TANZANIA NA MAREKANI ZAKUBALIANA UWEKEZAJI MKUBWA KWENYE UTALII NCHINI. - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Friday, 24 March 2023

TANZANIA NA MAREKANI ZAKUBALIANA UWEKEZAJI MKUBWA KWENYE UTALII NCHINI.




Na: Mwandishi wetu

maipacarusha20@gmail.com

Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mohamed Omary Mchengerwa leo Machi 23, 2023 amekutana na ujumbe wa Serikali ya Marekani ulioongozwa na  Balozi wa Marekani  hapa nchini,  Mhe. Michael Battle na kukubaliana kusaini mikataba  ya  kufanya uwekezaji mkubwa kwenye Sekta ya Utalii hapa nchini.


Mazungumzo hayo yamefanyika katika ofisi za Wizara hiyo zilizopo  jijini Dodoma ambapo pande zote mbili zimekubaliana kuisaini mikataba  hiyo  baada ya kuweka sawa maeneo machache ya mikataba hiyo ambayo pande hizo zilikuwa zikivutana.



 Aidha,  katika  kikao hicho ambacho kilihudhuriwa pia na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dkt. Hassan Abbasi pande zote zimekubaliana  kuyapitia maeneo hayo kwa haraka ili iweze kusainiwa katika  muda mfupi ujao.


"Nina furaha kuona kuwa kimsingi tumekubaliana mambo ya  uwekezaji mkubwa, kuna mambo machache  tu tumevutana kidogo kwa manufaa ya nchi yetu ambayo pia tumekubaliana kila pande iende  kuweka vizuri ili tukamilishe zoezi hili kwa wakati." Amesisitiza Mhe. Mchengerwa


Akifafanua, Mhe. Mchengerwa amesema katika kikao hicho pia  wamejadiliana kuhusu  namna gani wawekezaji kutoka Marekani watawekeza nchini  katika maeneo  yaliyohifadhiwa  yanayosimamiwa  na Wizara ya Maliasili na Utalii.


Ameongeza kuwa tayari Wizara imeipatia Serikali ya Marekeni vipaumbele vya Taifa ili iweze kujipanga vizuri katika eneo la kuwekeza katika Sekta ya Utalii hapa nchini.


Amesema imani waliyonayo kama Serikali endapo wakifanikiwa tukiondoa kero chache zilizopo  katika mkataba,  Serikali itaweza kuingiza  fedha nyingi kupitia Sekta ya Utalii kuliko kipindi chochote.


Akifafanua zaidi amesema " kwa sasa ni takribani  dola milioni 1.5  zinazoingizwa kutokana na utalii kwa lakini baada ya kuridhiana na kuingiza kwenye mikataba hiyo Serikali itaweza kuingiza hadi  dola milioni 11  katika kipindi cha mwaka mmoja".


Aidha, amepongeza kazi kubwa iliyofanywa na  Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan ya kuitangaza Tanzania kupitia Filamu ya Royal Tour ambapo amesisitiza kuwa kutokana  na kazi kubwa aliyoifanya na Rais wa Tanzania, Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan idadi ya watalii imeongezeka.

No comments: