AFUNGWA JELA MAISHA BAADA YA KUMBAKA MTOTO WA MIAKA 8 - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Saturday, 18 February 2023

AFUNGWA JELA MAISHA BAADA YA KUMBAKA MTOTO WA MIAKA 8





NA: MWANDISHI WETU

maipacarusha20@gmail.com
 

Mahakama ya Wilaya ya Arusha, imemhukumu kifungo cha maisha gerezani, Kelvin Laizer (19), baada ya kupatikana na hatia ya kumbaka mtoto wa kike mwenye umri wa miaka minane.


Laizer ambaye ni mkazi wa eneo la Muriet, jijini Arusha amehukumiwa adhabu hiyo Ijumaa Februari 17, 2023 na Hakimu Mkazi, Pamela Meena baada ya kumtia hatiani kwa kosa hilo la kumbaka mtoto huyo kwa nyakati tofauti.


Akisoma hukumu hiyo, Hakimu huyo amesema mahakama imemtia hatiani mtuhumiwa huyo aliyekuwa anakabiliwa na kosa la ubakaji kinyume na Kanuni ya adhabu iliyofanyiwa marejeo mwaka 2019.

 Amesema katika kesi hiyo ya jinai namba 75/2022, upande wa jamhuri umeweza kuthibitisha kosa hilo pasipo na shaka kupitia mashahidi wake wanne ikiwemo mtuhumiwa huyo kuthibitika kumbaka mtoto huyo ambaye ni mwanafunzi wa darasa la nne kwa nyakati tofauti kati ya Januari hadi Machi 21, 2022.

 "Kutokana na ushahidi wa upande wa mashtaka ulionyesha mshtakiwa alikuwa na tabia ya kumbaka mara kwa mara mhanga hadi alipokutwa naye katika kibanda cha movie eneo la Muriet-Patel.

"Na hilo lilithibitishwa na mashahidi waliotoa ushahidi mahakamani akiwemo daktari aliyemfanyia uchunguzi mhanga, mahakama imeridhika kesi dhidi ya mshtakiwa imethibitishwa bila kuacha shaka lolote hivyo mahakama imemtia hatiani mshtakiwa na kumpa adhabu ya kifungo cha maisha jela," amesema.

Awali, Wakili wa Serikali Grace Madikenya aliomba mahakama itoe adhabu kali kwa mshitakiwa huyo ili iwe fundisho kwa vijana wengine kwani hilo limekuwa kosa linalofanywa na vijana wengi kwa watoto wadogo mkoani hapa.

 

credit: gazeti mwananchi 

No comments: