WAZIRI KAIRUKI: MAENEO MAALUM YA UWEKEZAJI SWICA KUONGEZA WATALII NA MAPATO - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Wednesday 3 January 2024

WAZIRI KAIRUKI: MAENEO MAALUM YA UWEKEZAJI SWICA KUONGEZA WATALII NA MAPATO




Waziri wa Maliasili na Utalii Angela Kairuki pamoja na katibu Mkuu wa wizara hiyo Dkt. Hassan Abbas wakiwa katika hafla ya utiaji saini

Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii Dkt. Hassan Abbas akidafanua baadhi ya mambo wakati akizungumza katika hafla hiyo.



Mkurugenzi wa Kampuni ya Uwindaji ya Bushman Safari Trackers Ltd, Talal Abood akitoa shukurani zake kwa serikali kwa kampuni yake kusaini mkataba huo na wizara ya Maliasili akisema hiyo inafungua milango kwa wafanyabiashara kuwekeza katika sekta ya Utalii. 



Na Mwandishi wetu, MAIPAC

maipacarusha20@gmail.com

Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Angellah Kairuki (Mb) amesema utekelezaji wa mikataba sita ya uwekezaji katika Maeneo Maalum ya Uwekezaji wa Wanyamapori (Special Wildife Investment Concession Areas – SWICA) utaongeza utalii na mapato katika maeneo yatakayofanyiwa uwekezaji huo, hali itakayochangia kwa kiasi kikubwa kutekeleza lengo la kuongeza idadi ya watalii kutoka milioni 1.5 mwaka 2021/2022 hadi milioni 5 mwaka 2025/2026.

Hayo yameelezwa na Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt. Angella Kairuki jijini Dar es Salaam wakati akizungumza katika hafla utiani saini mikataba hiyo yenye thamani ya dola za Kimarekani milioni 278, sawa na shilingi za kitanzania Bilioni 696 kati ya Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) na kampuni hizo kwa kwa ajili ya kuendeleza miundombinu ya utalii katika maeneo sita ya uwekezaji.

Maeneo hayo ya uwekezaji yametajwa kuwa ni Pori la Akiba Mkungunero Mkoani Dodoma, Mapori ya Akiba ya Ikorongo na Grumet Mkoani Mara pamoja na Mapori ya Akiba ya Maswa Kimali, Maswa Mbono na Maswa Kaskazini yaliyopo Mkoani Simiyu.

Hafla ya utiaji saini imefanyika leo Januari 3, 2024 katika ukumbi wa Chuo cha Taifa cha Utalii jijini Dar es Salaam.

“Uwekezaji huu utaiingizia Serikali mapato yanayokadiriwa kufikia dola za Kimarekani milioni 314 katika kipindi cha miaka 20 ya uwekezaji sawa na dola milioni 16 kwa mwaka (sawa na shilingi za kitanzania bilioni 40). Mafanikio haya yanatokana kwa kiasi kikubwa na utangazaji utalii kupitia Filamu ya “Tanzania- The Royal Tour” iliyoandaliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan” amesisitiza Mhe. Kairuki.

Ameongeza kuwa miongoni mwa manufaa mengine yatakayopatikana kutokana na uwekezaji huo ni kuimarika kwa uhifadhi, utafiti na kuboresha maisha ya jamii zinazozunguka maeneo ya uwekezaji ambapo takribani dola za Kimarekani milioni 50, sawa na shilingi za kitanzania bilioni 125, zitatumika kufadhili Miradi ya Maendeleo ya Jamii katika kipindi cha miaka 20 ya uwekezaji.

Aidha, amezipongeza kampuni za Bushman Safari Trackers Ltd, Grumeti Reserves Ltd, Mwiba Holdings Ltd na Magellan General Trading LLC kwa kufanikiwa kusaini mikataba ya uwekezaji mahiri.
Naye, Mkurugenzi wa Kampuni ya Uwindaji ya Bushman Safari Trackers Ltd, Talal Abood amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa juhudi zake binafsi za kukuza utalii na kushirikisha sekta binafsi kwa lengo la kukuza uchumi wa Tanzania.

“Tunaishukuru Wizara ya Maliasili na Utalii kwa ushirikiano na tunaahidi kwamba tunaenda kutekeleza hili jambo kwa ufanisi mkubwa na uharaka mkubwa ili kuendana na kasi ya Serikali ya Awamu ya Sita kwenye kutekeleza Sera ya Utalii” amesema Bw. Talal.



Hafla hiyo imehudhuriwa na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Dunstan Kitandula (Mb), Katibu Mkuu, Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Hassan Abbasi, Mwenyekiti wa Bodi ya TAWA, Meja Jenerali Mstaafu Hamis Semfuko, Makamishna wa Uhifadhi kutoka Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), Wakala ya Huduma za Misitu Tanzania (TFS) na Mamlaka ya Uhifadhi ya Eneo la Ngorongoro (NCAA), baadhi ya watendaji na maafisa kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii na TAWA pamoja na wadau mbalimbali wa uhifadhi.

No comments: