Serikali Yaanza Kukabiliana na Mmomonyoko wa Maadili Nchini - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Friday 24 February 2023

Serikali Yaanza Kukabiliana na Mmomonyoko wa Maadili Nchini

 

 

Na Eleuteri Mangi, WUSM, Dodoma

 maipacarusha20@gmail.com

Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo imeanza kutekeleza agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan la kuhamasisha wadau wa malezi na makuzi ya watoto na vijana kuwajibikaji katika malezi ili kukabiliana na hali ya mmomonyoko wa maadili nchini.

 

Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Utamaduni kutoka Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Julieth Kabyemela amesema hayo Februari 23, 2023 alipokuwa akiwasilisha mada ya Wajibu wa Viongozi wa Dini katika kukabiliana na hali ya mmomonyoko wa maadili nchini kwa viongozi wa kanisa la Tanzania Assembly’s of God (TAG) jimbo la Dodoma Kati.

 

“Jamii kutokuwa na hofu ya Mungu ni sababu kubwa ya tatizo la mmomonyoko wa maadili nchini, hali hii inatokana na muingiliano wa tamaduni za jamii mbalimbali ambayo inasababishwa na ukuaji wa maendeleo ya sayansi na teknolojia, wazazi/walezi kuona fahari mtoto anavaa nguo zisizo na staha, kutafuta pesa na kusahau kusimamia watoto badala yake wanalelewa na wasichana wa kazi pamoja na utandawazi ambao sasa hivi vinaleta changamoto kubwa katika suala la malezi na makuzi ya watoto wetu” amesema Dkt. Kabyemela.

 

Amesema kuwa Wizara hiyo imejipanga kutekeleza agizo hilo la Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ambalo mara kwa mara linasisitizwa na Makamu wa Rais Dkt. Philip Mpango na Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa kuwafikia makundi mbalimbali ambayo ni msingi wa malezi.

 

Makundi hayo ni pamoja na viongozi wa dini ambao wanawajibu wa kuwhamasisha wazazi na walezi kutekeleza wajibu wao wa kuwalea watoto katika maadili ya Mtanzania, Dkt. Kabyemela anasema ndiyo maana tupo hapa kuwakumbusha na kuona kwa pamoja namna ya kulinusuru taifa kutoka katika dimbwi la mmomonyoko wa maadili.

 

Dkt. Kabyemela amewataja wadau wengine ambao watafikiwa na Wizara hiyo kuwa ni Wasimamizi wa taasisi zinazotoa mafunzo kuanzia shule za msingi, sekondari, vyuo, wakuu wa shule, wanafunzi wa shule za msingi, sekondari, vyuo, kamati ya ulinzi na usalamam waandishi wa habari, wasanii pamoja na wamiliki wa vituo vya kutoa mafunzo na kulea watoto.

 

Dkt. Kabyemela ameongeza kuwa mmomonyoko wa maadili ni kutokuzingatiwa kwa utaratibu wa maisha unaokubalika katika taifa ambao limejiwekea na madhara yake ni makubwa kwa jamii na hivyo kuathiri kuongezeka kwa vitendo vya ushoga, uasherati na uzinzi, wizi, ulevi, uvutaji bangi na matumizi ya dawa za kulevya ambavyo hivyo ni chukizo kwa Mungu.

 

Kwa upande wake Kiongozi wa Kanisa la kanisa la Tanzania Assembly’s of God (TAG) jimbo la Dodoma Kati Askofu Steven Mahinyila amesema kuwa nafasi ya viongozi wa dini katika kukabiliana na mmomonyoko wa maadili nchini ni kuweka utaratibu wa kufundisha vijana katika makundi rika na kufanya ufuatiliaji wa karibu kwa lengo la kuhakikisha yanayofundishwa makanisani yanatekelezwa.

 

Naye Mchungaji Marcel Paul wa kanisa hilo eneo la Mipango karibu na makaburi ya wahanga wa ajili ya treni Dodoma amemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na serikali yake kwa kuweka Wizara ambayo yeye anaguswa nayo kwa namna wanavyoifikia jamii mpaka kwenye meneo ya ibada na kuongeza kuwa Serikali imewaunga mkono na milango ipo wazi ili waendelee kushirikiana katika kusaidia kuelimisha jamii juu ya maadili.

 

“Nimetiwa nguvu mpya ya kuingia kwenye maeneo ambayo ninawakuta watoto wakiwa kwenye mazingira hatarishi, watoto wengi wapo mitaani, shule za msingi, sekondari na hata vyuo. Sasa kule tunahitaji kuingia kwenye vipindi vya dini ili tupeleke hii elimu” amesema Mchungaji Marcel.

 

Mkutano huo ni wa siku mbili ambao umeanza 21 hadi 23, 2023 na kuhudhuriwa na wachungaji wapatao 120 kutoka wilaya za Dodoma, Bahi na Chamwino.

 

No comments: