ZINGATIENI KUTUMIA MBEGU BORA KWA KILIMO BIASHARA ILA MPATE MAZAO BORA - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Wednesday, 12 March 2025

ZINGATIENI KUTUMIA MBEGU BORA KWA KILIMO BIASHARA ILA MPATE MAZAO BORA


Meneja Mkuu wa Balton Tanzania Jacob Vortzer akizungumza na waandishi wa Habari

Chonya Wema, Mtaalam wa sayansi ya mimea wa kampuni ya Balton Tanzania, akizungumza na waandishi wa Habari






Na mwandishi wetu, Arusha

maipacarusha@gmail.com

WAKULIMA wa mazao ya mbogamboga na matunda nchini wametakiwa kushirikisha familia zao katika biashara ya kilimo ili kilimo hicho kiwe endelevu kwa manufaa ya familia na taifa kwa ujumla.


Ushauri huo umetolewa mkoani Arusha hivi karibuni na mwenyekiti wa jumuiya ya wafanyabiashara wa uzalishaji na usambazaji wa mbegu nchini (TASTA) Bobu Shuma wakati wa mafunzo ya shamba darasa kwa baadhi ya wakulima kutoka mikoa mbalimbali nchini yaliyoandaliwa na kampuni ya BALTON Tanzania ambao ni waagizaji na wasambazaji wa mbegu nchini.

Aidha wakulima hao wametakiwa kupata ushauri wa mbegu inayofaa kulingana na mahali wanapolima ili kuendana na mazingira ya hali ya hewa ya eneo husika ili kumuwezesha mkulima kupata mazao bora na kuepuka hasara ya kutumia mbegu isiyostawi kama inavyotarajiwa.


Shuma aliwasihi wakulima kote nchini kununua mbegu baada ya kupata ushauri wa wataalam wa kilimo kutokana na hali ya hewa iliyopo katika maeneo wanayojishughulisha na kilimo kwani siyo kila mbegu iliyofanya vyema eneo Fulani inaweza pia kufanya vema eneo lingine ambalo hali ya hewa hazilingani.

Alisema kutokana na maendeleo ya teknolojia ya uzalishaji mbegu hakuna eneo ambalo haliwezi kutumika katika kilimo ikiwemo visiwa vya unguja na pemba ambapo ni ukanda wa bahari hivyo kuwahimiza wakulima wa maeneo hayo kutumia mawakala wa mbegu waliosajiliwa kupata ushauri kuhusiana na kilimo wanachohitaji kufanya na kujua ni aina gani ya mbegu inastahili.

Alisema kufanya kilimo chenye tija katika kipindi hiki cha mabadiliko ya tabia nchi kuna hitaji taaluma kutumika zaidi ili mkulima aweze kunufaika na uwekezaji wake katika kilimo.

Mtaalam wa sayansi ya mimea wa kampuni ya Balton Tanzania,  Chonya Wema aliwataka wakulima kutumia mbegu sahihi na kulima kwa kuzingatia ushauri wa wataalam wa mimea ili kunufaika katika kazi hiyo.

Alifafanua kuwa hivi sasa kuna uzalishaji wa aina nyingi ya mbegu lakini baadhi ya mbegu hizo haziwezi kuhimili mabadiliko ya hali ya hewa na kupelekea kushambuliwa na wadudu wa mimea kwa urahisi na hivyo kumpatia hasara kubwa mkulima.

Meneja wa Kanada ya kaskazini wa mamlaka ya kudhibiti mbolea,  Gothad Liampawe amesema kuwa mafunzo haya yamekuja wakati muafaka kwani ni kipindi cha kilimo na mamlaka yake imejitahidi kudhibiti uingizwaji wa mbolea feki ili kumkwamua mkulima na athari za matumizi ya mbolea feki.

“Udhibiti wa mbolea uko vizuri kwani serikali imetoa ruzuku kwa mbolea ambapo mkulima aliyejisajili kwa ngazi ya Kijiji na kumuwezesha mkulima kupata mbolea kwa bei ya ruzuku na kupunguza gharama za uzalishaji na kuongeza kipato cha familia kwa kupata mazao bora” Alisema Liampawe

Wakiongea mara baada ya kutembelea shamba darasa wasambazaji wa mbegu Saidi Bakari Hamza kutoka pemba na Masudi Salimu Nasoro kutoka unguja walisema wamejifunza sana katika kutambua mbegu bora kulingana na maeneo waliyotoka na kuahidi kwenda kutoa ushauri kwa wakulima wa maeneo yao.

‘’Kumekua na changamoto kwa wakulima tunaowahudumia kule pemba pindi unapowauzia mbegu waliyohitaji na mbegu hiyo kushindwa kuleta tija lakini sasa nimetambua si kila mbegu inaweza kuleta tija katika kila eneo hapa nchini bali hutegemea na hali ya hewa ya ukanda husika’’ Alisema Saidi Bakari kutoka Pemba.

Meneja mkuu wa kampuni ya Balton Tanzania Jacob vorster akizungumza katika mafunzo hayo alisema waliamua kuwaita wakulima hao na wasambaji wa mbegu katika mafunzo hayo ili kuongeza ujuzi wa wadau wa kilimo katika kuzalisha kwa tija katika maeneo yao na kufanikisha malengo ya mkulima kupata mazao mengi na bora baada ya kutumia mbegu bora.

Alisema kufanya kilimo chenye tija katika kipindi hiki cha mabadiliko ya tabia nchi kutapelekea nchi kuwa na chakula cha kutosha na pia kuongeza kipato cha mkulima mmoja mmoja.

==mwisho==




No comments: