Wakamatwa baada ya kuuwa Twiga wa MILION 35 - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Wednesday, 22 February 2023

Wakamatwa baada ya kuuwa Twiga wa MILION 35

 

Watuhumiwa wa ujangili wa Twiga, Masiali Kipara na Paulo Richard wakiwa chini ya Ulinzi wa askari wa Wanyamapori baada ya kukamatwa eneo la Jumuiya ya hifadhi ya Wanyamapori ya Burunge wilaya ya Babati



NA: Andrea Ngobole, MAIPAC

maipacarusha20@gmail.com


Watu wawili Wakazi wa kijiji cha Minjingu, wilaya ya Babati mkoa wa Arusha, Masiali Lais Kipara(19) na Paulo Richard(23) wamekamatwa baada ya kuwinda Twiga Ili wauze Nyama yake .


Nyama ya Twiga imekuwa ikiuzwa kati ya sh 5000 hadi 10000 kwa kilo na wawindaji haramu katika mji wa Magugu.


Biashara hiyo  inafanyika baada ya majingili kufanikiwa kuuwa Twiga ambao wapo wengi katika eneo la Jumuiya ya Hifadhi ya Wanyamapori ya Burunge ambayo ipo kati kati ya hifadhi ya Taifa ya Tarangire na hifadhi ya Taifa ya Manyara.


Watuhumiwa hao wa ujangili walikamatwa  katika eneo la jumuiya ya hifadhi ya wanyamapori ya Burunge, (Burunge WMA) na askari wa wanyamapori, askari wa Jumuiya ya  hifadhi ya Wanyamapori ya Burunge kwa kushirikiana na Askari wa taasisi ya chem chem ambayo imewekeza katika eneo hilo.


Kamanda wa polisi mkoa wa Manyara, George  Katabazi amethitisha  Leo February 22,2023 kukamatwa watuhumiwa  hao na kueleza amesema, Twiga aliyeuawa alikuwa na  kilo 54.5  mwenye thamani ya shilingi 35.1 milioni na  alikutwa tayari ameuawa.


Amesema watuhumiwa hao wanatarajiwa kufikishwa mahakamani wakati wowote kwani upelelezi wa shauri lao umekamilika.


Askari wa Wanyamapori ambaye aliongoza operesheni kukamamata watuhumiwa hao, Samweli Bayo,akiwa doria na askari wenzake wa Burunge WMA na Chemchem, alisema waliwakuta watuhumiwa na nyama hiyo, wakijipanga kuanza kuchuna ili wakauze.


Bayo amesema tukio hilo lilitokea February 14, saa 11 jioni na  walifanikiwa kuwakamata watuhumiwa hao, wakiwa porini na watuhumiwa wengine wawili walikimbia.

Afisa Idara ya kupambana na ujangili Taasisi ya Chem chem Erick Nyman kushoto akizungumza na waandishi wa habari 


Afisa Idaya ya kupambana na ujangili wa taasisi ya Chemchem association ambayo imewekeza Utalii wa picha na hoteli katika eneo hilo, Erick Nyman amesema kukamatwa kwa watuhumiwa hao ni jitihada za ulinzi shirikishi.


Amesema wamekuwa wakifanya doria  ya pamoja baina ya askari wa Mamlaka ya usimamizi wanyamapori(TAWA) Askari wa wanyamapori wilaya ya Babati, askari wa Chemchem na askari wa Burunge WMA


Nyman amesema  taasisi hiyo kwa mwaka imekuwa ikitumia zaidi ya sh 400 milioni katika harakati za kupambana na ujangili katika eneo hilo la Burunge WMA  kutokana na kushamiri matukio ya ujangili ukiwepo wa Twiga na wanyama wengine kwa ajili ya kitoweo.

Katika eneo hilo la Jumuiya ya hifadhi ya Wanyamapori ya Burunge kumekuwepo na matukio kadhaa ya ujangili wa Twiga na wanyama wengine kwa ajili ya Kitoweo.

Chanzo Cha ujangili kinatajwa na Wananchi kujenga ndani ya maeneo ya mapito ya Wanyamapori na hivyo imekuwa rahisi kuwawinda nyakati jioni.

Hata hivyo tayari Wizara ya Maliasili na Utalii ilianza operesheni ya kupima Ili kutenga maeneo ya mapito ya Wanyamapori katika eneo hilo la Ushoroba wa kwakuchinja

Tayari kaya zaidi ya 200 zimebainika kuishi mfano ya eneo la Mapito ya wanyamapori na kaya nyingine kufungua mashamba.



No comments: