JIJI LA ARUSHA KUKUSANYA SHILINGI BILIONI 8.7 ZA MADENI SUGU TOKA KWA WAFANYABIASHARA - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Friday, 8 December 2023

JIJI LA ARUSHA KUKUSANYA SHILINGI BILIONI 8.7 ZA MADENI SUGU TOKA KWA WAFANYABIASHARA

 

Mkurugenzi wa Jiji la Arusha Juma Hamsini akizungumza na waandishi wa habari Ofisini kwake



Na: Andrea Ngobole, Arusha

maipacarusha20@gmail.com


Halmashauri ya Jiji la Arusha linawadai wafanyabiashara kiasi cha shilingi 8.7 bilioni ikiwa ni malimbikizo ya Kodi mbalimbali na linaandaa kuwafikisha Mahakamani ambao wamegoma kulipa.


Miongoni mwa wafanyabiashara ambao wanaodaiwa na Jiji la Arusha ni wafanyabiashara wa maduka ya Jiji zaidi 400 ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakipinga kulipa Kodi.


Akizungumza na waandishi wa habari, Mkurugenzi wa Jiji la Arusha, Juma Hamsini alisema kabla ya kuwafikisha Mahakamani wafanyabiashara hao tayari wameandikiwa notisi za kulipa madeni hayo.


"Tumezungumza nao na tumewataka waanze kulipa hata kwa awamu kabla kuwafikisha Mahakamani"alisema


Hamsini alisema, wafanyabiashara wa maduka wametakiwa kujisajili upya katika mfumo wa Tausi ambapo tayari wafanyabiashara baadhi wamejisajili na ambao watapuuza watachukuliwa hatua.


"Kwa hawa wa maduka ya kituo  kidogo cha Mabasi tunawadai zaidi ya sh 320 milioni, tayari tumeanza uchunguzi kuwabaini wanaochochea kutolipwa Kodi na tumebaini Kuna wafanyabiashara zaidi ya 200 hawana leseni za biashara zao" amesema


Amesema kama madeni yote yakikusanywa jiji la Arusha litakuwa na uwezo hadi wa kujenga Soko jipya la kisasa na kuboresha huduma nyingine za Jiji.


Mwenyekiti wa wafanyabiashara Jiji la Arusha, Locken Masawe alisema wafanyabiashara wanapaswa kufuata sheria ikiwepo kulipa Kodi na kuwa na leseni.


"Wito wangu kwa wafanyabiashara wenzangu tufuate sheria na taratibu ikiwepo kuwa na leseni za biashara "alisema.


Mwenyekiti wa kamati ya Elimu na  Maendeleo ya madiwani  wa jiji la Arusha, Isaya Doita alisema kama wafanyabiashara wote wakilipa malimbikizo ya madeni yao changamoto nyingi za maeneo katika Jiji la Arusha zitapatiwa ufumbuzi.

Jiji la Arusha ni miongoni mwa majiji yaliyofanya vizuri kati sekta za Afya, elimu na miundombinu ya Taa za barabarani na kupendezesha Jiji myakati za usiku.


No comments: