KOMPYUTA 11 ZAKABIDHIWA KWA HALMASHAURI SABA MOROGORO ILI KUBORESHA HUDUMA ZA UKIMWI - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Thursday 15 February 2024

KOMPYUTA 11 ZAKABIDHIWA KWA HALMASHAURI SABA MOROGORO ILI KUBORESHA HUDUMA ZA UKIMWI

 




Na Lilian Kasenene, Morogoro


maipacarusha20@gmail.com


Katibu Tawala Mkoa wa Morogoro Dk Mussa Ali Mussa amekabidhi kompyuta 11 pamoja na Vichapishi (printer) kwa Halmashauri 7 za Mkoa huo zikiwa na lengo la kukusanya, kuhifadhi taarifa na kuboresha huduma za UKIMWI katika vituo vya Matunzo na Tiba ya UKIMWI kwenye Halmashauri hizo.


Akizungumza wakati wa kukabidhi kompyuta hizo kwenye Ofisi ya Mkuu wa Mkoa huo, Dk Mussa amesema, kompyuta hizo zimenunuliwa na fedha zilizochangwa na wadau mbalimbali wakati wa sherehe za Maadhimisho ya Siku ya UKIMWI Duniani ambayo Kitaifa zilifanyika Mkoani Morogoro Disemba Mosi, 2023.


Amebainisha kuwa jumla ya fedha zilizokusanywa kwenye maandalizi ya sherehe hizo ni sh 50,000,000 millioni na baada ya matumizi kwenye sherehe hizo, fedha zilizobaki zimeelekezwa kununua vifaa hivyo ambavyo ni Kompyuta na vichapishi kwa lengo lilelile la kuboresha huduma za masuala ya UKIMWI.  


Katika hatua nyingine Dk Mussa amewataka Waratibu wa UKIMWI wa Halmashauri saba zilizokabidhiwa kompyuta hizo kutumia vifaa hivyo kwa malengo yaliyokusudiwa ili kuhamasisha wadau kuendelea kuwa na moyo wa kuchangia.


“Mkazitunze sasa ili zitumike kwa muda mrefu na kuleta manufaa yale yanayotakiwa,” amesema Dk Mussa.


Naye Mratibu wa Kudhibiti UKIMWI, Magonjwa ya Ngono na Homa ya ini (RASHCo) Mkoa wa Morogoro Dk Neema Mtambo amesema kompyuta hizo zitagawanywa katika vituo 11 vya Matunzo na Tiba ya UKIMWI kwenye Halmashauri saba, lengo likiwa ni kuboresha huduma na takwimu za UKIMWI. 


Aidha Dk Neema ameishukuru Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Dk Samia Suluhu Hassan kwa kujali na kuboresha Sekta Afya huku akiwashukuru wadau waliochangia fedha hizo na kuahidi kuwa atasimamia ili kuhakikisha vifaa hivyo vinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa.


Kwa upande wake Mratibu wa Kudhibiti UKIMWI, Magonjwa ya Ngono na Homa ya Ini kutoka Halmashauri ya Mvomero  Dk Grace Emil kwa niaba ya Waratibu wa UKIMWI wa Wilaya amesema vifaa hivyo vitasaidia wananchi kutosafiri umbali mrefu kufuata huduma za UKIMWI na kupata takwimu sahihi na kurahisisha kazi katika Halmashauri hizo.


Halmashauri zilizopata kompyuta na Vichapishi hivyo ni Pamoja na Halmashauri ya Malinyi, Mlimba, Morogoro DC, Ulanga, Mvomero, Gairo na halmashauri ya Kilosa.



No comments: