Mbunge wa Simanjiro Christopher Ole sendeka |
Na: MWANDISHI WETU,BABATI
maipacarusha20@gmail.com
MBUNGE wa Jimbo la Simanjiro mkoani Manyara, Christopher Ole Sendeka amesema kupandishwa hadhi kwa mapori ya akiba katika Wilaya za wafugaji itakuwa kikwazo kwao hivyo serikali iangalie hilo kwa jicho la tatu ili kukomesha uanzishaji.
Ole Sendeka akizungumza mjini Babati amesema wafugaji wameshikwa na hofu na taharuki kwa kuondolewa walipozaliwa pindi mapori hayo ya akiba yakianzishwa.
Amesema wafugaji wa maeneo husika wameshikwa na hofu na taharuki kutokana na kuanzishwa kwa mapori hayo ya akiba kwani sehemu yao kubwa ya malisho itachukuliwa.
“Tumeona baadhi ya maandiko yaliyopo kwenye mitandao ya kijamii kuwa baadhi ya maeneo ya wafugaji yanapandishwa hadhi kuwa mapori ya akiba hivyo kukosa malisho jambo ambalo siyo jema” amesema Ole Sendeka.
Amesema kwa mujibu wa andiko hilo, maeneo mengi ya wafugaji yaliyotengwa kwa ajili ya malisho ya mifugo yanatarajiwa kuwa mapori tengefu.
Amesema maeneo ya wafugaji ya Simanjiro, Same mkoani Kilimanjaro na wilaya za Longido na Monduli mkoani Arusha, yameandaliwa kuwa mapori tengefu.
“Pamoja na hayo suala ambalo linatusikitisha ni kuwa andiko hilo linabainisha kuwa viongozi na wakazi wa maeneo husika wameshirikishwa jambo ambalo tunaamini siyo kweli,” amesema Ole Sendeka.
Amesema siyo kweli kuwa wawekezaji, makampuni ya uwindaji wa utalii na wawakilishi wa mashamba makubwa ya kilimo na ufugaji wameshirikishwa katika uanzishaji wa mapori hayo ya akiba.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CCM wa Mkoa wa Manyara, Peter Toima amemuunga mkono Ole Sendeka katika kupinga uanzishaji wa mapori hayo ya akiba ambayo ni kikwazo kwa wafugaji.
Toima amesema maeneo ya malisho ya wafugaji ambayo yalitengwa tangu awali yatakapofanywa kuwa mapori ya akiba itakuwa siyo sahihi hivyo serikali iangalie hilo.
Hata hivyo, mkuu wa mkoa wa Manyara, Queen Sendiga amesema suala hilo ndiyo kwanza analisikia kwani halijawahi kufika mezani kwake na akalitolea maelezo yoyote.
“Hata wakuu wangu wa wilaya na kamati yangu ya usalama ya mkoa hawajawahi kuzungumza juu ya hilo ila tutalifuatilia mwanzo wake na baadaye tutalizungumzia,” amesema Sendiga.
No comments:
Post a Comment