Viongozi wa Jumuiya ya wazazi CCM Kibaha wakitoa msaada katika wodi ya wazazi |
NA: JULIETH MKIRERI, MAIPAC KIBAHA
JUMUIYA ya wazazi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Kibaha Mjini imefanya ziara katika kituo cha afya Mkoani kilichopo Wilaya ya Kibaha na kutoa msaada katika Wodi ya wazazi.
Akizungumza wakati wa kutoa msaada huo Mwenyekiti wa jumuiya hiyo ya wazazi Yahaya Mtonda amesema kwamba wameamua kufanya ziara hiyo ya kutembelea kituo hicho cha afya ikiwa ni maadhimisho ya wiki ya wazazi hivyo wakaona kuna umuhimu kufanya matukio ya kuisaidia jamii.
Mwenyekiti huyo ambaye aliambatana na viongozi wa Jumuiya hiyo wakiwemo wajumbe wa kamati ya utekelezaji sambamba na baadhi ya Madiwani walitembelea wazazi waliojifungua kwa ajili ya kuwajulia hali na kuwapatia baadhi ya mahitaji.
Mtonda amesema kwamba Jumuiya yao imebaini vikwazo ambavyo viawakabili wanawake wajawazito pindi wanapojifungua ambao wanamahitaji mbali mbali ili kuweza kuwasaidia pindi wanapokuwa wodini wao pamoja na watoto.
"Tupo katika kipindi cha maadhimisho wiki ya wazazi ambapo kwa Upande wetu kama Wilaya ya Kibaha mji tumeamua kuchagua baadhi ya maeneo kwa ajili ya kuyatembelea ikiwemo kituo hichi katika wodi ya wazazi na kutoa msaada wa vitu sabuni, taulo za watoto (pampas) pamoja na mahitaji mengine muhimu kwa ajili ya watoto na wakinamama.
Aidha Mwenyekiti huyo amesema kuwa wazazi na walezi wanapaswa kubadilika kwa kuhakikisha kwamba wanawalea na kuwatunza watoto wao kwa lengo la kuijenga nchi.
Amesema wataendelea kushirikiana na Serikali katika kukabiliana na changamoto mbali mbali zinazokikabili kituo hicho ikiwemo kuboresha miundombinu ya majengo ili wagonjwa waweze kupata huduma nzuri.
Awali mganga mfawadhi wa kituo cha afya Mkoani Abdulkadri Sultan ameipongeza Jumuiya hiyo ya wazazi kutokana na kuona umuhimu wa kutumia wiki ya maadhimisho yao kutoa msaada katika wodi ya wazazi kwani wamekuwa wakikabiliwa na changamoto ya ukosefu wa mahitaji pindi wazazi wanapojifungua.
Sultan amesema kituo hicho kinakabiliwa na changmoto mbalimbali ikiwemo kupokea idadi kubwa ya wagonjwa ukilinganisha na wodi zilizopo ambazo ni chache .
Naye Diwani wa Tumbi Raymond Chokala ambaye naye alishiriki katika ziara amewashukuru kwa dhati uongozi mzima wa jumuiya ya wazazi Wiyala ya Kibaha mji kwa kuona umuhimu wa kuwasapoti kwa hali na mali wakinama hao pamoja na watoto wao.
Nao baadhi wa wakinamama ambao walipata fursa ya kutembelewa na kupatiwa msaada wa vitu mbali mbali wamesema kitendo hicho kimeweza kuwafariji kwa kiasi kikubwa kwani hawakuweza kutegemea kama watapatiwa msaada huo kwani utawasaidi wao pamoja na watoto wao.
Katika hatua nyingine uongozi wa jumuiya hiyo uliweza kutoa salamu zao kwa Mbunge wa Jimbo la Kibaha mjini Silvestry Koka pamoja na mke wa Mbunge Selina Koka kwa kuweza kusapoti kufanikisha zoezi hilo pamoja na wadau wengine wakiwemo baadhi ya madiwani wa Halmashauri ya Mji Kibaha.
No comments:
Post a Comment