Wapandishwa kuzimbani kwa tuhuma za kuuwa Twiga ili kuuza nyama - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Friday 24 February 2023

Wapandishwa kuzimbani kwa tuhuma za kuuwa Twiga ili kuuza nyama

 

Watuhumiwa waliopandishwa kizimbani


Mwandishi wetu, Babati 

maipacarusha20@gmail.com

Wakazi wawili wa kijiji cha Minjingu, wilaya ya Babati mkoa wa Manyara, wamefikishwa mahakama ya hakimu mkazi mkoa wa Manyara  kwa tuhuma za kupatikana na nyara za serikali, Twiga mdogo huku wakiwa wamemkata mguu mmoja.


Watuhumiwa hao ni Masiali Lais Kipara(19) na Paulo Richard(23) ambao pia walikamatwa na visu aina ya sime vitatu na Mkuki mmoja .


Mwendesha mashitaka wa  Polisi, Mkaguzi Msaidizi wa polisi, Obedi Machumu mbele ya hakimu mkazi wa mahakama ya mkoa Manyara, John Masao alisema, watuhumiwa hao, walikamatwa Februari 14,2023 saa 11 jioni katika eneo la jumuiya ya hifadhi ya wanyamapori ya Burunge.


Alisema  watuhumiwa hao, walikamatwa na  askari wa wanyamapori, kwa kushirikiana na askari wa Jumuiya ya  hifadhi ya Wanyamapori ya Burunge kwa kushirikiana na Askari wa taasisi ya chem chem.


Alisema watuhumiwa hao, walikutwa na   Twiga huyo mdogo mwenye kilo 54.5 ambaye tayari walikuwa wamemuua mwenye thamani y ash 35.1 milioni  mali ya serikali kinyume ya sharia ya umiliki wa nyara za taifa na uhujumu uchumi.


Machumu amesema katika kosa jingine watuhumiwa hao, wamekutwa na sime tatu na mkuki katika mazingira ya kutatanisha ambavyo wametuhumiwa kufanya uhalifu.


Hata hivyo, watuhumiwa hao, baada ya kuhojiwa na Hakimu, Masao kuhusiana na Mashitaka hayo, Mshitakiwa wa kwanzxa Kipara, alikiri na mshitakiwa wa pili alikana kosa hilo.


Hata hivyo, Hakimu Mkazi Masao, alimtaka Mwendesha mashitaka, Machumu  kuwasomea maelezo ya awali watuhumiwa hao.


Alisema Februari 14, 2011 askari wa wanyamapori  Samweli Daudi  Bayo na James Lesuka na Michael Mbilinyi wakiwa kwenye doria ya kawaida katika eneo  la Burunge WMA, waliwakamata watuhumiwa hao, wakiwa na nyama ya Twiga huyo, mdogo wakiwa tayari wamemkata mguu mmoja.


Kipara alikana maelezo hayo na  alieleza mahakama kuwa siku ya tukio yeye alikuwa akiogelewa mtoni na hakuuwa Twiga bali walioua ni watu wawili ambao walikimbia ambapo pia alikana kumiliki sime na mkuki.


Mtuhumiwa wa pili pia alikana maelezo siku ya tukio na kueleza alikamatwa akiwa anaelekea nyumbani akitoka kuchunga Ng’ombe.


Mtuhumiwa huyo, pia alikana kumiliki sime na mkuki ambavyo vilikamatwa katika operesheni hiyo.


Baada ya maelezo hayo, upande wa mashitaka ulieleza una mashahidi sita na  vielelezo vitano na kuomba mahakama ikubali shahidi wa kwanza, Sajenti  James(45) kutoa ushahidi wake.


Akitoa ushahidi wake, Sajenti  James alisema mnamo Februari 14, saa 1:30 usiku akiwa kama mtunzaa vielelezo katika kituo cha Polisi Babati alikabidhiwa  nyama ya Twiga, Mkuki na Sime tatu kama vielelezo.


Amesema  vifaa hivyo, alikabidhiwa na afisa Wanyamapori Samweli Bayo kwa ajili ya ushahidi katika shitaka hilo.


Mwendesha mashitaka Machumu, aliomba mahakama kupokea vifaa hivyo kama vielelezo na baadaye aliomba mahakama kuona vyama ya Twiga iliyokamatwa  ili baadaye iteketezwe kutokana na kuanza kuharibika.


Hakimu Masao, alikubaliana na maombi hayo na kutoka nje ya mahakama kushuhudia vielelezo hivyo na baadaye kuagiza kuteketezwa nyama hiyo porini.


Washitakiwa hao, hata hivyo, hawakuwa na pingamizi kuhusiana na kupokelewa vielelezo hivyo na kuteketezwa nyama hiyo.


Hakimu Masao alisema dhamana ya watuhumiwa hao, ipo wazi lakini wanatakiwa kuwa na wadhamini wenye mali ambayo haihamishiki yenye thamani ya zaidi ya milioni 10 namdhamini mmoja mmoja ambao pia watasaini dhamana hiyo.


Kesi hiyo, imeahirishwa hadi Februari 28 na watuhumiwa hao walirudishwa mahabusu ili kukamilisha taratibu za dhamana.


MWISHO.

No comments: