![]() |
Pichani ni SpIka wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar Zuberi Ali Maulid akikagua ujenzi wa soko la Machinga Kange jijini Tanga Picha na Burhani Yakub |
Na:Burhani Yakub, Tanga.
maipacarusha20@gmail.com
Wafanyabiashara wadogo (Machinga) wa jiji la Tanga wanatarajiwa kupata manufaa ya kuwa na sehemu maalumu ya kuuzia bidhaa zao baada ya Halmashauri ya Jiji la Tanga kuwajengea soko la kisasa litakalotumika kuuzia bidhaa mbalimbali.
Soko hilo linajengwa Kange jijini Tanga ambapo litagharimu sh 7,717,833,637.88 hadi utakapokamilika Juni 30 mwaka huu.
Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Tanga,Gwakisa Lusajo ametoa taarifa hiyo kwa Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar,Zuberi Ali Maulid alipokuwa akiweka jiwe la mradi wa ujenzi wa miundombinu ya wafanyabiashara mdogo (Machinga) Kange jijini hapa ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 61 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
Amesema Halmashauri ya Jiji la Tanga inatekeleza ujenzi wa miundombinu ya soko la Machinga Kange baada ya wafanyabiashara hao wadogo kukubaliana kuwa eneo hilo litakuwa rafiki kwao.
"Machinga walikubaliana kuwa ni eneo rafiki kwa utekelezaji wa shughuli zao kwani lipo karibu na huduma nyingine za kijamii kama vile kituo cha mabasi,jengo la kitega uchumi Samia Suluhu Hassan Business Center,maegesho ya maroli, viwanda vya saruji na ofisi ya wafanyabiashara Mkoa ambayo imekamilika"amesema Gwakisa.
Amesema hadi kukamilika unakadiriwa kugharimu sh 7,717,833,637.88 ikijumuishwa kodi huku ukiwa na sehemu nne ambapo kila moja inakadiriwa kugharimu sh 1,929,458,409.47.
"Mradi unatumia vyanzo mbalimbali vya fedha ambapo Serikali kuu ilitoa sh 540,340,273.00 za Uviko_19 huku Halmashauri ya Jiji la Tanga ilitoa sh 262,979,067.83 kupitia mapato yake ya ndani"amesema Gwakisa.
Mkuu wa Mkoa wa Tanga,Balozi Dkt Batilda Burian amesema soko la Machinga litaakisi ushirikiano wa pande mbili za muungano kwani litatumika pia na wakazi wa visiwa hivyo ambao kila wiki huwasili Tanga kwa meli kununua vyakula na bidhaa mbalimbali.
"Tanga ni mfano mzuri wa ushirikiano wa pande mbili za muungano kwani ni soko kuu la vyakula vya wakazi wa Zanzibar ambapo kila Jumapili ya kila wiki huwasili meli inayowaleta wafanyabiashara wa Zanzibar kununua vyakula na bidhaa mbalimbali...hivyo soko hili litarahisisha"amesema Balozi Dkt Burian.
Amesema mbali ya kutoa fedha za kuendesha miradi ya aekta ya elimu,afya, miundombinu,Serikali imetumia sh 429.Bilioni kuboresha bandari ya Tanga.
"Tulikuwa tukipokea meli chache lakini baada ya maboresho ndani ya miezi mitano bandari ya Tanga imepokea zaidi ya meli 150 ikiwa ni matunda ya uwekezaji mkubwa wa Serikali katika uboreshaji wa bandari hii"amesema Balozi Dkt Burian.
Akizungumzia baada ya kukagua ujenzi wa soko hilo, Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Zuberi Ali Maulid amewataka wakazi wa Tanga kuuenzi Muungano kwa kuwa una manufaa makubwa Kwa wananchi wa Tanzania Bara na Zanzibar.
"Tuendelee kuuenzi Muungano wetu ulioasisiwa na wazee wetu kwani una manufaa makubwa kwa wananchi wa pande zote mbili...kule Unguja Kaskazini Nungwi wapo watu kutoka Tanga na wengine kutoka kila Mkoa huku Bara halikadhalika na huku kuna wengi mno wa kutoka Unguja na Pemba"amesema Spika Maulid.
No comments:
Post a Comment