Viongozi wa JOWUTA wakiwa na afisa kazi Mkoa wa Mwanza |
Viongozi wa JOWUTA wakiwa nje ya Jengo la Sahara Media hivi karibuni |
Mwandishi wetu.
maipacarusha20@gmail.com
Chama cha Wafanyakazi kwenye Vyombo vya Habari Tanzania (JOWUTA) kimewataka waajiri kwenye vyombo vya habari nchini kuzingatia sheria za kazi na kuacha kuwafukuza kazi wafanyakazi bila kuzingatia sheria.
Baadhi wa wanahabari nchini, wamekuwa wakilalamikia kufukuzwa kazi na kusimamishwa kazi bila kuzingatia sheria, wengine kutopewa mikataba katika vyombo vyao licha ya kufanya kazi zaidi ya miaka 10 na pia wengine kutowekewa fedha kwenye mifumo ya hifadhi ya Jamii Wala kuwa na bima.
Katika taarifa kwa vyombo vya habari ya Kamati ya Utendaji wa JOWUTA iliyosainiwa na Mwenyekiti wa JOWUTA Taifa,Mussa Juma kufuatia wafanyakazi wanne wa kampuni ya Sahara Media kufukuzwa kazi baada ya kutoa malalamiko Yao kwa viongozi wa JOWUTA chama hicho kimetaka wamiliki wa vyombo vya habari nchini kuzingatia sheria.
Taarifa hiyo imeeleza Aprili 7,2023 Viongozi wa JOWUTA, walifanya ziara ya kikazi mkoani Mwanza, kuzungumza na wafanyakazi wa Sahara Media ambao wanafanyakazi Radio Free Afrika(RFA) na Star Tv ambao wamekuwa na madai ya kutolipwa mishahara ya Kila mwezi zaidi ya sh 2.5 Bilioni madai ambayo tayari yamesajiliwa Idara ya kazi Mkoa wa Mwanza hadi kufikia mwaka 2022 na sasa madeni yameongezeka.
Imeeleza kuwa baada ya mazungumzo na wafanyakazi wa vyombo hivyo vya habari ,Afisa kazi kiongozi mkoa wa Mwanza na baadae kuzungumza na vyombo vya Habari wafanyakazi walioshiriki kikao wamepewa barua za kufukuzwa kazi.
"Wafanyakazi waliohudhuria mkutano wa JOWUTA wameandikiwa notisi ya mwezi mmoja ya kusudio la kuwafukuza kazi kwa Kisingizio cha kupunguza wafanyakazi (Retrenchment)",imesema taarifa ya JOWUTA.
JOWUTA imeeleza kuwa baada ya Mwanachama mmoja wa JOWUTA kuendelea na kazi akisubiri mwezi ufike apewe barua yake rasmi ya kuondolewa kazini kwa mujibu wa kifungu cha 38 na kifungu Cha 41 cha Sheria ya ajira na Mahusiano kazini sura ya 366 Namba 6 ya 2004 ametakiwa kuondoka kazini.
"Pamoja na Mwanachama wetu kuheshimu sheria, Uongozi wa RFA ulitoa maelekezo mengine ya kufukuzwa kazi kinyume cha sheria kwa kuondolewa kwenye kipindi Redioni wakati anaendelea kutangaza Aprili 15,2023."imesema taarifa ya JOWUTA
Chama hicho kimeeleza mfanyakazi huyo, analazimishwa aombe likizo asionekane kazini wakati ambao notisi ya mwezi mmoja haijafika mwisho na Mwajiri hajatimiza wajibu wake wa kumpa stahiki zake(benefits) kwa mujibu wa Sheria za kazi. Huu ni ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu na kuvunja sheria za kazi ambao unastahili kukemewa na kila mtu.
Kutokana na Mgogoro huo,JOWUTA inapinga uamuzi wa kuwafukuza kazi wafanyakazi wa Sahara Media ambao walizungumza malalamiko yao na viongozi wa JOWUTA kwani ni haki yao na hakuna kosa ambalo walifanya.
JOWUTA imeeleza wanaitaka kampuni ya Radio Free Afrika na Star Tv kuheshimu sheria na kufanya majadiliano na wafanyakazi wake, katika mchakato wowote wa kuwaondoa kazini na kuwalipa stahiki zao kwa mujibu wa sheria husika"imeeleza taarifa hiyo.
"Wakati JOWUTA na wanachama na LHRC tunaendelea na hatua nyingine, tunaiomba serikali kukamilisha mchakato wa kufikishwa mahakamani wamiliki wa vyombo hivi vya habari kwani tayari Kamishna wa kazi nchini, amelifikisha shauri hili ofisi ya Mkurugenzi wa mashitaka mkoa Mwanza"imeeleza taarifa hiyo.
No comments:
Post a Comment