THRDC YAWAKUTANISHA MAJAJI NA MAHAKIMU KULINDA UHURU WA KUJIELEZA - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Saturday 1 April 2023

THRDC YAWAKUTANISHA MAJAJI NA MAHAKIMU KULINDA UHURU WA KUJIELEZA

 

Mratibu wa Mtadao wa THRDC, Onesmo Olengurumwa



Mwandishi wetu,MAIPAC Dodoma

maipacarusha20@gmail.com


MTANDAO wa watetezi wa haki za Binaadamu (THRDC) umewakutanisha Mahakimu na Majaji katika mafunzo kuhusu wajibu wa Mahakama katika kutunza na kulinda uhuru wa kujieleza pamoja na haki za binadamu nchini.


Mafunzo hayo ya siku mbili yanatolewa na Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) likiwa Ni kukumbushana masuala mbalimbali katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.


Mratibu wa Mtadao wa THRDC, Onesmo Olengurumwa akizungumza, wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo amesema lengo la mafunzo hayo ni kukumbushana wajibu katika kutekeleza majukumu ya kila siku.


“Kumekuwepo na mabadiliko mengi ya kisheria na masuala mbalimbali yanayohusu haki za binadamu hivyo wao kama watu ambao wanatoa haki kila siku katika Mahakama, wanapaswa kuyafahamu ili kulinda haki za binadamu na uhuru wa kujieleza”amesema 


Amesema pia mafunzo mengine ambayo yatatolewa ni masuala ya maadili kwa Mahakimu na Majaji katika utekelezaji wa majukumu ya utoaji wa haki katika maeneo yao.


Amesema Suala la maadili ni jambo la muhimu sana katika mahakama zetu nchini hivyo mafunzo haya pia yatasaidia kuwakumbusha Mahakimu na Majaji wajibu wao wa kutenda haki kwa kuzingatia maadili ya kazi zao.


Ameleza utoaji wa mafunzo hayo ni sehemu ya Mtandao huo kuunga juhudi za serikali katika kuboresha miundombinu ya utoaji haki nchini.


“Tusiwe watu wa kulalamika tunapaswa kushiriki kuboresha Mahakama zetu kufanya kwa pamoja kama taifa huduma ya Mahakama ni huduma ya haki jukumu letu kusaidia kuboresha sekta hii ili kupunguza malalamiko yaliyopo kwa wananchi katika masuala ya haki jinai”amesema 


Naibu katibu mkuu wa Chama cha Mahakimu na Majaji Tanzania (JMAT) Mary Kallomo, amesema mafunzo hayo yatawasaidia kuboresha utendaji wao wa kila siku katika kulinda haki za binadamu na uhuru wa kujieleza.


“Tunahitaji kukumbushana masuala mbalimbali katika utekelezaji wa majukumu yetu na suala la maadili ni jambo la muhimu sana kwakuwa sisi ndiyo tunatoa haki katika Mahakama zetu”amesema


Hata hivyo, ameeleza ipo haja kwa wadau wa masuala ya haki jinai nchini kutoa mafunzo kwa kundi hilo kuhusu masuala ya kimtandao.


“Teknolojia hivi sasa imekuwa sana hivyo kutokana na hali hiyo ipo haja Mahakiumu na Majaji kupatiwa mafunzo ya masuala ya kimtandao ili wanapotoa huduma zao wasivunje haki za binadamu pamoja na uhuru wa kujieleza”amesisitiza Kallomo


THRDC imekuwa ikiratibu mafunzo kwa asasi na Taasisi za umma na binafsi kuhusiana na masuala ya Haki za binaadamu,Usimamizi wa asasi za kiraia na masuala ya usalama kwa watetezi wa haki za binaadamu.


No comments: