Na: Mwandishi wetu, Ngorongoro
maipacarusha20@gmail.com
Jeshi la Polisi na Uongozi wa Mamlaka ya hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) wametakiwa kuwakamata Askari wa Jeshi la Uhifadhi wa Ngorongoro ambao wamehusika kumng'oa meno mawili Joshua Ole Patarro (15).
Kijana huyo ameng'olewa meno akiwa anarejesha Mifugo nyumbani katika eneo la Olmoti ndani ya hifadhi ya Ngorongoro.
Wakizungumza na MAIPAC Mbunge wa Jimbo la Ngorongoro, Emmanuel ole Shangai, Diwani James Moringe na watetezi wa Haki za binadamu wametaka kukomesha matukio ya ukiukwaji wa Haki za binadamu katika eneo hilo.
Mbunge wa Ngorongoro Ole Shangai amesema katika siku za karibuni mahusiano baina ya wananchi na baadhi ya Askari wa Jeshi Usu sio mazuri.
"Vitendo vya ukiukwaji Haki za Binaadamu vimeongezeka ,Mifugo inakamatwa vijana wanakamatwa juzi wametaka kumuumiza kijana mmoja baada ya kutaka kumgonga na gari"amesema
Amesema lazima wahusika wa tukio Hilo wakamatwe kwani wamefanya kosa kumng'oa meno kijana asiye na hatia.
"Sasa wanakamata watu kuingiza Mifugo Olmoti na Embakai wakati wao ndio wamezuia miradi ya Maji Ngorongoro hili haliwezekani" amesema
Diwani wa CCM , James Moringe amesema katika siku za karibuni Askari wageni wa NCAA wamekuwa wakifanya matukio ya ukiukwaji Haki za binaadamu ikiwepo kuharibu makazi.
"Wanakamata Mifugo Olmoti kule Embakai na wanaharibu makazi, wanafanya operesheni kumkamata pikipiki usiku jambo ambalo sio sawa"amesema
Ametaka waliohusika na ukatili wa kijana Joshua kukamatwa mara Moja kwani wamevunja sheria.
Jeremiah Laizer ameitaka serikali kuingilia Kati kutatua migogoro baina ya watendaji NCAA na wananchi ili kukomesha ukiukwaji Haki za Binaadamu.
"Hili tukio la ukiukwaji Haki za binaadamu lazima likemewe maana haiwezekani askari kumng'oa meno kijana asiye na hatia"amesema
Naibu Kamishna wa Uhifadhi,Elibariki Bajuta alipotakiwa kueleza tukio hilo alikiri kupata taarifa za tukio hilo.
Bajuta amesema baada ya kupata taarifa hiyo amewatuma askari kwenda eneo la tukio kufatilia kilichotokea.
Amesema hata hivyo amewaomba polisi nao kufatilia suala hilo.

No comments:
Post a Comment