MWENGE WA UHURU WAWEKA JIWE LA MSINGI JENGO LA MAFUNZO CHUO CHA USIMAMIZI WANYAMAPORI MWEKA - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Tuesday 27 June 2023

MWENGE WA UHURU WAWEKA JIWE LA MSINGI JENGO LA MAFUNZO CHUO CHA USIMAMIZI WANYAMAPORI MWEKA

 





Na Mwandishi wetu, Moshi


maipacarusha20@gmail.com


MWENGE wa uhuru umeweka jiwe la msingi kwenye jengo la kutolea mafunzo katika chuo cha usimamizi wa wanyamapori Mweka, kilichopo Wilaya ya Moshi Mkoani Kilimanjaro.


Afisa uhusiano mkuu wa chuo cha usimamizi wa wanyamapori Mweka, Ernest Emmanuel akisoma taarifa ya mradi huo kwa kiongozi wa mbio za mwenge wa uhuru kitaifa kwa mwaka 2023 Abdalah Shaib Kaim, amesema hadi kukamilika utagharimu shilingi za kitanzania 3,799,982,716.49.


Emmanuel amesema mradi huo umejengwa kwa kutumia fedha za mapato ya ndani ya chuo hicho, ambapo hadi hivi sasa wametumia shilingi 1,788,743,680.69 kumlipa mkandarasi wa ujenzi huo, kampuni ya SUMA JKT.


“Mradi hu ni moja ya kazi zinazoendelea kufanywa na Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dr Samia Suluhu Hassan, kupitia chuo hiki, kwa lengo la kuweka mazingira bora na rafiki kwa watumishi na wanafunzi, ili waweze kutekeleza majukumu yao na kufikia ndoto zao,” amesema Emmanuel.


Amesema jengo hilo litakapokamilika litakuwa  na uwezo wa kuchukua wanafunzi 1,200 kwa wakati mmoja na vyumba 10 vya ofisi kwa ajili ya walimu 28 na hivyo kupunguza changamoto ya uhaba wa miundombinu ya kujifunza na kufundishia.


Amesema jengo hilo litakapokamilika ni dhahiri kuwa faida zifuatazo zitapatikana ikiwemo uhaba wa madarasa, vyumba vya mihadhara na ofisi za wahadhiri utamalizika au kupungua.


“Pia ubora wa shughuli za utoaji mafunzo kwa wanafunzi utaimarika kutokana na ubora wa madarasa na vyumba vya mihadhara vyenye vitendea kazi na miundombinu ya kisasa,” amesema Emmanuel.


Amesema pia udahili wa wanafunzi utaongezeka kutokana na kuvutiwa na mazingira bora na rafiki ya kujifunzi na ongezeko la ofisi za wahadhiri, litaboresha utendaji kazi na utoaji huduma kwa wanafunzi na wateja wengine.


Amesema jengo hilo pia linaweza kutumiwa na wadau mbalimbali, zikiwemo taasisi za serikali na binafsi, kwa ajili ya kuendesha semina na mafunzo ya muda mfupi.


“Aidha katika kutekeleza mradi huu faida nyingine zimejitokeza, ikiwa ni pamoja na ajira za moja kwa moja miongoni mwa wananchi waishio jirani au nje ya eneo la Mweka, sambamba na soko la kuuza vyakula na matunda,” amesema Emmanuel.


Katika hatua nyingine kiongozi wa mbio za Mwenge wa uhuru kitaifa Kaim, amezindua rasmi maadhimisho ya miaka 60 ya chuo kwa kuongoza shughuli za upandaji miti ya kivuli katika eneo la mradi ambapo Juni 24 mwaka 2023 chuo kimetimiza miaka 60 toka kuanzishwa kwake na kilele cha maadhimisho hayo kitakuwa mwezi Novemba mwaka 2023.


Kauli mbiu ya mbio za mwenge wa uhuru kwa mwaka 2023 ya Okoa Mazingira, tunza vyanzo vya maji, inasadifu majukumu ya chuo ya msingi kama taasisi ya uhifadhi wa mazingira na bayoanuwai, ambapo zaidi ya miti 400 imepandwa kwa ajili ya kivuli katika maeneo mbalimbali ya chuo ikiwa ni pamoja na eneo la mradi na eneo la barabara kubwa.


Chuo kitaendelea na zoezi la kupanda miti katika eneo hili na maeneo menginne nchini kwa lengo la kutunza mazingira, kulinda vyanzo vya maji lakini pia ili kujipatia kipato.


Aidha chuo kitashiriki kikamilifu kutoa elimu kwa jamii juu ya umuhimu, aina za miti ya kupanda na utunzaji wa miti.



No comments: