New

Mkufunzi Mussa Juma akitoa mafunzo kwa wanahabari juu ya usalama wa matumizi ya mitandao ili kuwa salama na kulinda kazi zao zisidukuliwe.
Na: Marco Maduhu, DODOMA
WAANDISHI wa habari 20 kutoka mikoa mbalimbali hapa nchini, wamepewa mafunzo ya usalama mitandaoni, pamoja na kuzingatia usalama wao hasa wanapokuwa wakitekeleza majukumu yao.
Mafunzo hayo yameanza kutolewa leo Mei 30, 2022 Jijini Dodoma ambayo yatahitimishwa kesho, na yanaendeshwa na Umoja wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC) kwa kushirikiana na International Media Support.
Akizungumza kwenye mafunzo hayo Mratibu wa mafunzo kutoka (UTPC) Victor Maleko, amesema yatatolewa kwa waandishi wa habari 100 kutoka klabu za waandishi wa habari, na mpaka sasa yameshatolewa kwa waandishi 80.
Amesema lengo la mafunzo hayo ni kuwaweka waandishi wa habari katika hali ya usalama katika ulimwengu huu wa digital hasa wanapokuwa wakitekeleza majukumu yao.
“Mafunzo haya ya usalama wa kimtandao kwa waandishi wa habari (Digital Security and Safe Journalist)yanatolewa na umoja wa klabu za waandishi wa habari Tanzania (UTPC) kwa kushirikiana na International Media Support na yatatolewa kwa waandishi 100,”amesema Maleko.
Kwa upande wake Mkufunzi wa mafunzo hayo Mussa Juma, ambaye pia ni mkurugenzi mtendaji wa MAIPAC amewataka waandishi wa habari hapa nchini, wawe makini sana na ulimwengu huu wa digital kwa kuhifadhi kazi zao katika hali ya usalama, kwa kuweka Nywila ambazo ni bora zaidi (Strong Password) ili kutodukuliwa kazi zao na kuwa salama.

No comments:
Post a Comment