MAKAMU wa Rais Dkt.Philip Mpango |
Na Lilian Kasenene,Same
maipacarusha20@gmail.com
MAKAMU wa Rais Dkt. Philip Mpango ameziagiza Halmashauri zote nchini kuhakikisha wanaendelea kuhifadhi maeneo mapya ya hifadhi za misitu pamoja na kuongeza mashamba ya miti.
Pia amewataka wakala wa huduma za Misitu nchini TFS kuhakikisha kila Halmashauri inakuwa na vitalu vya miti kuanzia ngazi za vijiji hadi kata ambapo Halmashauri za miji zitengeneza bustani za kijani kwaajili ya kupumzikia na mazoezi.
Makamu wa Rais huyo alisema hayo wilayani Same mkoani Kilimanjaro wakati wa maadhimisho ya siku ya misitu duniani na siku ya upandaji miti kitaifa yaliofanyika wilayani humo yenye kauli mbiu 'Misitu na Ubunifu'.
" Vijiji vyote nchini vihakikishe vinatunza na kulinda miti yote ya asili iliopo katika maeneo yao"alisisitiza.
Aidha Dk Mpango ameiagiza Taasisi ya Utafiti wa Misitu Tanzania Tafori kufanya utafiti wa miti dawa kwenye wilaya zote nchini, kuchukua mbegu zake na kuzipanda sambamba na kuelezea aina ya dawa yake.
"Nendeni kwenye kila wilaya kuuliza watu miti dawa iliyopo kwenye maeneo yao nia ni kuendeleza na kutambua tiba asili,"alisema.
Alisema kufanya hivyo kutasaidia miaka ya badae kuweza kuelezea vizazi vijavyo na kuhamasisha kufanya utafiti zaidi wa miti hiyo dawa.
Pia aliitaka Tafori licha ya kutengeneza mbegu za miti mbadala ya asili kama Mvule na Mkongo kuhakikisha wanatengeneza pia mbegu nyingi za miti ya asili hiyo na kuzipanda ili zisipotee.
Kwa upande wa Wakala wa huduma za misitu Tanzania TFS aliwaagiza kutafuta suluhisho la matumizi ya mkaa na kuni sambamba na kuhamasisha wananchi waweze kutumia nishati safi na mbadala kwa asilimia 90 hadi 100.
Aliagiza kila mkoa kuhakikisha wanafanya zoezi la kuhamasisha matumizi ya nishati safi ili kuondokana na matumizi ya nishati chafu kama kuni na mkaa.
Vile vile aliagiza kuharakishwa kwa mwongozo wa kudhibiti matumizi ya msumeno mnyororo maarufu kama Chensoo ili kudhibiti uharibifu wa miti.
"Matumizi ya chenso yanasababisha Taifa zima kupata shida, watu wachache wananunua chensoo na kuingia msituni kukata miti, muda mfupi msitu wote unateketea" alisema.
Wakati huo huo ameagiza wizara ya Maliasili na Utalii kupitia upya sheria miongozo ya fidia kwa watu wanaopatwa na madhara ya kufariki kwa kuuliwa na wanyama ili iendane na hali halisi.
"Hatuwezi kufananisha thamani ya mtu anapokufa na malipo ya fedha lakini walao kifuta machozi kiwe cha maana. " alisema.
Wakati huo huo makamu huyo wa Rais ametaka hatua za haraka zichukuliwe kusafisha ziwa Jipe ambalo limeathiriwa na ongezeko la magugu maji pamoja na tope kutokana na shughuli za kibidadamu.
Katika hatua nyingine alimwagiza waziri wa Kilimo , idara ya kilimo mkoani humo pamoja na taasisi za utafiti kubuni mazao mbadala ya kibiashara yatakayofaa kulimwa katika kata za Tae, Saweni na Kilangale ambazo kwa sasa wanalima milungi na bange ili kuachana na zao hilo.
Alisema zao hilo sio zuri na kuwataka wananchi hao kuacha mara moja na badala yake walime mazao mengine ya biashara yatakayowapatia kipato tofauti na zao hilo.
Awali Waziri wa Maliasili na Utalii Angella Kairuki akielezea changamoto za uharibufu wa mazingira alisema Hekta 469 ,000 zinaharibiwa kila mwaka kutokana nacshughuli za kibinadamu.
"Ili kukabiliana na changamoto hiyo tunapaswa kuchukua hatua madhubuti ya kupanda miti na kuilinda"alisema.
Mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro Nuldin Babu alisema mkoa mpaka Sasa umefanikiwa kupanda miti milioni 8.7 ambapo alitoa Rai kwa wananchi wa mkoa huo kushirikiana katika katika harakati za utunzaji wa mazingira na upandaji wa miti ambapo aliwataka kuacha kukata miti ovyo.
No comments:
Post a Comment