DED MAKOTA AZIPONGEZA NGO’s ZA SIMANJIRO - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Saturday 19 August 2023

DED MAKOTA AZIPONGEZA NGO’s ZA SIMANJIRO

 




Na Mwandishi wetu, Simanjiro


MKURUGENZI Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara, (DED) Gracian Max Makota ameyapongeza mashirika yasiyo ya kiserikali Simanjiro kwa kusaidiana na serikali katika kusaidia jamii na kuwaletea maendeleo.


DED Makota ameyasema hayo wakati akizungumza kwenye mkutano wa nusu mwaka wa asasi zisizo za kiserikali (NGO’s) za eneo hilo uliofanyika kwenye kata ya Terrat.

 

Amesema NGO’s zilizopo Simanjiro zimefanikisha maendeleo mengi hivyo amezipongeza kwa kusaidiana na serikali, kuiletea jamii maendeleo na kuahidi kushirikiana nao kwa pamoja.


“Kazi mnayofanya ilipaswa kufanywa na serikali ili wananchi wake wapate maendeleo hivyo, tunawapongeza kwani tunashirikiana kwa lengo la jamii inufaike,” amsema DED Makota.


Hata hivyo, amewataka viongozi wa asasi hizo kuhakikisha wanaepuka kushiriki kufanya shughuli zilizo nje ya utu, maadili, desturi na utamaduni wa mtanzania.


Mwenyekiti wa umoja wa asasi zisizo za kiserikali wilayani Simanjiro, Edward Loure Parmelo amesema asasi hizo 47 zinafanya kazi kwa sekta tofautii ikiwemo mazingira, afya, elimu na ardhi.


Loure ni mratibu wa asasi ya Ujamaa Community Resource Team (UCRT), ambaye April 18 mwaka 2016 alitunukiwa tuzo ya mazingira ya Goldman jimbo la San Francisco, Marekani.


Amesema kupitia shirika hilo la UCRT wamefanikisha upimaji wa ardhi kwa vijiji 27 vya wilayani Simanjiro na kupanga matumizi bora hivyo kuepusha migogoro mingi ya ardhi.


Amesema kupitia fedha za wahisani, asasi hizo zinafanya kazi zao ipasavyo katika kuhakikisha wanawanufaisha watu wa Simanjiro kwani ndiyo malengo yao katika taasisi hizo.

 

“Hata hivyo, kuna changamoto ya baadhi ya wanasiasa wa  Simanjiro kugeuza migogoro ya ardhi kuwa rasilimali ya kuendelea kuwa kwenye madaraka,” amesema Loure. 


Mkurugenzi wa shirika la Helping heats initiative na Jamii yangu begani, Lowassa Lormuje amesema watu wanapaswa kuelimishwa juu ya matumizi sahihi ya dawa ili kuondokana na matatizo yatokanayo na utumiaji mbaya ikiwemo vifo, ulemavu na afya ya uzazi.


Lowassa amesema takwimu za shirika la afya ulimwenguni (WHO) za mwaka 2015 zinaonyesha kuwa asilimia 80 ya watu duniani ikiwemo Tanzania wanajitibu wenyewe.


Mkurugenzi wa shirika la Saidia wana jamii Tanzania (SAWATA) Mohamed Mughanja amesema wana mpango wa kuandaa uokotaji taka migodini ili kuhakikisha mazingira ya wachimbaji madini ya Tanzanite yanakuwa safi.

 


No comments: