![]() |
| Mbuzi na Kondoo wakiwa machungani katika nyanda za malisho zilizoathirika na ukame |
| Baadhi ya Viongozi wa kimila wilayani Longido wakiwa katika kikao cha kujadiliana njia bora ya kulinda nyanda za malisho ili mifugo ipate chakula cha kutosha |
| Mwenyekiti wa kijiji cha Orbomba Kashilo Alais akielezea namna nyanda za malisho zilivyoathirika na ukame |
Na: Andrea Ngobole, Longido
email: maipacarusha20@gmail.com
Jumla ya hekta 639,235 ambazo ni sawa na asilimia 82.14 ya hekta
778,575 za wilaya ya Longido zinafaa kutumika kwa ajili ya malisho ya mifugo na
wanyamapori.
Hekta hizo hazijaendelezwa kwa ajili ya malisho bora ambayo
ingesaidia mifugo kupata malisho ya uhakika kwa mwaka mzima.
Mabadiliko ya tabianchi yamesababisha ukame mkubwa na hatimaye uhaba wa malisho ya mifugo wilayani hapo.
Wataalamu wa hali ya hewa wanatafsiri mabadiliko ya tabianchi kuwa
ni mabadiliko katika wastani wa hali ya hewa katika eneo fulani kwa muda
mrefu mfano eneo liliokuwa na mvua ya kutosha na sasa mvua kunyesha chini ya
wastani uliozoeleka.
Wilaya ya Longido inakadiriwa kuwa na mifugo 918,248, ambao ni Ng’ombe, Mbuzi, Kondoo na Punda na hupata mvua ya
wastani kiasi cha 500mm hadi 900mm kwa mwaka,
hali inayosababisha ukame wa mara kwa mara.
Mifugo
katika wilaya hiyo imeathirika kwa kukosa malisho ya uhakika. Hali duni ya
mifugo imechangia kushuka kwa bei ya mifugo na
kuathiri uchumi wa kaya za wilaya hiyo unaotegemea mifugo kama chanzo kikuu cha
mapato yao ya kila siku.
Kijiji cha Kimokowa ni miongoni mwa vijiji vilivyoathirika na mabadiliko
ya tabianchi. Mwenyekiti wa kijiji hicho Killel Mollel amesema wameamua kutenga
maeneo ya nyanda za malisho ili kuyatunza kwa ajili ya malisho ya mifugo.
“Tumekumbwa na ukame mkubwa katika kijiji chetu hivyo tumeona ni vizuri kutenga maeneo maalumu ya malisho ambayo hayatavamiwa kwani tumejiwekea mpango bora wa matumizi ya ardhi ambayo yanakataza uvamizi wa maeneo hayo ili mifugo yetu ipate chakula muda wote,” amesema.
Naomi Mollel mkazi wa kijiji cha Kimokowa amesema
ameshuhudia ukame mkubwa kwa miaka mitatu mfululizo
kuanzia 2020 mpaka 2023 ambao umeathiri nyanda za malisho na kuathiri maisha
yao kwa sababu wanategemea mifugo kupata mahitaji yao ya kila siku.
Anasema wameshauriwa na wataalamu wa mabadiliko ya tabianchi
kuondoa mimea vamizi ili kuhakikisha nyasi za asili zinaota za kutosha katika nyanda za malisho ambazo
zitasaidia kuipatia mifugo yao chakula cha kutosha kwa mwaka mzima.
David Laizer mkazi wa kijiji ncha Orbomba anakiri mifugo yake kufa
kutokana na ukame na michache iliyopona analazimika kuipeleka nje ya kijiji
hicho kutafuta sehemu yenye malisho ya kutosha.
Mwenyekiti wa Serikali
ya Kijiji cha Orbomba,
Kashilo Alais anasema serikali ya kijiji imechukua hatua za haraka kudhibiti uchomaji wa mkaa na
ukataji wa miti katika kijiji hicho ili kuwa na misitu itakayosaidia mvua
kunyesha kwa kiwango cha kutosha.
Anasema serikali imechukua hatua hiyo baada ya kuona hali ya ukame imezidi na mifugo kufa
na watu kuishi kwa tabau kwani mifugo ndiyo chanzo kikuu cha mapato ya familia
nyingi kijijini hapo.
Aidha baadhi ya
watafiti, wafugaji na wahifadhi wanasema kuwa nyanda hizo za malisho zinapaswa
kutunzwa na kusimamiwa vema ili kuepusha
kuvamiwa na mimea vamizi inayozuia uoto wa majani ya asili ambayo ni chakula
cha mifugo.
Mimea hiyo vamizi ya Prosopis juliflora (Mrashia), Parthenium
hysterophorus (Gugu Karoti), Astripomoea hyoscyamoides (Gugu Kongwa), Ipomoea
hycanoides (ndelemeti), Chromolaena Odorata (Amachabongo), Dichrostachis
cinerea (Ndunduru) Acacia nubica (Oldepe) na Solanum incunum (Ndulele) inatajwa
kuathiri malisho ya wanyamapori na mifugo kwani licha ya kutoliwa na wanyama
pia inazuia uoto wa majani ya asili ambayo ni chakula cha mifugo na wanyama
hao.
Taarifa toka kwa mashirika ya TAWA, TNRF, CORDS, TAFORI na CABI yanayotekeleza
miradi ya kupambana na mimea vamizi katika nyanda za malisho zinasema kuwa
mimea hiyo vamizi imeathiri maeneo mengi ya nyanda za malisho katika wilaya ya
Longido.
Mtafiti wa Taasisi ya utafiti wa Misitu (TAFORI), Dkt. Richard
John amesema kumekuwa na ongezeko la mimea vamizi katika nyanda za maisho na kutaja
miti ya mrashia ambao kitaalamu hujulikana kwa jina
Prosopis Juliflora kuwa inaaathiri sana nyanda za
malisho kwani hutumia kiasi kikubwa cha maji na hivyo kusababisha ukame.
Ameshauri kamati za mazingira za vijiji Wilayani Longido kuweka
mkakati kabambe wa kuhakikisha miti hiyo inakatwa mapema na mimea vamizi
inaondolewa ili kuongeza ustawi wa malisho ya mifugo katika maeneo maalumu
yaliyotengwa.
Waziri wa Nchi Ofisi
ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Dkt.Seleman Jafo, akiwa katika kikao
cha siku nne na wadau wa mazingira jijini Arusha mwezi Oktoba mwaka 2022
kujadili mkakati wa nchi kuongeza uwezo wa kupata fedha za kukabiliana na mabadiliko
ya tabianchi alisema serikali imepanga kutumia dola za Marekani milion 19.2 ambazo
ni sawa na shilingi bilion 44 za Tanzania
kutekeleza Mpango wa Taifa wa Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi.
Amesema Serikali
inachukua hatua kubwa kama vile kuandaa Sera ya Taifa ya Mazingira ya mwaka
2021, Mpango Mkakati wa Kitaifa wa Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi 2021,
Mpango Kabambe wa Taifa wa Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (2022 – 2023) na
Miongozo na Kanuni za Biashara ya Kaboni, ikiwa ni jitihada za kukabiliana na
mabadiliko ya Tabianchi.
Mpango huu wa serikali ukifanikiwa kuwafikia
wakazi wa Longido na kamati zaa mazingira za kata na
vijiji vikisimamia vema nyanda hizi za malisho huenda zitawanufaisha wafugaji
wa wilaya ya Longido kuepukana na adha ya kukosa malisho ya mifugo
iliyowakabili kwa kipindi cha miaka minne sasa.
![]() |
| Musa Murdoko, mchungaji wa kanisa na Babtisti na mkazi wa kata ya Orbomba akielezea umuhimu wa kutengwa kwa nyanda za malisho |


No comments:
Post a Comment