WAZIRI UMMY MWALIMU AWATAKA MADAKTARI WA MIKOA KUDHIBITI UUZAJI HOLELA WA DAWA ZA ANTIBIOTICS - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Friday 17 November 2023

WAZIRI UMMY MWALIMU AWATAKA MADAKTARI WA MIKOA KUDHIBITI UUZAJI HOLELA WA DAWA ZA ANTIBIOTICS

 

Waziri wa Afya Ummy Mwalimu akizungumza katika kongamano la tatu la usugu wa vimelea dhidi ya dawa jijini Arusha mapema leo

Professa Tumaini Nagu Mganga mkuu wa Serikali akizungumza katika kongamano la tatu la usugu wa vimelea dhidi ya dawa jijini Arusha mapema leo 


Na: Andrea Ngobole, Arusha


maipacarusha20@gmail.com


Waziri wa Afya Ummy Mwalimu amewataka waganga Wakuu wa Mikoa na wilaya, kufuatilia na kufanya ukaguzi wa mara kwa mara katika maduka ya dawa ili kudhibiti uuzwaji holela wa dawa  Antibiotics bila cheti cha daktari.


Waziri Ummy ameyasema hayo Leo Novemba 17,2023 jijini Arusha wakati  wa kufunga kongamano la tatu la usugu wa vimelea vya magonjwa dhidi ya dawa za binadamu na mifugo.


Amesema Afya Bora ndiyo msingi thabiti wa maendeleo ya Taifa hivyo ni vema elimu kwa jamii isambazwe kufahamu madhara ya kutumia dawa za antibiotics bila kupewa cheti cha daktari.


Amesisistiza kuwa wataalamu  wa Afya ni lazima wazingatie muongozo wa Taifa wa matibabu kwa kutoa Elimu juu ya madhara ya matumizi yasiyo sahihi ya dawa kwa wagonjwa.


Awali akimkaribisha waziri Ummy, Mganga mkuu wa Serikali Profesa Tumaini Nagu amesema kuwa usugu wa vimelea dhidi ya dawa ni janga la kimataifa  lakini ni janga kubwa zaidi katika nchi zilizo kusini mwa jangwa la Sahara ikiwemo Tanzania na kusababisha vifo kwa watu 


Amesema katika kongamano hilo wameweka mpango mkakati wa kushirikiana katika tafiti za kupambana na usugu wa vimelea dhidi ya dawa kwani imeonekana kuwa ndiyo njia Bora zaidi ya kupunguza athari za usugu wa vimelea sugu dhidi ya dawa.


Akiwasilisha mada   juu ya kupambana na usugu wa vimelea Professa Robinson Mdegela amesema wameweka mikakati ya kuongeza uelewa kwa jamii na mabadiliko ya tabia kuhusu matumizi sahihi ya dawa, kuzuia na kupambana na maambukizi na kutumia dawa iliyo sahihi.


Amesema muunganiko kati ya binadamu na wanyama katika chakula na dawa ni mkubwa hivyo jamii inapaswa kuwa makini KATIKA kudhibiti matumizi yasiyo sahihi ya dawa ili kupunguza usugu wa vimelea dhidi ya dawa.


Professa Jeremiah Semi akiwasilisha  mada katika Kongamano hilo amesema mtu anapotumia dawa isiyo sahihi hupelekea mtu kutopona ugonjwa wake  na kusababisha vifo.


Kongamano hilo la siku mbili limefungwa kwa kuwekwa maazimio ya kuendeleza uelewa kwa jamii juu ya matumizi sahihi ya dawa, pia kumaliza dozi wanazoandikiwa na madaktari pia kuzinduliwa kwa wiki ya uhamasishaji matumizi sahihi ya dawa ili kupunguza usugu wa vimelea dhidi ya dawa inayoanza kesho tarehe 18 Hadi 24/11/2023

No comments: