TAMWA YAFANYA KUMBUKUMBU YAKE YA MIAKA 36 KWA KISHINDO, Matunda ya kazi ya waandishi habari wanawake Tanzania - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Saturday 25 November 2023

TAMWA YAFANYA KUMBUKUMBU YAKE YA MIAKA 36 KWA KISHINDO, Matunda ya kazi ya waandishi habari wanawake Tanzania

 




Na Elizabeth Marealle


maipacarusha20@gmail.com


Rais Samia Suluhu Hassan atakuwa mgeni rasmi wakati wa mkutano kusherehekea miaka 36 ya Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA). 


Inatarajiwa baada ya kuhutubia mkutano huo  utakaofanyika Dar es Salaam tarehe 28 hadi 29 Novemba, Rais atazindua mradi maalumu wa  TAMWA. 


Tulikuwa wanahabari wanawake 13 tulioanzisha TAMWA. Tulifanya kazi kwa kujitolea kwa hali zote ili kufanikisha malengo yetu. Tulijitoa kwa muda na mali kwa kuchangia kifedha. 


Tulianza katika sebule ya marehemu Nelly Kidela ambaye alikuwa miongoni wa waanzilishi. 


Hicho ni kipindi baada ya kuwa na Mwongo wa Wanawake wa Umoja wa Mataifa ambapo baadhi ya wana TAMWA walishiriki katika baadhi ya matukio kabla, kule Nairobi na baadaye  Beijing. China. 


Kwa hiyo, TAMWA tuliyoitaka sio ya kujiangalia sisi wadau pekee, bali ilikuwa ni kukazia macho hali iliyopo katika jamii kwa ujumla wake. Maono ya TAMWA ni: "Kuwa na jamii ya Kitanzania iliyo na amani na inayo heshimu haki za binadamu kwa mtazamo wa kijinsia." 


Licha ya kuanzishwa miaka 36 iliyopita chama hichi kiko imara hadi sasa.  Wanachama wake wanakaribia 200. Sasa TAMWA ni jina la mfano wa utetezi wa haki za binadamu hadi ngazi ya kaya nchini.


Baada ya miaka10 ya ushawishi wa TAMWA na wadau wengine hatimaye Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mwaka 1998 likatunga Sheria ya Masuala ya Kujamiiana. Lengo ni kuzuia ukatili na kulinda heshima, hadhi, utu na haki za wanawake na watoto. Inajulikana kama "The Sexual Offences Special Provisions Act of 1998" (SOPSA). 


TAMWA ilizindua gazeti la "Sauti ya Siti" lililoibua masuala ya uchunguzi na utafiti na makala hizo ziliandikwa na waandishi wanawake na wanaume. Kadiri siku zilivyokwenda watu binafsi, taasisi, asasi, Serikali na wadau wengine walianza kuunga mkono jitihada za TAMWA kupiga vita ukiukwaji wa haki za binadamu kwa mtazamo wa kijinsia. 


Wakati huo ilikuwa huko  Zanzibar msichana akipata mimba alifungwa jela. Na kama ni mwanafunzi hakuruhusiwa kurudi tena kusoma shule kwa mujibu wa Sheria iliyojulikana kama: "Sheria ya Wanawali ya mwaka 1985".


Kwa jitihada na ushawishi wake,  TAMWA ilimwendea hadi, Mheshimiwa Rais, Samia Suluhu Hasan, ambaye kwa wakati huo alikuwa Waziri Zanzibar aliyekuwa na dhamana ya masuala ya kijinsia. Na yeye alilibeba tatizo hilo hadi hatimaye ile Sheria ikafutwa. 


TAMWA ilitumia vyombo vya habari kuhamasisha na kushawishi ili kuwatia moyo wadau waliokuwa tayari kugombea nafasi za kuchaguliwa za kisiasa. Baada ya kampeni hiyo kwa kushirikiana na wadau wengine, wanawake wengi wako kwenye nafasi za kisiasa na uongozi katika nyanja tofauti tofauti.


Lilipozuka tatizo la vifo vya tauni Lushoto 1990 wanawake na watoto wengi walikufa. TAMWA ikaanzisha kampeni kwa njia ya vyombo vya habari. Utafiti ulionesha kuwa wanawake na watoto ndio waliathirika zaidi kwa vifo kuliko wanaume. Sababu ni kuwa wanawake walikuwa wakilala chini; hivyo kushambuliwa zaidi na viroboto kutokana na kuwepo panya wengi kwenye eneo hilo. Tatizo liliendelea kwa muda mrefu bila suluhu. 


TAMWA iliitisha mkutano wa Waandishi wa habari kueleza matokeo ya utafiti. Vichwa vya habari magazetini, TV na redio vilifanya wadau wengi kuchukua hatua mara moja. Baada ya jitihada za Serikali na wadau wengine kukabili hali iliyokuwepo, ugonjwa wa tauni sasa ni historia Wilaya ya Lushoto.


TAMWA haikufanya kazi peke yake. Ilifungwa mkono kwa dhati na Serikali kwa njia mbalimbali. Asasi, taasisina mashirika mengi ya Serikali na yasiyo ya kiserikali yalihusika kutekeleza yaliyoibuliwa na TAMWA.


Katika kampeni hizi za kutumia vyombo vya habari, wana TAMWA walitumia kalamu zao na vinasa sauti kufanikisha kazi yao ya uandishi wa uchunguzi kuibua kero za ukiukwaji wa haki kwa wanawake na watoto.  


Hadi sasa Chama hicho kimetekeleza miradi 145 iliyogusa maisha ya watu wengi nchini Tanzania.




No comments: