Makamu wa Rais azungumzia zoezi la kuhamishwa wananchi wa Ngorongoro - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Wednesday, 17 May 2023

Makamu wa Rais azungumzia zoezi la kuhamishwa wananchi wa Ngorongoro






 SOPHIA FUNDI KARATU.

maipacarusha20@gmail.com


Makamu wa Rais Dkt. Philip  Mpango ameutaka uongozi wa mamlaka ya Hifadhi  ya Ngorongoro kuharakisha zoezi la kuwahamisha kwa hiari wananchi wanaoishi ndani ya hifadhi ya Ngorongoro.


Makamu aliyasema hayo jana wakati akizungumza na watumishi wa mamlaka pamoja na wananchi akiwa kwenye ziara yake wilayani Karatu ambapo aliweka jiwe la msingi ujenzi wa jengo la ofisi za makao makuu ya Mamlaka ya hifadhi ya Ngorongoro katika eneo la Njiapanda wilayani Karatu


Dkt. Mpango ameagiza uongozi wa mamlaka  kwenda kutoa elimu ya uhifadhi kwa wananchi walioko ndani ya hifadhi na kueleza changamoto zitokanazo na shughuli za binadamu ili zoezi Hilo kukamilika Desemba mwaka huu.


Akizungumza  katika hafla hiyo,waziri wa maliasili na utalii Mohamed Mchengerwa amesema kuwa wizara  imejipanga kumaliza changamoto mbalimbali ndani ya hifadhi likiwemo msongamano wa shughuli za kibinadamu ndani ya hifadhi ambapo wananchi wamehiarika kuhama wenyewe kwenda kijiji Cha Msomera wilayani Handeni pamoja na Mamlaka kuhamisha ofisi zao wilayani Karatu


Amesema kuwa kuhamishwa kwa ofisi za Mamlaka kutapunguza msongamano wa shughuli za watumishi ndani ya hifadhi.




Kwa  upande wake Naibu Kamishna Mamlaka ya hifadhi ya Ngorongoro Elbariki Bajuta amesema kuwa awamu ya Kwanza ya kuwahamisha wananchi kwa hiari ndani ya hifadhi ilimalizika mwezi January mwaka huu ambapo jumla ya kaya 551yenye watu 3010 na mifugo 15521 walihamishwa eneo la Msomera.


Bajuta amesema kuwa awamu ya pili ya zoezi Hilo litaanza mwezi Mei mwaka huu ambapo  wamekamilisha hatua zote na tiyari wananchi wengi wamejiandikisha kwa hiari  kuhamia eneo la Msomera.


Amesema kuwa kuwahamisha wananchi ndani ya hifadhi kutasaidia kupunguza msongamano wa shughuli za kibinadamu ndani ya hifadhi na kuongeza utalii pamoja na  mapato ya serikali.




No comments: