Madini ya Tanzanite yanayopatika NCHINI TANZANIA tu KATIKA eneo la Mererani MKOANI MANYARA |
Mmiliki WA MGODI WA uchimbaji madini ndugu Miroshi akionesha eneo la MGODI wake aliodhulumiwa |
Na Mwandishi wetu Mererani.
maipacarusha20@gmail.com
Mgogoro wa umiliki wa mgodi wa madini ya Tanzanite uliokuwa unamilikiwa na Mchimbaji mdogo Patrick Miroshi na baadae kuuziwa mfanyabiashara maarufu jijini Arusha, Japhet Lema umetinga taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa(TAKUKURU) na leo mgodi huo utapimwa upya kujua nani ni mmiliki halali.
Hatua hii, imekuja takriban wiki moja tangu, Miroshi kumuomba Rais Samia Suluhu kumsaidia kurejeshewa mgodi wake wenye leseni namba PML 000943NZ, ambao amekuwa akiuchimba tangu mwaka 2012 na mfanyabiashara huyo alikuwa akimfadhili.
Akizungumza na vyombo vya Habari jana Miroshi alisema anamshukuru Rais Samia Suluhu kutuma maafisa wake kushughulikia suala lake na LEMA.
"Baada ya maombi yangu kwa Rais, Maafisa wa TAKUKURU wameniita na nimewapa maelezo yangu yote na nyaraka zote na wameahidi kulifanyia kazi suala langu"alisema
Mchimbaji mdogo WA Madini mererani ndugu Patrick Miroshi akiwa KATIKA eneo la uchimbaji madini hayo ya Tanzanite |
Alisema pia anashukuru machi 17 mwaka huu, , aliitwa na maafisa wa madini Mererani, ambapo walikwenda kupima upya mgodi na ilithibitika mgodi ambao amemilikishwa mfanyabiashara huyo ni mali yake.
"Tulikwenda na maafisa madini, wakiongozwa na Afisa madini mkazi Mererani, Menard Msengi na mpimaji migodi Elias Azaria na mashahidi wa pande zote na baada ya kupima mgodi ilithibitika mgodi upo ndani ya leseni yangu"alisema
Afisa madini Mkazi wa Mererani, Msengi alikiri ofisi yake kuanza kushughulikia mgodi huo na walipima mgodi katika hatua za awali hata hivyo mfanyabiashara Lema alipinga matokeo ya vipimo hivyo.
Msengi alisema leo watakwenda tena kupima tena mgodi huo, kwa kutumia wapimaji kutoka Wizarani ili kuona haki ipo wapi kwani inaonekana mgodi kuwa kati kati ya leseni mbili.
"Kesho(leo) tutapima kujua eneo kubwa la mgodi lipo wapi na baada ya hapo tutakuwa katika mazingira mazuri ya kuzungumza"alisema
Kabla ya mgogoro huu, Miroshi alikuwa amesaini mkataba na mfanyabiashara huyo Lema ambaye ni maarufu kwa jina la Njake, Julai 5, mwaka 2018 kumfadhili kushirikiana kuchimba madini katika mgodi huo,
Hata hivyo, alisema mfadhili huyo, baada ya kuchimba kwa miaka miwili, alianza kushinikiza kuwa mmiliki mwenza jambo ambalo alikataa na mgogoro kufikishwa chama cha wachimbaji madini mkoa Manyara na baadaye wizara ya madini bila ya kupata suluhu.
Hata hivyo, alisema, alishangazwa Februari 13, mwaka huu, maafisa wa madini kutoka wizara ya madini, kufika katika mgodi wake na kumweleza kuwa amekuwa akichimba kwa miaka 11 eneo ambalo sio lake na wakamuonesha eneo la pembeni na mgodi wake kuwa ndilo lake
Mfanyabiashara Lema, alikiri kuwa alikuwa na mkataba wa miaka 10 kuchimba madini katika mgodi huo wa Miroshi na kueleza ameuziwa mgodi huo na Angoshi Selemani na Omari Masanyika wenye namba PML 00416 SMN.
No comments:
Post a Comment