CHONGOLO AKAGUA JENGO LA TANZANITE CITY MIRERANI - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Wednesday 8 March 2023

CHONGOLO AKAGUA JENGO LA TANZANITE CITY MIRERANI

 

KATIBU Mkuu wa CCM Daniel Chongolo akipewa maelezo juu ya jengo la Tanzanite City.


Na Mwandishi wetu, Mirerani 

maipacarusha20@gmail.com

KATIBU Mkuu wa CCM Daniel Chongolo amekagua ujenzi wa mradi wa jengo la soko la madini Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara (Tanzanite City) na kupongeza hatua iliyofikiwa.


Chongolo akizungumza Machi 8 wakati akikagua jengo hilo amesema Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan imetoa fedha za kujenga jengo hilo.


"Jengo lilikamilika wafanyabiashara wataingia kufanya kazi na kusababisha mji mdogo wa Mirerani kuchangamka zaidi kiuchumi," amesema go Chongolo.


Meneja wa shirika la Nyumba la Taifa (NHC) Mkoa wa Kilimanjaro, Juma Kiaramba akisoma taarifa ya utekelezaji wa mradi huo wa ujenzi wa jengo la soko la madini  Mirerani amesema utagharimu shilingi 5,494,724,533.28.


Kiaramba amesema mkataba huo ni wa miezi 15 kuanzia Machi 2022, usanifu umeanza Machi 22 na ujenzi ukaanza Mei 22 mwaka 2022 na unatarajiwa kukamilika Mei 21 mwaka 2023.


Amesema usanifu ni wa ghorofa tano ila ujenzi kwa awamu ya kwanza ni ghorofa tatu, hata hivyo mazungumzo yamefanyika kati ya mkandarasi na Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro ambapo  shirika litajenga ghorofa ya chini na ghorofa nne na kufanya umaliziaji wote wa sakafu ya chini kufanya baadhi ya kazi kubwa katika sakafu ya kwanza kwa gharama ile ile ya awali.


"Kazi zilizokamilika ni pamoja na maandalizi yote muhimu ya awali yanayohitajika kabla ya ujenzi kuanza, ujenzi wa sakafu mbili za awali na upigaji wa plasta kwa sakafu ya kwanza kwa ndani umekamilika," amesema Kiaramba.


Ametaja kazi zinazoendelea ni ukamilishaji wa ujenzi wa sakafu ya tatu, manunuzi na kuhakiki vifaa vyote muhimu vya ujenzi vinavyohitajika, ujenzi wa ukuta wa tofali wa sakafu ya kwanza na ujenzi wa ukuta wa nje kuzunguka jengo.


Amesema kupanda kwa bei za vifaa vya ujenzi kila mara ni moja ya changamoto za kuongezeka kwa gharama za ujenzi kwa upande wa shirika.


Amesema katika kujikwamua na changamoto hiyo shirika limekuwa likifanya manunuzi pamoja moja kwa moja kwenye maeneo ya uzalishaji.


Amesema hali hiyo imelenga kuzuia ucheleweshaji kazi unaoweza kusababisha ongezeko zaidi ya gharama za ujenzi.


"Ni matarajio ya shirika kuwa litakamilisha mradi huu muhimu kwa wakati na kwa kiwango tarajiwa kwa ushirikiano na mshitiri, ofisi ya DED Simanjiro na Mkoa wa Manyara kwa ujumla," amesema Kiaramba.



No comments: