Dkt. JAFO AWAPONGEZA KIWANDA CHA A TO Z KWA KUKAMILISHA MTAMBO WA KUCHAKATA MAJI MACHAFU - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Thursday 2 March 2023

Dkt. JAFO AWAPONGEZA KIWANDA CHA A TO Z KWA KUKAMILISHA MTAMBO WA KUCHAKATA MAJI MACHAFU



WAZIRI wa Nchi ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Dkt. Selemani Jaffo, amekipongeza kiwanda cha kutengeneza nguo na chandarua chenye dawa cha A to Z kwa kujali afya za wakazi wanaozunguka kiwanda hicho baada ya kukamilisha mtambo wa kuchakata maji machafu yanayozalishwa na kiwanda hicho.




Waziri wa nchi ofisi ya Makamu wa Rais, Selemani Jaffo mwenye suti ya blue akifanya ukaguzi wa mtambo mpya wa kuchakata maji machafu ndani ya kiwanda cha ATOZ kabla ya kuruhusiwa kuelekea kwenye makazi ya watu.


Akizungumza jana kiwandani hapo alipotembelea kutaka kujua hatua iliyofikiwa na kiwanda hicho, Waziri Jaffo amesema kiwanda cha AtoZ ni kiwanda cha mfano kwa kuwa kimeweza kutekeleza agizo lililotolewa na Serikali kupitia kwa Naibu Waziri wa Wizara hiyo kuhusu kukamilisha mchakato wa ujenzi wa mtambo huo.


Amesema afya za wananchi ndio jambo la kwanza kabisa kuangaliwa na Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan hivyo baada ya kuwepo kwa malalamiko ya uwepo wa maji yasiyosalama amelazimika kutembelea na kushuhudia mwenyewe ukweli kuhusu malalamiko hayo.


"Nikiwa Dodoma nilipokea malalamiko kuwa mnatiririsha maji machafu, nikasema nije mwenyewe hapa kushuhudia maagizo tuliyotoa kama mmeyatekeleza, nimefurahi sana kuona mmemaliza mtambo huu na mmenihakikishia maji mnayotoa ni salama na watu wangu wa NEMC wamethibitisha hilo,"amesema.


Hata hivyo ameuagiza uongozi wa NEMC Kanda ya Kaskazini kuendelea kuchukua vipimo vya mara kwa mara vya maji yanayotiririshwa ili kujiridhisha kuwa maji hayo hayana kemikali mbaya ambazo zinaweza kuleta madhara kwa binaadam.


Waziri Jaffo ameutaka uongozi wa ATOZ kutoiga baadhi ya viwanda ambavyo vimekuwa vikitumia mwanya wa kutiririsha maji kwenye mfumo wa maji taka na kutitirisha maji machafu jambo ambalo ni hatari sana kwa afya za binaadam.


"Kuna baadhi ya viwanda Jijini Dar es salaam vimekuwa vikidanganya kusafisha maji yake ya viwanda na badala yake vimekuwa vikitiririsha maji machafu kwa siri na kuyaingiza kwenye mabwawa yaliyotengwa hadi hapo walipobainika, nawaombeni sana msifanye hivyo,"alisema Jaffo.


Akijibu hoja hiyo, Mkurugenzi wa uzalishaji wa kiwanda cha A to Z Binesh Haria alimuhakikisha Waziri Jaffo kuwa hali hiyo haitaweza kutokea kwa kuwa kiwanda hicho kimekuwa kikifanyakazi kupitia tenda za kimataifa na zimekuwa zikiangalia sana suala la mazingira na afya za binaadam lakini pia ujenzi wa mtambo huo umegharimu fedha nyingi hivyo kiwanda hakitakubali kuharibu hadhi yake.




Meneja usalama na mazingira Harrison Rwehumbiza akitoa maelekezo kwa Waziri Jaffo



Akitoa taarifa ya hali ya ufanyaji kazi wa mtambo huo kwa waziri, Meneja usalama na mazingira wa kiwanda cha ATOZ, Mhandisi Harrison Rwehumbiza amesema mtambo huo unafanyakazi saa 24 kwa kuwa kiwanda hicho kimekuwa kikizalisha kwa mfumo huo.



Amesema mtambo huo umekamilika kwa asilimia 98 na kinachosubiriwa hivi sasa ni Mamlaka ya Maji safi na Taka Arusha (AUWSA), kufikisha miundo mbinu yao karibu na kiwanda hicho kwaajili ya kuchukua maji hayo ili kuondokana na mtindo wa sasa wa kuyaachia moja kwa moja mtoni.

Meneja Usalama na Mazingira Mhandisi Harrison Rwehumbiza akitoa maelekezo ya namna mtambo wa kuchakata maji machafu uanvyoyasafisha hadi kufikia hatua ya mwisho kwa Waziri Selemani Jaffo, wa kwanza kulia nyuma ni Mtendaji Mkuu wa ATOZ Kalpesh Shah na aliyevaa shati jeupe ni Mkurugeni Uzalishaji, Binesh Harria


Waziri wa Nchi ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira na Muungano Selemani Jaffo akizungumza na uongozi wa kiwanda cha ATOZ baada ya kushuhudia mazingira rafiki yaliyopo ndani ya kiwanda cha ATOZ kuhakikisha afya za wananchi wanaozunguka kiwanda zinakuwa salama wakati wote



No comments: