BILA USALAMA HAKUNA MAENDELEO- ASP. NCHIMBI - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Saturday, 2 December 2023

BILA USALAMA HAKUNA MAENDELEO- ASP. NCHIMBI

 

Mkuu wa Polisi Jamii wilaya ya Monduli Mrakibu Msaidizi wa Polisi (ASP) Rashid Nchimbi, akiongea na baadhi ya viongozi wa vijiwe vya boda boda vilivyopo wilayani humo juu ya kuwepo kwa mahusiano bora kati yao na Jeshi la Polisi, kikao hicho kilifanyika mapema leo katika kituo cha Polisi Monduli.



 Na Mwandishi wetu_ Monduli 


maipacarusha20@gmail.com


Mkuu wa Polisi Jamii wilaya ya Monduli Mrakibu wa Polisi (ASP) Rashid Nchimbi amesema kwamba msingi wowote wa maendeleo unatokana na hali thabiti ya usalama.


Amesema hayo mapema leo ofisini kwake wakati anaongea na baadhi ya viongozi wa  vijiwe vya boda boda vilivyopo wilaya ya Monduli mjini.


ASP. Nchimbi alisema kwamba, sehemu yoyote ambayo haina utulivu katika usalama basi hakuna kinachoweza kufanyika hususani upande wa maendeleo.


" Kama kutakuwa na uhalifu uliokithiri itawakatisha tamaa wafanyabishara kufanya shughuli zao, hali ambayo itaathiri kipato chenu nyinyi (Madereva wa boda boda) maana hamtapata wateja wa kutoka kwenye Bar na kumbi nyingine za starehe hasa nyakati za usiku kwa kuwa maeneo hayo yatakuwa yamefungwa mapema kwa kuogopa uhalifu. 


Vile vile watu ambao ni wateja wataogopa kutembea usiku kwa kuwa watakuwa na hofu juu ya usalama wao." Alisema ASP. Nchimbi ambaye ni mkuu wa Polisi Jamii wilaya ya Monduli.


Sambamba na hilo, ASP. Nchimbi alidokeza suala la usajili wa vijiwe vyao ili wahusika waweze kutambulika badala ya kila mmoja kukaa kijiweni kiholela hali ambayo itawasidia kudhibitiana pindi mwenzao atafanya ndivyo sivyo. 


Alisema madereva wa Boda boda ni watu muhimu katika kuimarisha usalama wilayani humo kwa kuwa huwa wanakesha mpaka asubuhi hivyo ni rahisi kwao kushuhudia matukio mbalimbali yakiwemo ya kiuhalifu na kuwezesha kutoa taarifa haraka kwa Jeshi la Polisi.


Kwa upande wake mmoja wa viongozi hao wa vijiwe vya Boda boda aliyefahamika kwa jina la Teeneger Mwinyi alisema kwamba,  wanatamani kuwe na mkutano baina ya Jeshi hilo na wao ili na madereva wengine wapate elimu hiyo na hatimaye kufanya kazi kwa pamoja kwa nia ya kutokomeza uhalifu.


Wilaya ya Monduli mjini ina jumla ya vijiwe 14 vya madereva wa Boda boda ambavyo vimegawanyika katika maeneo mbalimbali.


No comments: