamishiwa mabasi ya kuwaendesha wabunge"amesema Zubeda.

Kampuni nyingine alizofanyia kazi akiwa dereva wa mabasi makubwa ya abiria ni RATCO, Tashriff, Hajees na Tawfic.

Alizitaja changamoto kuu tano alizokumbana nazo katika kazi ya udereva kipindi cha miaka 37 aliyokuwa barabarani kuwa ni pamoja na watu barabarani kumshangaa dereva mwanamke 

Changamoto nyingine ni kuendesha gari kipindi cha mvua ambapo magari hayakai barabarani, uendeshaji wa gari kutoka Chalinze kwenda Dodoma ambapo alisema Kuna malori mengi hivyo inataka dereva wa mabasi kuwa na subira ya hali ya juu.

"Changamoto nyingine ni kipindi kirefu kuacha familia nyumbani na kuwa barabarani, mimi ni mama na mlezi familia yangu inahitaji niwe karibu.... lakini hili kasumba ya jamii kudhani kuwa mwanamke ni mtu wa kupika tu jikoni ni changamoto kubwa katika kazi za madereva wanawake"alisema Zubeda.

Mwanamke huyo Kwa sasa ameamua kustaafu kazi ya udereva wa mabasi na kujihusisha na ufugaji wa kuku wa nyama na mayai wa kisasa na kienyeji, njiwa na ujasiliamali wa kutengeneza na kuuza dawa lishe itokanayo na mmea wa mwani.

"Ujasiliamali wa ufugaji wa kuku unaniwezesha kumudu maisha yangu ya kila siku, njiwa japokuwa idadi yao ni kubwa sana lakini siuzi...lakini dawa lishe ya unga wa mwani inasaidia kutibu magonjwa mengi na inaagizwa na wateja kutoka mikoa ya ndani na nje ya nchi.

Miongoni mwa mafanikio aliyoyapa Zubeda kutokana na kazi ya udereva ni pamoja na kujenga nyumba ya kisasa, kumiliki magari mawili na kuendesha shughuli mbalimbali za kusaidia jamii .

Zubeda amewatia moyo wanawake kujitoa kwa wingi katika kazi za udereva wa magari, meli, ndege na mitambo ya kutengeneza vitu mbalimbali Kwa kuwa Ina vipato vya uhàkika.

Meneja mstaafu wa Wakala wa barabara (Tanroads) Mkoa wa Tanga, Alfread Ndumbaro anamwelezea Zubeda kuwa alikuwa akifanya kazi yake ya udereva kwa umahiri na hakuwahi kupata ajali katika kipindi chote.

"Kunapotokea misafara ya viongozi wa kitaifa tulikuwa tukimuomba Zubeda kuendesha magari na hii ilitokana na umahiri wake, kujiamin na kuipenda kazi yake


       MWISHO 

No comments: