BUNGE lapitisha maazimio ya kuanzishwa kwa msitu wa hifadhi ya Kigosi na kurekebisha mpaka wa Hifadhi ya Ruaha kwa kishindo - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Wednesday 28 June 2023

BUNGE lapitisha maazimio ya kuanzishwa kwa msitu wa hifadhi ya Kigosi na kurekebisha mpaka wa Hifadhi ya Ruaha kwa kishindo

 





Na: Mwandishi wetu 


maipacarusha20@gmail.com


Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limepitisha kwa kishindo maazimio  ya kuridhia kufutwa  kwa Hifadhi ya Taifa Kigosi ili kuruhusu kuanzishwa kwa Msitu wa Hifadhi Kigosi pia kurekebisha  mpaka wa Hifadhi ya Taifa ya Ruaha yaliyotolewa Juni 27,2023  kwenye  kikao  cha 56 cha Bunge  na Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mohamed Mchengerwa  baada ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan kuridhia.


Kwa mujibu wa masharti ya nyongeza ya kifungu cha 4 cha Sheria ya Hifadhi za Taifa, Sura ya 282, Rais amepewa mamlaka ya kurekebisha mipaka ya eneo lolote lililotangazwa kuwa Hifadhi ya Taifa baada ya kupata idhini ya Bunge, na kwa Tamko litakaochapishwa kwenye Gazeti la Serikali. 


Akisoma azimio la kwanza  la Kigosi mbele ya Bunge, Waziri Mchengerwa  amesema Hifadhi ya Taifa Kigosi ilianzishwa kwa Tangazo la Serikali Namba 924 la Mwaka 2019 ikiwa na ukubwa wa kilometa za mraba 7460 ikiwa na lengo la kuimairisha uhifadhi na hivyo kukuza utalii, uchumi na kuwezesha kufanyika kwa tafiti na kutoa elimu ya vitendo kwa wananchi watakaotembelea hifadhi hiyo.  



Ametaja  manufaa yatakayopatikana  baada ya Kuanzishwa kwa Hifadhi hiyo  inayosimamiwa na Sheria ya Misitu, Sura ya 323 kuwa  ni pamoja na  wananchi wa Mikoa 5 ya Geita, Kagera, Kigoma, Shinyanga na Tabora; Wilaya  6 za Bukombe, Mbongwe, Biharamulo, Kakonko, Kahama na Kaliua na Kata 25. Aidha,  vijiji 126 na Kaya 113,547 vitanufaika kiuchumi na uamizi huu ambapo wataruhusiwa kufanya shughuli mbalimbali za kiuchumi ndani ya Hifadhi hiyo ikiwemo ufugaji nyuki na uvuvi wa samaki kwa mujibu wa Sheria.



Pia kuchochea shughuli za ufugaji nyuki kibiashara ambapo takriban wafugaji 1,764 wenye mizinga zaidi ya 521,406 waliokuwepo awali kwenye maeneo hayo wataongezeka maradufu. Hatua hiyo itachangia ongezeko la uzalishaji wa asali nchini kutoka wastani wa tani 32,691 hadi 138,000 kwa mwaka na kuongeza mauzo ya mazao nyuki nje ya nchi ambapo ameeleza kwamba kwa sasa nchi yetu inauza nje takriban tani 1,700 zenye thamani ya Dola za Marekani Milioni 14 ambayo ni sawa asilimia 5 ya kiasi chote kinachozalishwa kwa sasa. 



Aidha, kupata uhakika wa malighafi kwa viwanda 6 vya kuchakata na kufungasha mazao ya nyuki ambavyo ujenzi wake umewezeshwa na Serikali kwa zaidi ya gharama ya Shilingi bilioni 2.5 kwenye Wilaya za Mlele, Kibondo, Bukombe, Nzega, Sikonge na Wilaya ya Manyoni.



Pia kufanyika  kwa shughuli za kimila na hivyo kujenga mahusiano mema kati ya wananchi na wahifadhi kupitia programu ya usimamizi shirikishi wa misitu kwa mujibu wa Sera ya Taifa ya Misitu ya Mwaka 1998; na kuongeza mchango wa sekta ya misitu na nyuki katika Pato la Taifa. 



Kwa upande wa Hifadhi ya Ruaha amesema, Hifadhi ya Taifa Ruaha ilianzishwa kwa Tangazo la Serikali Namba 464 la Mwaka 1964 ikiwa na ukubwa wa kilometa za mraba 10,300 na baadaye kufanyiwa marekerebisho kupitia Tangazo la Serikali Namba 28 la Mwaka 2008 kwa kuongeza eneo la Bonde la Usangu na kufikia ukubwa wa kilomita za mraba 20,300 lengo likiwa ni kuhifadhi na kulinda bioanuai hususan wanyamapori, mimea,  mazalia na makuzio ya samaki na mtiririko wa maji kwenye mto Ruaha Mkuu ambao ni chanzo kikuu cha maji kwenye mabwawa ya kufua umeme. 



Ametaja  baadhi yatakayopatikana kwa eneo lenye ukubwa wa kilometa za mraba 478 ambalo limemegwa kutoka kuwa sehemu ya hifadhi kwenda kwa wananchi kwa ajili ya shuguhuli mbalimbali za kiuchumi kama vile kilimo na ufugaji katika vijiji 29 kuwa  ni pamoja na Kuhifadhi vyanzo vya maji vilivyopo katika Bonde la Usangu na kuimarisha mtiririko wa maji kwenye milima ya Kipengere na Uporoto kuelekea lindimaji la Ihefu ambalo ni chanzo cha mto Ruaha Mkuu unaotegemewa kuzalisha Umeme wa Maji katika Mabwawa ya Mtera, Kidatu na Bwawa la Julius Nyerere ili kuimarisha upatikanaji wa umeme nchini.



Kuboresha mifumo ikolojia ya  Bonde la Usangu ili kurejesha wanyamapori na uoto wa asili kwenye Hifadhi ya Taifa ya Ruaha.



Kuimarisha uhifadhi wa maliasili, hususani wanyamapori, mimea, mazalia na makuzio ya samaki na viumbemaji wengine, kuondoa migogoro ya mipaka baina ya Hifadhi ya Taifa Ruaha na vijiji husika na kuongeza mchango wa Pato la Taifa kupitia utalii katika Hifadhi ya Taifa Ruaha; na kuwezesha upatikanaji wa maji kwa ajili ya shughuli nyingine za kiuchumi ikiwemo kilimo, ufugaji na uvuvi. 



Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliaslini na Utalii, Mhe, Timotheo Mzava amesema kutokana na umuhimu na manufaa ya maazimio hayo  Kamati yake imeridhia na  kuwaomba wabunge waipitishe kwa manufaa ya taifa letu.


Aidha,  ameitaka Wizara  kuzingatia  pamoja  masuala kadhaa  wakati wa utekelezaji wake ikiwa ni pamoja na kuliwalipa fidia kwa wakati wananchi wanaoondolewa katika maeneo hayo,  kushirikiana na wananchi, kuwaelimisha wakati wa zoezila kuweka alama za mipaka  pia eneo la kapunga 1 lililomegwa litengenezewe miundombinu na kukabidhiwa.




No comments: