AFISA Maendeleo ya Jamii Halmashauri ya Mji wa Kibaha Lea Lwanji akizungumza KATIKA kongamano |
NA: JULIETHMKIRERI, MAIPAC KIBAHA
maipacarusha20@gmail.com
AFISA Maendeleo ya Jamii Halmashauri ya Mji wa Kibaha Lea Lwanji amesema ili kupunguza wimbi la vijana ambao hawana ajira ni vema wakajiunga na vikundi ili kazi zinapotokea waweze kuunganishwa kwa urahisi na kuondokana na kukaa mitaani bila kazi
Amesema yapo Mashirika na Taasisi zinafanya ujenzi wa miundombinu mbalimbali ikiwemo barabara hivyo kukiwa na vikundi vya vijana vyenye vigezo zinapotokea fura kama hizo kipaumbele kitatolewa kwa vijana .
Lwanji ameyaeleza hayo mjini Kibaha wakati wa kongamano la uwasilishaji wa utafiti wa Vijana kuhusiana na Utekelezaji wa lengo namba 16.7.2 la Maelengo ya Maendeleo endelevu Tanzania.
Utafiti huo ambao umefanywa katika Halmashauri 18 hapa nchini zinazotekeleza mradi wa Kijana Wajibika ikiwemo Taasisi ya Pwani Youth Network ambayo imeshiriki utafiti huo kwa Kibaha Mji na imeandaa Kongamano hilo kwa lengo la kujadiliana na Vijana pamoja na Viongozi wa Serikali kuhusiana na yaliyobainika.
Akizungumza katika Kongamano hilo Lwanji amesema ni wakati sasa Vijana kutambua fursa zilizopo na kuzitumia kwa kuunda vikundi ambavyo vitaeawezesha kuunganishwa na kazi zinazopatikana lakini pia kunufaika na mikopo ya Halmashauri.
" Hamasikeni kuunda vikundi na mvisajili tuwatambulishe mpate kazi, matokeo ya huu utafiti yameibua masuala yanayohusu vijana kiasiasa na kiuchumi na hii inataka pia vijana washiriki wanaposhirikishwa kuondoa vikwazo vilivyopo kwenye maeneo yao" amesema.
Mkurugenzi wa Pwani Youth Network Fred Mtei amesema katika utafiti huo uliofanyika umebaini mifumo inahotumika kutoa taarifa ni kikwazo kwa vijna kushiriki katika mikutano na shughuli mbalimbali.
Mtei amesema kutokana na hali hiyo Taasisi yao inawajibu wa kutoa elimu kwa vijana kushiriki mikutano kwenye maeneo yao ili kujua kinachojadiliwa na mipango inayowekwa.
" Wito wangu Taasisi za kiraia tushirikishe jamii na Serikali kuhakikisha fursa zinawafikia wananchi sisi tuwe kiunganishi kwa kufanya hivi tutafikia malengo ya maendeleo" amesema Mtei.
Mmoja wa Vijana walioshiriki katika Kongamano hilo la kupokea matokeo ya utafiti Ruth Macha alisema ushiriki wa Vijana wa kike kwenye mambo mbalimbali ikiwemo ya uongozi bado ni mdogo na kwamba wengi wao wameshindwa kuthubutu kutokana na hofu jambo ambalo linahitaji elimu.
Naye Abdulrazak Mungi amesema wapo vijana wanashindwa kuingia kwenye uongozi kutokana na ukosefu wa rasilimali fedha hivyo wanahitaji kuungwa mkono na wadau ili wafikie malengo yao kwenye kinyang'anyiro nafasi za uongozi.
No comments:
Post a Comment