RPC KATABAZI: WAANDISHI MANYARA KEMEENI UKATILI NA WANAOCHUKUA SHERIA MKONONI - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Wednesday 1 November 2023

RPC KATABAZI: WAANDISHI MANYARA KEMEENI UKATILI NA WANAOCHUKUA SHERIA MKONONI

 





Na Mwandishi wetu, Babati


KAMANDA wa polisi wa Mkoa wa Manyara, kamishna msaidizi (ACP) George Katabazi ametoa wito kwa waandishi wa habari kutoa elimu kwa jamii kwa kuandika habari na makala ili waache kufanya ukatili wa kijinsia hususani wa kingono na wasijichukulie sheria mkononi.


Kamanda Katabazi ameyasema hayo mjini Babati kwenye mdahalo wa ulinzi na usalama wa waandishi wa habari, uliondaliwa na shirikisho la vilabu vya waandishi wa habari nchini UTPC na kuhusisha klabu ya waandishi wa habari mkoa wa Manyara (MNRPC) na polisi.


Amesema waandishi wa habari wana uwezo mkubwa wa kutumia taaluma yao ili kutoa elimu kwa jamii hivyo kupitia redio, TV, magazeti na mitandao kukemea hayo.


Amesema matukio ya ukatili wa kijinsia hasa wa kingono na watu wanaojichukulia sheria mkononi yanakuwa yanatokea mara kwa mara hivyo yanatakiwa kukemewa.


"Toeni elimu kupitia kalamu, kemeeni kwani vyombo vya habari vina nafasi kubwa mno ya kubadilisha mtazamo wa jamii hivyo tumieni fursa hiyo kwa kuhabarisha changamoto hizo ambazo zinatokea," amesema kamanda Katabazi.


Hata hivyo, kamanda Katabazi amesema askari polisi wanne wamefukuzwa kazi kwa makosa ya kupokea rushwa na utovu wa nidhamu wakati wakiwa kwenye utendaji kazi wao.


Akizungumza bila kuwataja majina askari hao wanne, kamanda Katabazi amesema polisi imewafukuza kazi hivi karibuni kwa makosa ya kupokea rushwa na utovu wa nidhamu.


Mkurugenzi mtendaji wa UTPC Kenneth Simbaya amesema mdahalo huo umelenga kuendeleza ushirikiano kati ya polisi na waandishi wa habari katika kuitumikia jamii bila mikwaruzo kwani wanategemeana.


Simbaya amesema waandishi wa habari wanawajibika kwa jamii siyo kwa viongozi hivyo ni muhimu kushirikiana na polisi ili waweze kutimiza wajibu wao kwa amani.


Mwenyekiti wa klabu ya waandishi wa habari mkoa wa Manyara, (MNRPC) Zacharia Mtigandi amempongeza kamanda Katabazi kwa namna anavyoshirikiana na waandishi wa habari hasa katika kutoa taarifa za matukio mbalimbali.


"Tumekuwa tukipata ushirikiano mkubwa kwa kamanda Katabazi hivyo kuturahisishia ufanyaji wa kazi zetu, hivyo nampongeza sana kwa namna anavyofanya kazi zake," amesema Mtigandi.


Ofisa program, mafunzo, utafiti na machapisho wa UTPC, Victor Maleko amesema mdahalo kama huo utafanyika tena wilayani Kiteto na kuhusisha polisi na waandishi wa habari.


"Lengo la UTPC ni kuhakikisha waandishi wa habari wanatimiza majukumu yao ilimradi hawavunji sheria za nchi na polisi nao wanatimiza majukumu yao kwani hakuna aliye juu ya sheria," amesema Maleko.


Mwandishi mwingine wa habari, Mohamed Hamad amesema kamanda Katabazi amekuwa mfano bora kwa makamanda wa polisi kwa namna anavyotoa ushirikiano kwao.



No comments: