THRDC YASAINI MKATABA WA FEDHA WA MIAKA MITATU NA SWEDEN - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Friday 2 June 2023

THRDC YASAINI MKATABA WA FEDHA WA MIAKA MITATU NA SWEDEN

 



Na Mwandishi wetu, DSM

maipacarusha20@gmail.com

Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), leo umesaini mkataba wa miaka  mitatu (3) wenye thamani ya fedha za kitanzania Bilioni 3.2  na Sweden. 

THRDC na Sweden wamekuwa na ushirikiano kwa zaidi ya miaka 10 sasa toka Mtandao huu uanzishwe. Ubalozi wa Sweden nchini Tanzania ni mdau mkubwa wa kazi za taasisi na haki za binadamu nchini Tanzania


Mkataba huu wa miaka mitatu umelenga kuendeleza kazi na mafanikio ya Mpango Mkakati wa awali wa (2018-2022) na kuimarisha utekelezaji wa Mpango Mkakati mpya wa Taasisi wa (2023-2027).Lengo kuu la mpango huu ni kuboresha mazingira kwa watetezi wa haki za binadamu, kwa kuzingatia mambo matatu yafuatayo:


1. Kuendelea kutoa msaada wa haraka kwa Watetezi wa haki za binadamu ikiwemo msaada wa kisheria pale wanapopitia mazingira hatarishi wakiwa katika shughuli zao za utetezi, kufanya uchechemuzi wa sera na sheria kandamizi zinazowaathiri watetezi wa haki za binadamu na haki za binadamu kwa ujumla. Kutafuta fursa za majadiliano na mashirikiano baina ya watetezi wa haki za binadamu na taasisi mbalimbali za ndani na nje zikiwemo za kiserikali na zisizo za kiserikali.


2. Kuwajengea watetezi wa haki za binadamu ikiwemo mashirika wanachama na yasiyo wanachama uwezo wa namna ya kutekeleza kazi zao za utetezi na kujilinda wanapopitia mazingira hatarishi.  Lakini pia kujengea uwezo asasi za kiraia kuhusu haki na wajibu wao ikiwemo swala la kuzingatia sheria zinazowahusu.


3. Na Kukuza ustawi na ujenzi wa taasisi.


Shughuli zote zitakazotekelezwa kwenye mradi huu zitachangia moja kwa moja kwenye kutekeleza malengo ya Mpango mkakati huu mpya wa Mtandao (2023- 2027).


Makubaliano hayo  yamesainiwa rasmi leo June 02, 2023 na utekelezaji wake utaanza mapema mwezi huu na kumalizika December 31, 2026. Mojawapo ya wanufaika wa mradi huu ni Watetezi wa Haki za Binadamu nchini (Tanzania Bara na Zanzibar), wakiwemo wanachama na wasio wanachama wa Mtandao. 



No comments: