![]() |
| Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe Profesa William Mwegoha akifungua kongamano la kimataifa la wajasiriamali jijini Arusha mapema leo |
![]() |
| Mratibu wa mradi huo Dkt. Nsubili Isaga kutoka shule kuu ya biashara ya chuo Kikuu Mzumbe akizungumza na wataalamu wa Biashara Toka vyuo vikuu nchini katika kongamano hilo |
![]() |
| Picha ya pamoja |
Na: Andrea Ngobole, Arusha
maipacarusha20@gmail.com
Chuo Kikuu Mzumbe kwa kushirikiana na Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo nchini (Sido) wametoa mikopo kwa wajasiriamali wadogo 100 kwa njia ya mtandao (C4YET) Kwa udhamini wa Shirika la Kimataifa la Maendeleo Denmark (DANIDA).
Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe, Profesa William Mwegoha akizungumza katika kongamano la kimataifa la wajasiriamali jijini Arusha mapema leo amesema mradi huo umewezesha vijana kuainisha biashara wanayofanya pamoja na namna Bora ya urejeshwaji wa mikopo yenye riba ya asilimia Tano kulingana na mkopo waliyopewa.
Alisema chuo hicho kiliona changamoto wanazopata wajasiriamali wadogo na hususani vijana ambao hawawezi kukopesheka na mabenki kwa urahisi nchini ndipo wakafanya utafiti juu ya changamoto za ajira na hatimaye kuchagiza sekta ya ajira ili vijana wa kitanzania kuchangia shughuli za kiuchumi na ajira kupitia mradi huo.
Mradi huo ulioanza mwaka 2019 umewanufaisha vijana wajasiriamali 187 kwa kupata mafunzo ya jinsi ya kupata mikopo kupitia majukwaa ya uchangiaji ya umati ambayo huwezesha kuchangamkia fursa kupitia njia za mtandao chini ya usimamizi wa Sido.
"Mradi huu ulianza mwaka 2019 na mwakani unatarajia kuisha lakini mafanikio ni makubwa kwa vijana kuweza kukopesheka ikiwemo kujikwamua kiuchumi kupitia Sido " alisema Profesa Mwegoha
Naye Mratibu wa mradi huo, Dkt. Nsubili Isaga kutoka shule kuu ya biashara ya chuo Kikuu Mzumbe amesema mradi huo umesaidia vijana wengi wajasiriamali kukopesheka kwani mabenki mengi nchini hayakopeshi vijana kutokana na ukosefu wa dhamana ambzo ni mali zisizohamishika na hivyo watafiti hao wa chuo kikuu Mzumbe waliamua kutafuta njia ya kuwezesha vijana kukopesheka na kuongeza ajira nchini.
Alisema mradi huo awali ulianza kwa wanataaluma lakini badae ukaenda kwa wajasiriamali kutokana na kubuni nyenzo za uandishi wa andiko lililowavutia wafadhili kwaajili ya washirika kusaidia tafiti na hatimaye chuo hicho kushirikisha Sido kwaajili ya kuwakwamua wajasiriamali vijana kwenye mikoa ya Arusha, Mwanza, Dar es Salama, Morogoro na Mbeya.
Aliongeza kuwa jumla ya wajasiriamali 187 walipewa mafunzo hayo ambapo wajasiriamali 100 kati yao waliweza kupata mikopo yenye riba ya asilimia 5 inayowawezesha kurejesha mikopo yao kwa wakati na baadae vijana wengine watafikiwa zaidi ili wajiunge na majukwaa ya biashara mitandaoni.



No comments:
Post a Comment