DK BITEKO - WATANZANIA HAKIKISHENI TUMUENZI SOKOINE KWA KUFANYA KAZI KWA KUJITUMA - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Monday 8 April 2024

DK BITEKO - WATANZANIA HAKIKISHENI TUMUENZI SOKOINE KWA KUFANYA KAZI KWA KUJITUMA



Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko akizungumza katika mdahalowa Kitaifa wa Kumbukizi ya Miaka 40 ya Hayati Edward Moringe Sokoine iliyofanyika Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), mkoani Morogoro


Na:  Lilian Kasenene, Morogoro

 

maipacarusha20@gmail.com


Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko amesema Watanzania wanapaswa kumuenzi Hayati Edward Moringe Sokoine kwa kufanya kazi kwa bidii ili kuinua uchumi wa nchi na kuboresha maisha yao.


Dk Biteko alisema hayo mkoani Morogoro alipomwakilisha Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi,Dk Hussein Ali Hassan Mwinyi wakati wa kufungua Mdahalo wa Kitaifa wa Kumbukizi ya Miaka 40 ya Hayati Edward Moringe Sokoine iliyofanyika Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), mkoani Morogoro.


Dk Biteko alisema Hayati Sokoine atakumbukwa daima kama kiongozi aliyepigania maendeleo ya taifa kwa moyo wake wote na katika uongozi wake kwa nyadhifa zote alitilia mkazo wananchi kwanza kuwa ndio msingi wa maendeleo.


“Mze wetu hayati Sokoine alifanya kazi kubwa katika shughuli mbalimbali za maendeleo ya taifa na aliweka misingi imara iliyoendeleza muongozo wa kila kiongozi wa Tanzania awe wa namna gani,” alisema Dk Biteko


Aidha alisema Hayati Sokoine aliwataka Viongozi wa Serikali na wananchi kueleza wamezipata wapi mali kwa namna gani kwa hiyo watu wengi waliopata mali kwa njia haramu walimuogopa Sokoine walidiriki kutupa fedha na mali nyingine kwa kuhofia kuhojiwa.


Dk Biteko akizungumzia sekta ya Kilimo, alisisitiza Sekta ya Kilimo iwe kimbilio katika kuinua na kuboresha maisha ya wananchi, na kuondokana na fikra za zamani kuwa Kilimo ni cha watu wa Hali ya chini..


Alisema sekta hiyo ina mchango mkubwa katika kuleta maendeleo ya Taifa na mtu mmoja mmoja kwa kuwa imeajiri watanzania wengi hususan vijana na kukipongeza chuo cha SUA kwa mchango wake mkubwa katika maendeleo ya Sekta ya Kilimo nchini.


Naye, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda alisema Hayati Sokoine amefanya kazi kubwa katika maendeleo ya Sekta ya Kilimo na kuongeza kuwa Wizara ya elimu inafanya kazi kubwa kuhakikisha sekta hiyo inakuwa na mchango mkubwa kwa wananchi hususani vijana.


Makamu Mkuu wa Chuo cha SUA, Prof.Raphael Chibunda alisema kuwa, Edward Moringe Sokoine alikuwa kiongozi wa kipekee hasa katika suala la kutoa maamuzi, uzalendo, uchapa kazi, uadilifu na uaminifu.


“Kwa mfano, alifanya kazi bila kuchoka usiku na mchana, pia alisimamia sera za nchi kwa bidii na kwa weledi. Alichukia na alipiga vita ruswa na kuhakikisha nchi inapiga hatua katika maendeleo kiuchumi na kijamii,” alisema Prof.Chibunda.


Mdahalo wa kumbukizi ya miaka 40 ya kifo cha Sokoine umejadili mambo yanayohusu uongozi na mambo ambayo taifa la Tanzania limerithi kutoka kwa Sokoine ikiwemo Sokoine na Uongozi iliyowasilishwa na Anna Makinda, Spika mstaafu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.


Pia, Profesa mstaafu wa Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam Prof. Issa Shivji akiwasilisha mada juu ya Uongozi na Maendeleo, huku mada ya Kilimo na Maendeleo iliyowasilishwa na Jaji Mstaafu Joseph Sinde Warioba ambaye pia ni Mkuu wa Chuo Kikuu cha SUA na Sokoine na Maendeleo ya kilimo iliyowasilishwa na Prof. Kalunde Sibuga ambaye ni nguli wa kilimo wa chuo cha SUA.      


Hayati Sokoine alikuwa mstari wa mbele kukemea rushwa na ufisadi atakumbukwa kama kiongozi aliyepigania maendeleo ya taifa.


Naibu Waziri Mkuu huyo Dk Biteko asisitiza pia Sekta ya Kilimo iwe kimbilio na vijana waelimishwe vya kutosha na kumjua Hayati Sokoine.


Akizungumza kwa niaba ya familia ya hayati Edward Sokoine, Bi Catherine Sokoine alisema Rais Dk Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika kumbukizi ya miaka 40 ya Hayati Edward Moringe Sokoine itakayofanyika kijiji kwake.


Kauli mbiu ya kumbukizi hiyo ni 'Urithi wa Taifa katika Uongozi wake, Bidii, Uadilifu na, Uaminifu'.


No comments: