WANAWAKE WADAU WA TANZANITE WASAIDIA YATIMA, WAPANDA MITI, WAGAWA TUZO MIRERANI - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Thursday 16 March 2023

WANAWAKE WADAU WA TANZANITE WASAIDIA YATIMA, WAPANDA MITI, WAGAWA TUZO MIRERANI

 




Na Mwandishi wetu, Mirerani

maipacarusha20@gmail.com

WANAWAKE wanaofanya biashara ya madini ya magonga ya madini ya Tanzanite, wachekechaji na wadau wa madini hayo wameadhimisha siku ya wanawake duniani kwa kupanda miti, kugawa tuzo na kutoa msaada kwa watoto yatima.


Makamu Mwenyekiti wa chama cha wachimbaji madini wanawake (TAWOMA) Rachel Njau amesema wamefanya maadhimisho hayo baada ya Machi 8 kuwa na shughuli nyingine ya kitaifa kwenye eneo hilo.


Njau ambaye pia ni Katibu wa chama cha wachimbaji madini Mkoa wa Manyara (MAREMA) Tawi la Mirerani amesema katika maadhimisho hayo, wamefanya shughuli mbalimbali za kijamii.



Amesema wamekutana na kuadhimisha siku yao kwa kupanda miti 50 ndani ya ukuta unaozunguka migodi ya madini ya Tanzanite na kutoa tuzo kwa kutambua michango ya wadau wa maendeleo. 


“Pia tumetoa msaada wa shilingi 500,000 vyakula, mbuzi, nguo, vinywaji, mafuta na sabuni kwa ajili ya watoto yatima wenye kuishi katika mazingira magumu ambapo uwezeshaji mkubwa umetoka kwa dada yetu Anna ambaye yupo nje ya nchi,” amesema Njau.


Amesema watoto yatima hao waliopatiwa misaada hiyo ni wale wanaoishi katika mazingira magumu na kulelewa kwenye kituo cha Light In Africa kilichopo Kata ya Mirerani.


Ofisa madini mkazi Mirerani Menard Msengi, ambaye amejitolea shilingi 200,000 kwa ajili ya kuwasaidia watoto hao yatima amesema amegushwa kutoa sadaka hiyo baada ya kufika eneo hilo.


Mwenyekiti wa UWT Wilaya ya Simanjiro Anna Shinini ambaye amejitolea shilingi 100,000 kwa ajili ya watoto hao amesema jamii inapaswa kuwajali watoto wenye kuishi katika mazingira hatarishi.


Diwani wa kata ya Mirerani, Salome Nelson Mnyawi ambaye alijitolea shilingi 100,000 kwa ajili ya watoto hao amesema wametembelea kituo hicho ili kuwafariji nao wajisikie faraja.


Diwani wa viti maalum Tarafa ya Moipo, Paulina Makeseni amewaahidi watoto hao wanaoishi kituo cha Light In Africa, kuwapa mbuzi kwa ajili ya mboga.


Mwenyekiti wa wanawake wa magonga Mirerani Joyce Mkilanya amesema wanampongeza Rachel Njau kwa kuwaongoza kutembelea kituo hicho cha watoto ili kuwafariji.




No comments: