UKOSEFU WA MAJI SAFI NA SALAMA UNAVYOATHIRI AFYA ZA WAKAZI WA OLMOLOG WILAYANI LONGIDO - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Wednesday 16 August 2023

UKOSEFU WA MAJI SAFI NA SALAMA UNAVYOATHIRI AFYA ZA WAKAZI WA OLMOLOG WILAYANI LONGIDO

 



Baadhi ya akina Mama wa kata ya Olmolg wilayani Longido wakiwa na ndoo tupu za maji


 

NA: ANDREA NGOBOLE, Longido

 maipacarusha20@gmail.com


Maji safi na salama yenye ubora unaokubalika kwa matumizi ya nyumbani na usafi wa mazingira ni muhimu katika kulinda afya za wananchi, maendeleo ya kiuchumi na kijamii.


Aidha utumiaji wa maji yasiyo safi na salama huchangia katika kusababisha mlipuko na kuenea kwa magonjwa kama kuhara na kipindupindu ambayo husababisha vifo.


Kwa mujibu wa Sera ya Maji ya Mwaka 2002 nchini Tanzania, inasema hadi kufikia mwaka 2022 maji safi na salama yawe yanapatikana vijijini kwa asilimia 85 na mjini kwa asilimia 95.


Umoja wa Mataifa unaelekeza kuwa maji safi na salama yanatakiwa yapatikane umbali usiozidi mita 1,000 kutoka kwenye nyumba ya mtumiaji, pia atumie dakika zisizozidi 30 kwenda kuchota maji na kurudi nyumbani na gharama za upatikanaji wa maji hayo yasizidi asilimia tatu ya pato la kaya husika.


Hata hivyo, wakazi wa vijiji vya Elerai, Lerangwe na Olmolog vinavyounda kata ya Olmolog wilayani Longido mkoani Arusha wanakosa huduma ya maji safi na salama hali inayowalazimu kwenda kilomita 10 kupata maji hayo kutoka kijiji cha Muton Wilayani Siha Mkoani Kilimanjaro.


Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) Wilayani Longido Mkoani Arusha wanasimamia ujenzi wa Tenki la maji safi na salama toka chanzo cha maji ya mto Simba na kisha kusambaza kwa kaya za vijiji katika kata ya Olmolog Wilayani Longido Mkoani Arusha ulioanza kujengwa mwaka 2021 na kupaswa kukamilika Juni 2022. Mradi wa tenki hili la maji na usambazaji wa maji ulitarajiwa kugharimu shilingi milioni 900 lakini mpaka sasa August 17, 2023 bado haujakamilika.


Meneja RUWASA Wilaya ya Longido, Petro Nyerere, alisema mradi huo umechelewa kukamilika kwa sababu ya ukosefu wa fedha ya kumlipa mkandarasi na kwa kuwa pesa zimekwishapatikana na kutolewa kwa mkanadarasi watahakikisha mradi unakamilika ndani ya Miezi sita toka sasa.


Kata ya Olmolog ina vyanzo vya maji viwili vya Olomoni na Sowetu. Maji hayo hufaa kwa matumizi ya mifugo, umwagiliaji na matumizi ya usafi majumbani isipokuwa kunywa tu hivyo wakazi hao hulazimika kutembea umbali wa kilomita 10 hadi 15 kwenda kuchota maji safi na salama katika kijiji cha Muton Wilaya ya Siha, Mkoani Kilimanjaro.


Neema Mollel mkazi wa kijiji cha Olmolog anasema changamoto ya kusaka maji safi na salama kwa akina mama wa kijiji hicho ni kubwa kwani huamka usiku sana kwenda kuchota maji safi na salama kijiji cha Muton Wilaya Siha Mkoani Kilimanjaro ili kupata maji hayo na hivyo kushindwa kufanya kazi za uzalishaji kwa ufanisi kwa sababu ya uchovu wa kwenda mbali kuchota maji.


  “Kwa kweli hali ni mbaya sana hapa. Tunaamka usiku mnene kusaka maji na usiku una mambo mengi mabaya. Kwahiyo tunalazimka kwenda kwa vikundi vya akina mama watatu mpaka wane. Tunatumia punda kubeba angalau madumu manne ya maji kwa punda mmoja hivyo tunachota maji ya kututosha matumizi ya wiki nzima,” alisema.


Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Elerai, Simon Ole Nassari anasema kwa kuwa kijiji hicho kinakosa huduma ya maji safi na salama, wakazi wake wameelimishwa umuhimu wa kuvuna maji ya mvua na kuhifadhi katika matenki kwa ajili ya matumizi. Hata hivyo maji hayo hayakidhi mahitaji kwa mwaka mzima kwani mvua ni chache.


 “Serikali ya kijiji inakusudia kuongeza matenki ili kuvuna maji mengi ya mvua lakini pia kutafuta dawa za kutibu maji ya visima ili wananchi wawe huru kutumia maji hayo,” alisema.


Diwani wa Kata ya Olmolog, Loomoni Olesiato Mollel, anasema kuwa upatikanaji wa maji safi na salama ni tatizo kubwa linalowakabili wakazi wa kata yake licha ya juhudi kubwa wanayotumia kutibu maji yaliyopo katika matenki saba ya kuhifadhia maji katika vijiji vitatu vinavyounda kata hiyo.


Amesema kuwa ujenzi wa Tenki la maji safi na salama unaojengwa katika kata yake ulipaswa ukamilike Juni 2022 lakini mpaka sasa umefikia asilimia 60 ya ujenzi na kumtaka mkandarasi kuongeza kasi ya kukamilisha ujenzi huo kwani malipo ya fedha yamekamilika kwa sasa.


Wilaya ya Longido yenye kata 18 inakabiliwa na chanagamoto ya Usamabazji wa maji safi na salama katika kata hizo, ambazo hutegemea chanzo cha maji Mto Simba uliopo wilayani Siha mkoani Kilimanjaro.


Naibu Waziri wa Maji, Mhandisi Maryprisca Mahundi akizungumza wakati wa ziara ya ukaguzi wa miradi ya maji wilayani Longido hivi karibuni amesema serikali itatoa shilingi milioni 200 kwa ajili kuchimba visima 14 vya maji safi na salama kwa matumizi ya watu.


“Serikali inataka kila kata na kijiji kupata maji kwa haraka na ya uhakika na sisi kama wizara tuko hapa kuhakikisha tunasimamia jambo hilo ili kuendana na maono ya Rais Samia ya kumtua mama ndoo kichwani,” alisema. 

 

Naibu Waziri wa Madini, Dkt Stephen Kiruswa ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Longido amesema ukosefu wa maji safi na salama kwa wakazi wa kata ya Olmolog ni tatizo kubwa kwa akina Mama na watoto kwani alipotembelea kata hiyo alishuhudia akina mama waliobeba ndoo tupu za maji na kumlalamikia tatizo hilo linawaumiza sana na kutoa ahadi ya usafiri wa kupeleka vifaa vya ujenzi wa Tank kubwa la kuhifadhia maji maji safi na salama kabla ya kusambazwa mabomba kwa wanakijiji ili kuwakwamua akina mama hao na adha ya maji inayowakumba.


Daktari wa wilaya ya Longido Seleman Mtenjela anasema kwamba kukosekana kwa maji safi na salama katika kata hiyo kulipelekea magonjwa ya mlipuko kama kuhara na homa ya matumbo, ambapo watoto wa umri miaka 5-13 wapatao 100 ndiyo waliongoza kuugua, Watu wazima 70 kati yao Akina mama 40 waliugua na ndipo Wakaja na mkakati wa kuelimisha wanavijiji hao watumie maji yaliyotibiwa kwa vidonge lakini pia kuchemsha maji ya kunywa. Hali hii ilisaidia kupunguza magonjwa ya mlipuko kwa wakazi hao.

 

No comments: