KAMPUNI ZA MWIBA HOLDINGS NA GRUMETI RESERVES WAPEWA VYETI VYA UWEKEZAJI. - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Friday, 1 April 2022

KAMPUNI ZA MWIBA HOLDINGS NA GRUMETI RESERVES WAPEWA VYETI VYA UWEKEZAJI.


Watendaji wa kampuni ya Mwiba Holding wakipewa cheti cha uwekezaji na Aliyekuwa Waziri wa maliasili na utalii Dk Damas Ndumbaro.

Viongozi mbali mbali wa mwiba holding wakiwa katika picha ya pamoja na aliyekuwa waziri wa maliasili na utalii Dr. Ndumbaro



Na: MAIPAC TEAM.

Aliyekuwa Waziri wa Maliasili na Utalii Dk Damas Ndumbaro amesema serikali itaendelea kuweka mazingira wezeshi kwa wawekezaji wa sekta ya utalii na kuboresha huduma za upatikanaji wa leseni kwa uharaka zaidi pamoja na mifumo ya malazi.

Amesema Wizara ya Maliasili na Utalii itaendelea kutoa fursa katika maeneo yaliyohifadhiwa kwa Wawekezaji wa Ndani na Nje ya nchi kwa kuzingatia maslahi mapana ya nchi

Amesema hayo leo Alhamisi Machi 31Jijini Dar Es Salaam wakati akikabidhi vyeti kwa wawekezaji  wa Kampuni za Grumeti Reserves Ltd na Mwiba Holding Ltd waliokidhi vigezo na kufanikiwa kupata maeneo ya uwekezaji mahiri ya Wanyamapori (SWICA)yanayosimamiwa na Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA).

Amewasisitiza wawekezaji wazawa na wa kigeni kulinda na kutangaza utalii na maeneo ya uhifadhi na vivutio hapa nchini, katika maeneo waliyopewa kuwekeza kwa kushirikiana na serikali,huku akihamasisha wawekezaji wa kigeni kuwekeza hapa nchini kwa kuwa Tanzania ni salama.

“Sisi Kama Wizara ya Maliasili na Utalii, falsafa yetu ni moja tu, mteja ni mfalme ndio maana mimi, Naibu Waziri, Katibu Mkuu na Naibu Katibu Mkuu, tuko tayari kukutana na mwekezaji wa aina yoyote yule, muda wowote ule kujadili changamoto zozote zile, milango iko wazi”amesema.

Waziri huyo ameipongeza TAWA kwa kazi kubwa wanayoifanya ya kulinda na kuhifadhi rasilimali za Taifa licha ya kuwa taasisi hiyo ni changa kuliko Taasisi zingine lakini wanafanya kazi kubwa katika mazingira magumu.

 Mwenyekiti wa bodi ya Wakurugenzi TAWA,Meja Jenerali Mstaafu Hamis Semfuko, ameishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan na Wizara ya Maliasili na Utalii, kwa kuipatia TAWA fedha zaidi ya Sh12.9 bilioni kwa ajili ya kutekeleza miradi ya miundombinu ya Utalii kupitia kampeni ya Maendeleo ya Ustawi wa Taifa na Mapambano Dhidi ya UVIKO-19.

Amesema miradi  hiyo inaendelea kutekelezwa katika maeneo mbalimbali ikiwemo kwenye maeneo ya SWICA huku akithibitisha kuwa TAWA imeweka mipango madhuhuti,itahakikisha miradi yote ambayo imekusudiwa kutekelezwa kwa kutumia fedha hizo inatekelezwa ndani ya muda uliopangwa na kwa ubora uliokusudiwa.


Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Mwiba Holding Ltd, Jean Claude McMenamin alishukuru Serikali kwa juhudi inazofanya kuhakikisha shughuli za Uhifadhi zinaleta tija kwa taifa  kwa kuhakikisha Uhifadhi unaimarika kwa kuleta faida ya moja kwa moja kwa maisha ya wananchi kwa kupitia uwekezaji huo wa muda mrefu.

Mwiba imekuwa ikifanya utalii  wa picha na  kuvutia mamia ya watalii  kutokana na uhifadhi mzuri wa eneo lake.


Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Grumeti Reserves Ltd, Mr Graham Ledger amesema kampuni ya Grumeti inashukuru kupata cheti cha umiliki wa Vitalu viwili kwa sasa na  inaahidi kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika kulinda na kuendeleza shughuli za Uhifadhi nchini.
 

 

No comments: