SIMANJIRO YATUMIA BILIONI MOJA KUJENGA MADARASA 17 NA MATUNDU 17 YA VYOO - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Saturday 19 August 2023

SIMANJIRO YATUMIA BILIONI MOJA KUJENGA MADARASA 17 NA MATUNDU 17 YA VYOO





Na Mwandishi wetu, Simanjiro


maipacarusha20@gmail.com


MKUU wa Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara, Dkt Suleiman Hassan Serera, amesoma taarifa ya utekelezaji wa ilani ya uchaguzi wa CCM kwa mwaka 2020/2025 kipindi cha Januari hadi Juni mwaka 2023 kwenye Halmashauri Kuu ya CCM Wilaya ya Simanjiro.


Akisoma taarifa hiyo Dkt Serera amesema Halmashauri ya Wilaya hiyo imepokea kiasi cha shilingi 1,063,900,000.00 fedha za kutekeleza miradi ya Boost katika shule za msingi kwa ajili ya ujenzi wa vyumba 17 vya madarasa na matundu 17 ya vyoo.


Ametaja shule hizo za msingi ni Endiamtu madarasa matatu na matundu matatu ya vyoo, shilingi 81,300,000 ambapo ujenzi upo hatua ya ukamilishaji.


“Shule ya msingi Loiborsiret madarasa matatu na matundu matatu ya vyoo shilingi 81,300,000 na ujenzi upo hatu ya ukamilishaji,” amesema Dkt Serera.


Amesema shule ya msingi Mbuko madarasa matatu na matundu matatu ya vyoo pia na shule ya msingi Naberera madarasa matatu na matundu matatu ya vyoo, shule ya msingi Narakauo madarasa mawili na matundu matatu ya vyoo shilingi 56,300,000.

 

Amesema shule ya msingi Saniniu Laizer imejengwa madarasa mawili ya elimu ya awali kwa shilingi 69,100,000 na ujenzi wa shule mpya ya msingi Namalulu yenye mikondo miwili na nyumba ya mwalimu shilingi 638,300,000.


Amesema kwa shule za sekondari zipo 19 kati ya hizo 17 ni za serikali na shule mbili siyo za serikali, shule za kidato cha tano na sita zipo nnne, ambapo tatu za Simanjiro, Emboree na Naisinyai ni za serikali na moja ya Mgutwa siyo ya serikali.


Amesema kwa upande wa msimu wa kilimo 2021/2022 jumla ya hekta 121,869 zililimwa mazao ya chakula na kuzalisha tani 304,686.5 na katika msimu wa 2022/2023 hali ya uzalishaji inategemewa kuwa chini ya kiwango kutokana na ukosefu wa mvua ambao umejitokeza maeneo mengi ila tathimini ya uzalishaji bado inaendelea kufanyika.


“Wakulima wapatao 16,000 walipatiwa mafunzo juu ya kanuni za kilimo bora ili waweze kufanya kilimo chenye tija sambamba na uhifadhi wa mazao,” amesema Dkt Serera.


Amesema kutokana na uhaba wa chakula na bei kuwa juu wilaya iliomba kiasi cha tani 525 za mahindi ya chakula cha bei nafuu na kupatiwa tani 494 kilichosambazwa wilayani.


Amesema kwa upande wa sekta ya mifugo na uvuvi kuna jumla ya ng’ombe 450,187 mbuzi 418,653 kondoo 237,603 punda 22,217 ngamia 53 kuku 94,229 na nguruwe 896.


Amesema ujenzi wa majosho kwa ufadhili wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, mawili vijiji vya Loiborsoit A, na Kitwai A umekamilika na matano vijiji vya Lerumo, Gunge, Loiborsoit B, Namalulu na Kitiangare umekamilika Julai 30 mwaka 2023. 


“Ujenzi wa josho na birika la kunywea maji mifugo kwa ufadhili wa fedha kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais kupitia mradi wa EBARR umekamilika na ujenzi wa gharala katika kijiji cha Langai unaendelea,” amesema Dkt Serera. 


Wilaya ya Simanjiro ina eneo la kilometa za mraba 20,591 na ipo kwenye nyanda kame na mbuga, hupata mvua za wastani wa kati ya milimita 400 na 500 kwa mwaka.


Wilaya ya Simanjiro inapakana na wilaya ya Monduli upande wa kaskazini magharibi ni Arumeru mkoani Arusha, upande wa kaskazini ni wilaya za Hai na Moshi mkoani Kilimanjaro, upande wa kusini ni wilaya za Kondoa mkoani Dodoma, Babati na Kiteto, upande wa magharibi ni wilaya za Mwanga, Same na Kilindi na upande wa mashariki ni Korogwe mkoani Tanga.


Kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022 Simanjiro ina watu 291,169 kati yao wanaume ni 144,654 na wanawake ni 146,515.

 

Wakazi wa Simanjiro wanajihusisha na shughuli za kilimo, ufugaji, uvuvi, uchimbaji madini, biashara na ujasiriamali ila shughuli kuu za uchumi asilimia 80 ni kilimo na ufugaji.

No comments: