Baadhi ya waandishi wa Habari Mkoa wa Morogoro wakimsikikiza Mkuu wa Takukuru mkoa wa Morogoro, Manyama Tungaraza |
Na Lilian Kasenene,Morogoro
maipacarusha20@gmail.com
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Morogoro imemtia mbaroni mwenyekiti wa Kamati ya shule Suleiman Mwishehe na wenzake na kumfikisha mahakamani kwa tuhuma za kujaribu kumhonga Ofisa wa Taasisi hiyo.
Ofisa huyo alikuwa anachunguza tuhuma dhidi ya ubadhilifu wa Sh milioni 90 zilizotolewa kwa ajili ya ujenzi.
Fedha hizo ziliidhinishwa kwa ajili ya ujenzi wa nyumba ya walimu na vyumba vya madarasa ya shule ya msingi Mlilingwa, kijiji cha Mlilingwa Kata ya Tununguo, wilaya ya Morogoro.
Mkuu wa Takukuru mkoa huo, Manyama Tungaraza amesema hayo jana mjini Morogoro katika taarifa ya kipindi cha Oktoba hadi Desemba 2023 cha utekelezaji wa majukumu mbalimbali ya Taasisi hiyo yakiwemo ya ufuatiliaji wa utekelezaji miradi ya maendeleo inayohusu Elimu ,Maji na Mifugo.
Mwishehe ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ujenzi na Mlezi wa Kikundi cha Bosu Kuku Group, alikamatwa baada ya kumpa Ofisa wa Takukuru kiasi cha Sh milioni 3 kati ya milioni 5 alizoshawishi awali kuwa yeye (Mwishehe ) na watuhumiwa wenzake watampa ili wasifikishwe Mahakamani .
Tungaraza amesema mtuhumiwa huyo alipofikishwa Mahakamani alikiri kosa na kutiwa hatiani na kuhukumiwa kifungo cha miaka miwili jela au kulipa faini ya Sh 500,000 na fedha alizozitoa kama hongo kutaifishwa na kuwa mali ya Serikali.
Mkuu huyo wa Takukuru mkoa amesema mshitakiwa alilipa faini ya Sh 500,000 na kiasi cha Sh milioni tatu zilmetaifishwa kuwa za serikali.
Hivyo alitoa onyo kwa Mwananchi yoyote asijaribu kushawishi au kutoa hongo kwa mtumishi wa Takukuru mahali popote mkoani humo kwa lengo la kuharibu uchunguzi au ushahidi wa tuhuma zozote zinazochunguzwa na Takukuru kwani hatua kali za kisheria zitachukuliwa.
Tungaraza ameelezea mazingira ya kukamatwa kwa Mwishehe kuwa, baada ya kuidhinishiwa kwa mradi huo na thamani ya Sh milioni 90 ambazo zilipitia kwake alikaa nazo muda mrefu bila kuanza kuifanya kazi hiyo.
Mkuu wa Takukuru mkoa amesema baada ya kuitwa kwa ajili ya mahojiano na kuhojiwa alioana hiyo sio sawa na ya kwamba ataweza kufikishwa Mahakamani
“Alipogundua alianza kushawishi kuwa atatoa sh milioni 5 ili suala hilo lisiende Mahakamani na taarifa zake kupatikana, tukamwambia Ofisa wetu amwambie alete hizo fedha naye bila ajizi alizileta fedha hizo hapa Ofisi kwetu Takukuru mkoa na akakamatwa hapa kwetu na fedha zake Sh milioni 3,“ amesema Tungaraza .
Tungaraza amesema licha ya suala hilo kumalizika Mahakamani na kukamilika kwa majengo hayo , bado Takukuru inaendelea na uchunguzi wa tuhuma nyingine za kubaini ubora wa majengo yaliyojengwa.
No comments:
Post a Comment