KAMATI YA BUNGE YARIDHISHWA NA UZALISHAJI SUKARI KIWANDA CHA MKULAZI - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Monday 5 February 2024

KAMATI YA BUNGE YARIDHISHWA NA UZALISHAJI SUKARI KIWANDA CHA MKULAZI

 


Kamati Waipongeza Serikali kwa Uwekezaji wa kiwanda cha sukari mkulazi




Na Lilian Kasenene, Morogoro


maipacarusha20@gmail.com


Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii imeridhishwa na hatua iliyofikiwa katika uwekezaji wa kiwanda cha uzalishaji sukari cha Mkulazi kilichopo wilayani Kilosa mkoani Morogoro na kuanza kuzalisha sukari hiyo nchini.


Wajumbe wa Kamati hiyo,pamoja na kuridhishwa na uwekezaji walipongeza serikali kwa usimamizi,kamati hiyo imefanya ziara katika kiwanda cha kuzalisha sukari cha Mkulazi kinachomilikiwa kwa ubia baina ya Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii(NSSF) na Jeshi la Magereza, Mkoa wa Morogoro.


Mwenyekiti wa Kamati hiyo Fatuma Toufiq akizungumza katika ziara hiyo amesema kuwa, wameridhishwa na uzalishaji wa kiwanda hicho na kuhimiza uzalishaji huo ufanyike kwa wingi ili kupunguza tatizo la upungufu wa sukari nchini ambalo kwa sasa serikali limeagiza tani laki moja ya sukari ili wananchi waweze kupata nafuu ya ununuzi kwa bei elekezi iliyowekwa.


Toufiq amesema Kiwanda hicho cha Kimkakati kitaenda kupunguza nakisi ya sukari iliyopo ya tani 250,000 kwa kuchangia asilimia 20 ambapo mkakati wa kiwanda hicho ni kuzalisha sukari tani 50,000 kwa ajili ya matumizi ya sukari za viwandani na matumizi ya majumbani.                                                                                              “Mradi huu ni wa kimkakati, na ni mkakati mkubwa, kwa sababu mwisho wa siku utasaidia kupunguza upungufu wa sukari hapa Nchini, Tumeona miundombinu, Tumeona sukari ambayo imeanza kuzalishwa, lakini pamoja na changamoto ya mvua za Elnino lakini tunaona kabisa kwamba huko mbele kuna mwanga kwa Watanzania amesema mwenyekiti Toufiq.


Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Patrobas Katambi amesema Serikali ina dhamira ya kuhakikisha nchi inaondokana na upungufu wa sukari, na kwamba pamoja na kiwanda hicho kuwa na uwezo wa kuzalisha tani hizo 50,000 kwa mwaka, uboreshaji utaofanyika utawezesha kiwanda hicho kuzalisha zaidi ya tani elfu 75,000.


Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Kampuni hodhi ya Mkulazi, Dk Hildelitha Msita amewahakikishia wajumbe wa kamati hiyo kuwa wamejipanga kutekeleza maagizo yote yaliyotolewa na kamati hiyo ili kuboresha mradi huo.


Mkurugenzi mkuu wa NSSF Masha Mshomba amesema pamoja na NSSF kuwa wabia wa mradi huo kwa asilimia 96  imepata faraja kuona uwekezaji huo kufikia hatua ya kuanza uzalishaji, kwani lengo la mradi ni kuona unaanza kuleta faida ili kurudisha fedha za wanachama wa mfuko huo.


“Niwaahidi Watanzania wote hususani wanachama wa NSSF, kwamba fedha zao zipo salama, mradi huu utalipa kwa kadiri tulivyokusudua, lakini kikubwa zaidi utasaidia kupunguza nakisi ya sukari hapa Nchini, Ndio maana tunahimizwa tujenge utaratibu wa kuwekeza katika viwanda kama hivi,”amesema Mshomba.


Aidha Mkurugenzi huyo ameahidi kusimamia vyema mradi huo ili uweze kuleta tija na kurudisha fedha za wanachama.


Naye Mtendaji Mkuu wa Kampuni hodhi ya Mkulazi Selestine Some amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk Samia Suluhu Hassan kwa kutoa miongozo ya uwekezaji wa mradi huo uliogharimu shilingi bilioni 344 ambapo umeanza kutoa matunda kwa Watanzania.


“Mradi unafaida kwa jamii, mradi umejenga Zahanati inayoweza kuzihudimia jamii zinazozunguka mradi huo, lakini pia ukipita maeneo ya Dumila utaona shughuli za kiuchumi zikiendelea na kutoa fursa za vijana kujiajiri kutokana na uwepo wa mradi huu,”amesema Some


Sambamba na uwekezaji huo wenye faida za kiuchumi kwa Watanzania, Kampuni hodhi ya Mkulazi imeweza kuzingatia usalama wa Wafanyakazi wake mahala pa kazi kwa kuwapatia vifaa kinga vya kuzuia ajali (PPE) wafanyakazi wake, ambapo Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira, Vijana na Watu wenye Ulemavu Patrobas Katambi alitoa cheti kwa Mtendaji Mkuu wa Kampuni hiyo kwa kujali usalama wa wafanyakazi mahala pa Kazi.




No comments: