SERIKALI YAJENGA CHUO CHA UALIMU NGORONGORO - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Friday 17 November 2023

SERIKALI YAJENGA CHUO CHA UALIMU NGORONGORO

 




Na Elinipa Lupembe - Arusha


maipacarusha20@gmail.com


Kutokana na ongezeko la wanafunzi wanaoandikishwa kuanza darasa la awali, la kwanza na kidato cha tano, linalotokana na sera ya elimu bila malipo, serikali inawekeza nguvu katika ujenzi wa vyuo vya ualimu vya kati.


Halmashauri ya Ngorongoro ni miongoni mwa halmashauri zilizonufaika na mpango huo, kwakupata shilingi bilioni 3.4, kwa ajili ya ujenzi wa chuo cha Ualimu Ngorongoro, lengo likiwa ni kuzalisha walimu wa ngazi ya Cheti na Astashahada, walimu watakao kwenda kufundisha shule za msingi na sekondari.


Mkuu wa mkoa wa Arusha, Mhe. John V.K.Mongella, amebainisha kuwa, serikali ya awamu ya sita, imedhamiria kuhakikisha, sekta ya elimu inajitosheleza ili wanafunzi wapate ujuzi na maarifa na kuja kuwa watalamu wabobezi wa kulitumikia Taifa la Tanzania.


"Ili kupata watalamu wenye ujuzi na maarifa, lazima uwekeze kwenye elimu na sekta mtambuka, tunafahamu elimu ndio nguzo mama ya maendeleo ya nchi yoyote dunia, Rais wetu Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan yuko 'serious' na hili, ni jukumu letu watanzania, kumuunga mkono ili kufikia malengo ya serikali yetu"Amesema Mhe. Mongella


Ameongeza kuwa licha ya vijana wa kitanzania kunufaika na ujenzi wa chuo kwa kupata elimu, bado ni fursa kwa jamii nzima, wapo wengine watapata ajira, fursa za kibiashara kwa inayozunguka eneo hilo, lakini ongezeko la watu watakaofanya shughuli mbalimbali, litakaloleta mabadiliko ya kifkra, kiuchumi na kijamii pia.


Naye Mkurugenzi Mtendaji, halmashauri ya Ngorongoro, Nassor Shemzigwa, amethibitisha kuwa, uwepo wa chuo hicho wilayani hapo,  kitawapa fursa vijana wa eneo hilo kuvutika, kupata elimu ya uwalimu karibu na nyumbani, jambo ambalo kimsingi itawapunguzia wazazi gharama za kufuata elimu hiyo mbali kwa kuzingatia  Jiografia ya eneo hilo kuwa pembezoni kabisa mwa nchi ya Tanzania.


Amesema kuwa, ujenzi ukao katika hatua za mwisho za ukamilishaji, tunaendele kuwasimamia  mafundi kwenda kwa kasi,  ili majengo yakamilike, tunafuatilia usajili pamoja na hati miliki ya eneo hilo, tuna uhakika, mwaka ujao wa masomo chuo kianze kufanya kazi kama yalivyo makusudio ya serikali ya awamu ya sita ya mama yetu Samia Suluhu Hassan" Ameweka wazi Mkurugenzi huyo.


James Nyangusi, mkazi wa Ngorongoro, hakusita kuishukuru serikali ya awamu ya sita, kwa kuwajengea chuo hicho na kuongeza kuwa, Serikali ya mama Samia imeleta maendeleo makubwa Ngorongoro tofauti na hapo awali, walisahaulika kutokana na umbali.


"Tunamshukuru Mama Samia, tunamuombea kwa Mungu, ametupa miradi mingi sana, tunashangaa kila siku hela imeingia, ya kujenga shule, barabara, kituo cha afya, maendeleo yamekuwa mengi na kwa haraka, tunamuahidi kufanya kazi kwa bidii ili kazi iendelee kama anayosema mama yetu" Amesema Nyangusi


Awali mradi wa ujenzi wa chuo cha Ualimu Ngorongoro,  unatekelezwa na Serikali kwa gharama ya shilingi bilioni 3.4, kupitia mradi wa ESP chini ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia na unatarajia kuanza kupokea wanafunzi mwaka ujao wa masomo.

No comments: