FAISAL AWASAIDIA WAFANYABIASHARA WANAWAKE WA MADINI YA TANZANITE ARUSHA - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Friday 2 June 2023

FAISAL AWASAIDIA WAFANYABIASHARA WANAWAKE WA MADINI YA TANZANITE ARUSHA

 

Mfanyabiashara wa madini ya Tanzanite Faisal Juma


Mwandishi wetu,Arusha

maipacarusha20@gmail.com


Mfanyabiashara maarufu wa  madini  ya Tanzanite,Faisal Juma Shabhai amewasaidia wafanyabiashara Wanawake wa madini na vijana zaidi ya 100 mtaji wa sh 30 milioni ili kuendeleza biashara zao.




Wafanyabiashara  hao wanakabiliwa na ukata kutokana na kuporomoka kwa soko la madini katika jiji la Arusha kufuatia serikali kuzuia biashara ya madini ya Tanzanite nje ya mji wa Mererani Wilaya ya Simanjiro mkoa wa Manyara.


Akizungumza katika hafla ya kutolewa misaada hiyo, Mkuu wa mkoa Arusha, John Mongela alisema serikali inatambua changamoto za wafanyabiashara wa madini Arusha baada ya kusitishwa biashara ya Tanzanite nje ya Mererani.


Mongela alisema tayari amefanya mazungumzo na Waziri wa Madini Dotto Biteko muhusiana na biashara ya Tanzanite kurejeshwa Arusha.


"Nilizungumza na Waziri Dotto serikali inalifanyia kazi suala hili na tutapata maelezo karibuni"alisema 


Mkuu wa mkoa pia alitaka kurejeshwa maonesho ya kimataifa ya madini ya Vito ambayo yalikuwa yakifanyika Jijini Arusha lakini yamesitishwa.


Naye Shabhai akizungumza wakati wa kutoa msaada huo alisema ameutoa kutokana na kutambua changamoto za wafanyabiashara wa madini katika jiji la Arusha na kuona anawajibu wa kusaidia.


Shabhai alisema msaada huo anatarajia utasaidia kurejesha mitaji yao ambayo imedhoofika kutokana na kuyumba kwa biashara ya madini katika jiji la Arusha.


Wakizungumza katika hafla hiyo, Mwenyekiti wa chama cha wafanyabiashara wa madini nchini(TAMIDA) Sammy Mollel na Mwenyekiti wa chama Cha wafanyabiashara wa madini wanawake mkoa Arusha,Sweet Nkya  walieleza changamoto kadhaa ambazo zinawakabili.


Mollel alisema ni muhimu kurejesha Arusha biashara ya Tanzanite na kufufua maonesho kwani yalikuwa na faida kubwa kwa sekta ya madini.


Mwenyekiti Nkya alimshukuru Mfanyabiashara Faisal Shabhai kwa msaada aliotoa na kueleza utasaidia kupunguza  shida kubwa ya baadhi yao kukosa mitaji baada ya kufa kutokana na kushindwa kufanya biashara ya madini ya Tanzanite.


Serikali ilisitisha biashara ya madini ya Tanzanite nje ya Mererani miaka Saba Sasa ikiwa ni sehemu ya mikakati kudhibiti utoroshwaji nje madini hayo.



No comments: