Wanawake wa Jamii ya kimasai waomba kampeni ya Samia legal Aid, iwafikie vijijini - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Wednesday, 12 March 2025

Wanawake wa Jamii ya kimasai waomba kampeni ya Samia legal Aid, iwafikie vijijini

 




Na Mwandishi Wetu, Arusha.


 maipacarusha20@gmail.com


Wanawake wa Jamii ya Kimasai wameiomba serikali kufikisha huduma za msaada wa kisheria katika jamii za pembezoni ili kusaidia kukabiliana na vikwazo vya kimila vinavyowanyima haki zao.


Wamesema kuwa kwenye jamii yao bado kuna baadhi ya mila potofu ambazo zimekuwa vikwazo vya kuleta usawa wa kijinsia katika jamii zao ikiwemo  haki sawa ya umiliki wa ardhi, ndoa za utotoni lakini pia haki ya mtoto wa kike kupata elimu.


Akizungumza kwa niaba ya wenzake, jijini Arusha, Mwenyekiti wa Taasisi ya Enyorata, Himid Joel Ole Mollel amesema kuwa pamoja na changamoto hizo wanamshukuru Rais Samia Suluhu Tangu aingie madarakani sera mbalimbali zimetungwa na utekelezaji kufanyika ambazo zimepunguza makali ya vikwazo vya kimila.


Himid amesema, ili kutatua na kotokomeza kabisa mambo hayo, wanaiomba serikali chini ya uongozi wa Rais Samia kufikisha elimu ya kisheria katika maeneo ya vijijini ili kuwasaidia wanawake kupata ufahamu zaidi wa haki zao na jinsi ya kuzitumia katika kuboresha maisha yao na ya familia zao.


 “Tunashukuru tangu Rais Samia Suluhu aingie madarakani kushika nafasi ya Makamu wa Rais na sasa ni Rais,  kwanza imetupa chachu kubwa na morali kwamba kumbe mwanamke inawezekana kupata nafasi hizi kubwa,  lakini pia amefanya harakati na kampeni nyingi za kuhakikisha usawa wa kijinsia katika jamii zote na hii imesaidia kuongeza thamani ya mwanamke kwenye jamii zetu”amesema na kuongeza;


“Hata hivyo bado kuna baadhi ya vikwazo vinachelewesha kasi ya usawa wa kijinsia katika jamii zetu za pembezoni hivyo tunaomba hizi huduma za msaada wa kisheria ikiwemo kampeni ya ‘Samia Legal Aid’ ambazo tumeona kwenye maonyesho hapa mjini katika maadhimisho ya siku ya mwanamke yasiishie mjini tu bali yafike hadi vijijini maana nadhani sisi ndio wahitaji wakubwa zaidi”amesema.


Amesema kuwa katika jamii hiyo awali mtoto wa kike hakuwa na haki ya kupata elimu tofauti na sasa huku mwanamke akiwa haruhusiwi kumiliki ardhi tofauti na sasa hivyo kuishukuru serikali kwa hatua hizo.


“Waswahili husema moyo usio na shukrani hupoteza vyote tumeona mabadiliko makubwa na hii imetupa hadi sisi wanawake wa kimasai tuliobahatika miaka ya nyuma kupata elimu, kuungana kikundi kwa ajili ya kusomesha wasichana wa jamii zetu ambao wana moyo na maono ya mbali ikiwa sehemu ya kumshukuru Mungu lakini kuisapoti serikali kwa kutupigania” amesema.


Nae Katibu wa Kikundi hicho Glory Lengidare amesema kuwa kikundi chao chenye wanataaluma mbalimbali za udaktari, seremala, walimu, wakandarasi na wahandisi kimefanikiwa kusomesha zaidi ya wasichana 200 wa jamii hiyo ili nao kuja kuwa mabalozi wazuri wa kusaidia wenzao.


“Bado jamii yetu pamoja na muamko wa Elimu, lakini wako wanapigwa vita ili kutokwenda shule huku wakitakiwa kubaki nyumbani waolewe, hivyo sisi tuliovuka vikwazo hivyo tuliona ni muhimu kuwatetea katika vita hiyo na kuwawezesha kupata elimu kwa lengo la kuinua familia zao kiuchumi baadae” amesema.


Alitumia nafasi hiyo kuishukuru Serikali kwa kampuni zao za ukandarasi na useremala kupata tenda nyingi za ujenzi wa madarasa na utengenezaji wa madawati kwa fedha Uviko-19 ambayo mbali na kusaidia uchumi wao binafsi lakini pia imetunisha mfuko wao wa kusaidia kusomesha wasichana wengi zaidi.


 mwisho

No comments: