Mabalozi, Waandishi na Maafisa 200 waanza kupanda Mlima Kilimanjaro kuadhimisha miaka 62 ya Uhuru - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Tuesday, 5 December 2023

Mabalozi, Waandishi na Maafisa 200 waanza kupanda Mlima Kilimanjaro kuadhimisha miaka 62 ya Uhuru






Baadhi ya mabalozi wakiwa tayari kupanda mlima Kilimanjaro 



Na. Jacob Kasiri - Kilimanjaro.

maipacarusha20@gmail.com


Katika kuelekea kuadhimisha miaka 62 ya uhuru wa Tanganyika ifikapo Disemba 9, 2023 zaidi ya watalii 200 wa ndani na nje ya mipaka ya Tanzania wameanza safari ya kuelekea katika kilele cha Mlima Kilimanjaro kupitia lango la Marangu.

Katika safari hiyo wamo waheshimiwa mabalozi 11 wanaiwakilisha Tanzania katika mataifa mbalimbali, akiwaaga watalii hao, Mkuu wa Wilaya ya Moshi Mjini Mhe. Kisare Makori alisema, "Kupanda kwa Waheshimiwa mabalozi katika kilele hiki kirefu kuliko vyote barani Afrika kuna manufaa makubwa kwa Taifa kwani mnatazamwa na kufuatiliwa na mataifa mnayotuwakilisha, hivyo msisite kurusha tukio zima la (Twenzetu Kileleni), vivutio vya utalii mtakavyoviona na fursa za uwekezaji zinazopatikana katika hifadhi hii ili kuvutia watalii na wawekezaji wengi zaidi.

Vilevile, Mkuu wa Wilaya ya Moshi Mhe. Makori aliongeza kuwa Tanzania ina vivutio vingi na vyenye maajabu mengi yanayovutia, hivyo mnapoviona vivutio na mandhari nzuri ya hifadhi hizi ni rahisi kuvielezea na kuvinadi tofauti na mtu aliyesoma katika majarida mbalimbali.

Aidha, Mkuu wa Wilaya huyo, pia alikemea vitendo vya uharibifu wa mazingira unaopelekea kupungua kwa barafu katika kilele cha Mlima Kilimanjaro alisema, "Nitoe wito kwa Watanzania wanaoishi mwambao wa Pwani kuwajibika kuhifadhi maeneo yao, kwani yana mchango mkubwa katika uwepo wa barafu katika Mlima Kilimanjaro".

Amidi wa muda wa Mabalozi Mhe. Maadhi Maalim alilipongeza Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) kwa kuendeleza uhifadhi na utalii katika maeneo linayoyasimamia ukiwemo Mlima Kilimanjaro.

"Tumekuja kujionea wenyewe uzuri wa mlima huu wa Kilimanjaro na tumedhamilia kufika kileleni ili tutakaposhuka tukayaambie mataifa tuliyomo fursa gani zipo ili waje kuwekeza na wengine kutalii", aliongeza Mhe. Balozi Maalim.

Naye, Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini - TANAPA, Jenerali Mstaafu George Waitara  aliwashukuru waheshimiwa mabalozi na watalii wengine waliojitokeza katika zoezi la "Twenzetu Kileleni 2023" kwa kuwa wazalendo kupandisha Bendera ya Taifa katika kilele cha Uhuru ili kuadhimisha kumbukumbu ya miaka 62 ya Uhuru wa Tanganyika.

Sambamba na hayo, Jenerali Mst. Waitara alisema kuwa TANAPA itaendelea kusimamia rasilimali zote zinazopatikana katika Hifadhi za Taifa na kuimalisha miundombinu wezeshi ili kurahisisha shughuli za utalii na uhifadhi. 

Akizungumza kwa niaba ya Kaimu Kamishna wa Uhifadhi -TANAPA, Naibu Kamishna wa Uhifadhi na Maendeleo ya Biashara Herman Batiho, alisema kuwa TANAPA itaendeleza shughuli za uhifadhi wa pamoja utakaosaidia kutunza mazingira hasa ya ukanda wa Pwani ili kupunguza kasi ya kupungua kwa barafu ya mlima Kilimanjaro.

Kumekuwepo na utamaduni katika nchi yetu kusherehekea kumbukizi ya siku ya uhuru wa Tanganyika katika kilele cha Mlima Kilimanjaro. Ili kufanikisha tukio hilo adhimu, TANAPA imeruhusu kwa mwaka huu zitumike njia 3 ambazo ni Lemosho, Machame na leo tarehe 05.12.2023 safari ya kukwea jabali hilo refu kuliko yote barani Afrika limefanyika katika lango la Marangu.



No comments: