DC NGOMA NA DC MOYO WALIVYOTEMBEA MIRERANI NA KUZAMIA MGODI WA FRANONE MINING - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Tuesday 8 August 2023

DC NGOMA NA DC MOYO WALIVYOTEMBEA MIRERANI NA KUZAMIA MGODI WA FRANONE MINING

  





Na Mwandishi wetu, Mirerani 


WAKUU wa Wilaya za Ruangwa, Hassan Ngoma na Nachingwea Mohamed Moyo, wa Mkoani Lindi wamewaongoza baadhi ya viongozi wa Wilaya zao, kuingia ndani ya mgodi wa machimbo ya madini ya Tanzanite mji mdogo wa Mirerani, Wilayani Simanjiro, Mkoani Manyara.


Ngoma, Moyo na baadhi ya viongozi hao wamezama chini ya mgodi wa mwekezaji mzawa, kampuni ya Franone Mining and Gems LTD, eneo la kitalu C na kujionea shughuli za uchimbaji madini unavyofanyika.


Akizungumza baada ya kuingia kwenye mgodi huo, Ngoma amesema lengo la ziara yao ni kujifunza namna shughuli za uchimbaji madini ya Tanzanite unavyofanyika ili nao waige mazuri.


"Tumeona shughuli za uchimbaji kwa mwekezaji mzawa kampuni ya Franone kwa kweli wanastahili pongezi kwa kufanya kazi kwa ufanisi," amesema Ngoma.


Amesema wilaya yao ya Ruangwa pia kuna uwekezaji mkubwa wa baadhi ya migodi hivyo kupitia uwekezaji wa kampuni ya Franone Mining wamejifunza kupitia madini ya Tanzanite.


"Uwekezaji uliopo hapa Franone, unapaswa kupongezwa kwani tumeshuka chini ya ardhi mgodini mita 700 kisha tukamaliza kilomita 1.2 tumeshuhudia kazi nzuri," amesema Ngoma.


Mkuu wa wilaya ya Nachingwea Hassan Moyo ambaye naye alizama kwenye mgodi huo ameipongeza kampuni ya Franone kwa kuweka miundombinu thabiti ya uchimbaji madini ya Tanzanite.


"Watanzania wanaweza tumeona vijana wamepata ajira kwenye kampuni ya Franone na wanampongeza hayati John Magufuli kwa kujenga ukuta unaozunguka migodi ya madini ya Tanzanite," amesema Moyo.


Mkurugenzi wa kampuni ya Franone Mining and Gems LTD,  Onesmo Mbise amesema wametoa ajira rasmi 328 na  zisizo rasmi 1,000.


Wilaya za Ruangwa na Nachingwea, zinachimba madini ya aina mbalimbali ikiwemo dhahabu, nickel, ganeti ya kijani, manganese, marble, gypsum na ulanga (kinywe).


Mkoa wa Lindi unatarajia kufanya maonyesho ya madini, kilimo, mifugo, misitu na fursa za uwekezaji Agosti 21 hadi Agosti 26 mwaka 2023.



No comments: