Na Farida Ramadhani, WFM -Dodoma
maipacarusha20@gmail.com
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango ametoa maagizo sita ya kuzingatiwa katika Maandalizi ya Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050, ikiwemo kuimarisha uwezo wa uchumi uliopo na kulinda mafanikio yaliyopatikana katika utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Taifa 2025.
Alitoa maagizo hayo jijini Dodoma wakati wa akizundua Mchakato wa Maandalizi ya dira mpya ya Maendeleo ya Taifa 2050.
Alisema maandalizi hayo pia yazingatie matumizi ya fursa ambazo hazijatumiwa ipasavyo hadi sasa na kuzikamata fursa zinazochipukia huku akitolea mfano kilimo, mifugo na uvuvi, mazao ya misitu, uongezaji thamani ya mazao pamoja na uvunaji wa rasilimali za kimkakati na kujenga viwanda.
“Katika kilimo Tanzania inafursa ya kuwa ghala la chakula katika Bara la Afrika na hata mashariki ya kati na duniani kama tukilenga uzalishaji mkubwa wa mahindi, ngano, shayiri, maharage ya soya, sukari, mafuta ya kupikia, korosho, matunda, mbogamboga na viungo ”, alibainisha Mhe. Dkt. Mpango.
Mhe. Dkt. Mpango alisema maamdalizi pia yazingatie suala la elimu, hususani elimu ya sayansi, elimu ya ufundi na ufundi stadi, utafiti na maendeleo na ubunifu ili kukuza ujuzi na uwezo wa nguvu kazi ya Taifa.
“Jambo la nne ni namna gani tutavutia na kuasili teknolojia ili kukuza tija katika sekta zote za uzalishaji na kukabiliana na mabadiliko ya tabia ya nchi ikiwa ni pamoja na kuingia ubia wa kimkakati ili kuiwezesha Tanzania kuwapita washindani wetu katika kipindi kifupi” , aliongeza Mhe. Dkt. Mpango.
Alisema kubaini uhalisia wa rasilimali zote zitakazo hitajika kuwezesha utekelezaji makini wa Dira mpya na utekelezaji wa mipango, pamoja na kubainisha mfumo thabiti wa ufuatiliaji na tathimini kwa kuangalia vigezo mahsusi vilivyowekwa.
Mhe. Dkt. Mpango alisema ni vema timu zilizoundwa zikajifunza kutoka katika nchi zilizoendelea kwa kasi kuanzia miaka ya 1960 hususan zile za Bara la Asia pamoja na kuangalia namna nchi nyingine zilivyoweza kujikwamua kutoka katika uchumi wa kati.
Alisema ni matumaini ya Serikali kuwa wananchi wote watapata nafasi ya kutoa maoni yao katika mchakato wa maandalizi ya Dira mpya ambayo inayotarajiwa kuleta mageuzi makubwa ya kiuchumi na kijamii.
“Vile vile makundi mahsusi kama vile Bunge, Mahakama, Sekta Binafsi, Idara za Seriali, Vyombo vya Ulinzi na Usalama, Taasisi za Elimu, Asasi za Kiraia na Watanzania waishio ughaibuni na washirika wetu wa maendeleo watapatiwa muda wa kutosha kushiriki mchakato huu muhimu”, alibainisha Mhe. Makamu wa Rais.
Aidha, aliagiza Wizara zote, Taasisi za Umma, wakala wa Serikali, Idara zinazojitegemea, Sekretarieti za mikoa na Serikali za Mitaa, Sekta Binafsi, Wanadiaspora na Wadau wa Maendeleo kutoa ushirikiano kwa timu ya maandalizi ya Dira mpya ya Maendeleo 2050 pale watakapohitajika kufanya hiyo.
Kwa upande wake Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe.Dkt.Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) alisema utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025 umefanikiwa kwa kiasi kikubwa katika nyanja za uchumi, elimu, afya, miundombinu, umeme, mawasiliano na michezo.
Alisema kabla ya utekelezaji wa Dira iliyopo sasa makusanyo ya kodi kwa mwezi yalikuwa Sh. bilioni 30, lakini baada ya utekelezaji wa Dira hiyo makusanyo kwa mwezi yamefikia zaidi ya Sh. trilioni 2.
“ Kabla ya Dira umeme ulikuwa unakutanao makao makuu ya mikoa na makao makuu ya wilaya chache, sasa tunaongelea idadi ndogo ya vijiji na vitongoji ambavyo havijapata umeme baada ya utekelezaji wa Dira”, alibainisha Mhe.Dkt. Nchemba.
Kuhusu suala la elimu Mhe. Dkt. Nchemba alisema kabla ya utekelezaji wa Dira ilikuwa ni jambo la kawaida wanafunzi waliomaliza elimu ya msingi kutochaguliwa kujiunga na elimu ya Sekondari lakini sasa wanafunzi wanaomaliza wanajiunga na elimu ya Sekondari.
Awali akitoa maelezo kuhusu Dira, Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Dkt. Natu El-Maamry Mwamba alisema utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025 umewezesha nchi kufikia mafanikio mbalimbali ikiwemo kuingia katika uchumi wa kati wa hadhi ya chini ambapo Taifa lilifanikiwa kuongeza kasi ya ukuaji wa uchumi kwa wastani wa asilimia sita na kupungua kwa kiwango cha umaskini kwa zaidi ya asilimia tisa kutoka asilimia 35.7 mwaka 2000/01 hadi asilimia 24.6 mwaka 2017/18.
Alisema vifo vya mama na watoto nchini vimepungua kutoka vifo 854 kwa vizazi 100,000 na vifo 99 kwa vizazi 1,000 mtawalia mwaka 2000 hadi vifo 524 kwa vizazi 100,000 na vifo 36 kwa vizazi 1,000 mtawalia mwaka 2020.
“Kiwango cha udahili wa wanafunzi wa elimu ya msingi kimeongezeka kutoka asilimia 58.8 mwaka 2000 hadi 95.7 mwaka 2020; upatikanaji wa maji umeongezeka kutoka asilimia 50 mwaka 2000 hadi asilimia 86.7 mwaka 2020 kwa mijini na asilimia 55 mwaka 2000 hadi asilimia 72.3 mwaka 2020 kwa vijijini; na upatikanaji umeme vijijini umeongezeka na kufikia asilimia 69.8 mwaka 2020”, alibainisha Dkt. Mwamba.
Kuhusu maandalizi ya Dira 2050, Dkt. Mwamba alisema maandalizi hayo yametokana na mambo manne ikiwemo kuelekea ukomo wa utekelezaji wa Dira 2025, kuendeleza mafanikio yaliyofikiwa kutokana na utekelezaji wa Dira 2025, uhitaji wa mkakati utakaowezesha nchi kunufaika na maendeleo ya kiuchumi na kiteknolojia yanayoendelea kuibuka duniani.
“ Masuala kama vile uchumi wa buluu, matumizi ya roboti, biashara ya hewa ukaa) pamoja na uhitaji wa Mkakati utakaoanisha Agenda ya Maendeleo ya nchi na mikakati mingine ya Kikanda na Kimataifa ambapo Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 itahakikisha kuwa Tanzania inaendelea kuoainisha Agenda yake ya Maendeleo na Agenda na Mikakati ya Kimataifa”alisema Dkt. Mwamba
Alisema maandalizi ya Dira hiyo yanajumuisha tathmini ya utekelezaji wa Dira 2025 kwa kuwa tathmini hiyo ni muhimu katika kuainisha mafanikio, hatua za utekelezaji na changamoto zilizojitokeza kipindi cha utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Taifa 2025.
No comments:
Post a Comment