MWIGULU AZITAKA WIZARA TAASISI ZA UMMA KUZINGATIA WELEDI NA TAALUMA KATIKA UNUNUZI NA UGAVI - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Wednesday 13 December 2023

MWIGULU AZITAKA WIZARA TAASISI ZA UMMA KUZINGATIA WELEDI NA TAALUMA KATIKA UNUNUZI NA UGAVI








Na Mwandishi Wetu,Arusha.

maipacarusha20@gmail.com

WAZIRI wa Fedha na Mipango ameziagiza wizara na taasisi zote za umma nchini kuhakikisha kazi zote zinazohusu manunuzi na ugavi zinafanywa na watumishi wenye weledi ambao wana sifa na uzoefu unaohitajika na si vinginevyo.

Dkt Mwigulu Nchemba ambaye alikuwa mgeni rasmi katika ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa 14 wa Mwaka wa Wataalamu wa Ununuzi na Ugavi unaoendelea Jijini Arusha, katika hotuba yake alisisitiza umuhimu wa sekta hiyo muhimu kusimamiwa na wataalamu wenye uzoefu na waliosajiliwa na bodi husika.

Alisema hatua hiyo itasaidia kuziba mianya ya ubadhirifu wa fedha za umma.

“Hii ni moja kati ya sekta nyeti katika kuboresha uchumi wa taifa kwa sababu inashughulika moja kwa moja na takribani asilimia 70 ya jumla ya bajeti ya mwaka ya nchi” alisisitiza Waziri.

Katika kuhakikisha maagizo hayo yanatekelezwa kwa umakini, Dkt Nchemba amemuagiza Katibu Mkuu wa wizara ya fedha na mipango kukutana na mwenzake wa Ofisi ya Rais (Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa- TAMISEMI) ili kujadili na kuweka mikakati muhimu ya kuhakikisha agizo hilo linatekelezwa kwa wakati katika ofisi zote za umma na wizara zote.

Akitoa taarifa zaidi kuhusu maendeleo ya sekta hiyo, waziri Nchemba alieleza kuwa serikali inafanyia kazi changamoto ya kuwepo kwa wataalamu wachache katika sekta hiyo muhimu.

"Na katika mchakato mzima wa kutoa zabuni za utoaji huduma kwenye taasisi za umma na wizara, ni vyema maafisa wa ununuzi kuwapa kipaumbele watoa huduma wazawa ili kusaidia kukuza uchumi wa uchumi wa nchi na uzalendo" alihimiza.

Alieleza kwamba, kwa mujibu wa kanuni zilizowekwa na serikali, michakato yote ya ununuzi na usambazaji kwa sasa inatakiwa kushughulikiwa kupitia Mfumo wa Kitaifa wa Ununuzi wa Kielektroniki (“NePS”).

"Ninafurahishwa na namna ya kitaalamu ambayo Bodi ya Wataalamu wa Ununuzi na Ugavi (PSPTB) inavyofanya kazi kwa bidii ili kuimarisha weledi wa wataalamu wa ununuzi na ugavi nchini, ikiwa ni pamoja na kuwasaidia kutumia vyema mfumo wa kidijitali wa NePS,"alieleza.

Aidha, Dkt Nchemba amewataka washiriki wa kongamano hilo muhimu linalofanyika katika ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Arusha (AICC) kutumia vyema mkutano huo ili kujadili na kuweka mikakati muhimu kwa mustakabali mzuri wa sekta hiyo.

Mada kuu ya mkutano huo unaojumuisha karibu wajumbe 2000 kutoka ndani na nje ya nchi, ni "Mabadiliko ya Kidijitali kwa Kuboresha Ununuzi na Usimamizi wa Mnyororo wa Ugavi Kuelekea Maendeleo Endelevu"

Katika hotuba yake wakati wa ufunguzi wa Mkutano huo, Mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi ya PSPTB, Jacob Kibona alieleza baadhi ya mafanikio waliyoyapata hadi sasa, pamoja na changamoto zilizopo.

"Tumepiga hatua kubwa katika kazi za jumla ya kufuatilia na kuboresha utendakazi wa sekta kwa kuandaa mafunzo kadhaa kwa wataalamu husika, kuwa kagua, kuwaidhinisha na kuwasajili kulingana na kanuni, ikiwa ni pamoja na miongozo ya ithibati ya mtaala husika," alisemakina.

Na akitoa maelezo kuhusu changamoto zilizopo, Mwenyekiti huyo wa bodi ya wakurugenzi alibainisha kuwa PSPTB inakabiliwa na upungufu wa fedha za kutosha ili kutekeleza majukumu yake ya msingi, ikiwa ni pamoja na kazi ya kuwakagua wataalamu wa ununuzi na ugavi.

Hata hivyo, kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa PSPTB, Bwana Goodfred Mbanyi, alisema lengo lao kuu kwa sasa ni kuhakikisha wataalamu wa ununuzi na ugavi nchini wanapatiwa ujuzi muhimu unaohitajika katika matumizi ya mfumo wa kidijitali.

Mkutano huo umefadhiliwa na makampuni kadhaa, ambayo ni pamoja na Zanzibar Insurance Cooperation (ZIC), Dynatech Solutions, Shades of Green Safaris, Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL), Bravado Solutions, Tanzania Social Action Fund (TASAF), Bisech Tour Company, Nekira Company Ltd, Haier Tanzania, e- Government (e-GA), Tanzania Standard Newspapers (TSN), Soft Tech Consultant na UTT AMIS.

Nyingine ni Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), Shirika la Bima la Taifa (NIC), Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), UCSAF, Tume ya Ushindani wa Haki (FCC), Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), Shirika la Nyumba la Taifa (NHC). ) pamoja na Fidia kwa WafanyakaziMfuko (WCF).





No comments: