MVUA ZINAZONYESHA IFAKARA,MLIMBA ZAKATISHA BARABARA WANANCHI WAKWAMA - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Tuesday 9 April 2024

MVUA ZINAZONYESHA IFAKARA,MLIMBA ZAKATISHA BARABARA WANANCHI WAKWAMA




Na: Lilian Kasenene, Morogoro 


maipacarusha20@gmail.com


MAWASILIANO  ya barabara kati ya Ifakara, Mng’eta na Mlimba Wilaya ya Kilombero mkoani Morogoro yamekatika baada ya mvua zinazoendelea kunyesha kuharibu miundombinu hiyo ya barabara na kuleta adha kwa wananchi wanaotumia njia hiyo kwa usafiri.

Kutokana na barabara hiyo kukatika  
Wakala wa Barabara (TANROADS) mkoa wa Morogoro imeahidi kufungua njia katika kipindi cha siku mbili kuanzia Sasa ili iweze kupitika na mafundi wakiendelea na kazi ya kuimarisha barabara hiyo.

Wakieleza adha wanayoipata wananchi hao wa Mji wa Mng’eta walisema wanapata adha ya usafiri wa kutoka katika miji hiyo kwa kutozwa fedha nyingi tofauti na awali baada ya mvua kuharibu miundombinu ya barabara huku magari yakikwama njiani kwa zaidi ya siku mbili hadi wiki kutokana na baadhi ya maeneo mengine kukatika.

Mkazi wa Wilaya ya Kibiti mkoani  Pwani, aliyekuwa ameenda kumjulia Hali mtoto wake shule, Everiline Kikwesha alisema amelazimika kutumia shilingi 90,000 kutoka Ifakara kwenda Mlimba baada ya mawasiliano ya barabara kukatika kati ya Ifakara na Mlimba.

“Usafiri Ifakara kwenda Mlimba ni wa shida sana na nimelazimika kutumia fedha nyingi nje ya bajeti yangu tofauti na nilivyopanga.” alisema Everline.

Msafiri huyo alisema ametozwa shilingi 15,000 kutoka Ifakara kwenda Mng’eta badala ya kulipa shilingi 8,000 au shilingi 10,000 ambapo ameishia Mng’eta.

Aliongeza kuwa alilazimika kupanda usafiri wa bodaboda hadi Mlimba kwa nyingine ya gharama ya shilingi 30,000 kutokana na kipande cha Mng’eta hadi Mlimba maji kusomba makaravati na magari kushindwa kupita na kufanya gharama za usafiri kuwa kubwa.

“ Kipande hiki ni korofi zaidi kwani hata pikipiki imelazimika ivushwe katika mto ndio tukaendelea na safari.”alisema.

Kwa upande wake dereva wa gari za abiria Ifakara hadi Mlimba, Timotheo Ndopwe alisema kwa sasa wenye magari ya abiria wamesitisha kutoa huduma ya kwenda Mlimba na baadhi yakiishia Mng’eta kutokana na barabara kipande cha Mng’eta hadi Mlimba kukatika.

“Kuna maeneo ya Kisata, Makutano na Ikule huwezi kupitisha gari ndio maana abiria wanaotoka Ifakara kwenda Mlimba lazima aishie Mng’eta na ili kuendelea na safari itampasa apande pikipiki (Bodaboda) kwa sababu maji yameharibu barabara zaidi kipande cha Mng’eta kwenda Mlimba lakini hata kipande cha Ifakara hadi Mng’eta sio kizuri sana magari yamekuwa yakikwama na kunasuliwa kwa kuvutwa na matrekta.”amesema Timotheo.

Timotheo alisema kipindi hiki nauli ya kutoka Ifakara kwenda Mng’eta ni shilingi 15,000 tofauti na kiangazi kuwa shilingi 8,000 hadi shilingi 10,000 na Mlimba hadi Ifakara ni shilingi 15,000.

Meneja wa TANROADS mkoa wa Morogoro Alinanuswe Kyamba alisema kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha nchini zimeleta athari kwa kuharibu miundombinu ya barabara na kazi walionayo kama Wakala wa barabara ni kuhakikisha wanarejesha mawasiliano kipande kimoja baada ya kipindi.

Kyamba alisema timu ya wahandishi kutoka kwa Wakala huyo wameweka kambi wilaya ya Kilombero kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha kuharibu maeneo mengi ya barabara katika mkoa huo.

“Tupo hapa Mchombe (Mng’eta) na wahandishi kusimamia seti nne za mitambo kuanzia eneo la Londo, Mchombe, Chita na Kihansi ili kurekebisha maeneo yote korofi na matarajio yetu njia ipitike ndani ya siku mbili kwa lengo la kufungua njia.”amesema Mhandisi Kyamba.

Mkandarasi wa barabara kipande cha Mng’eta hadi Chita, Mhandishi Lazaro Malya alisema wao wamejipanga kurekebisha kufanya kazi kwa uharaka ili kuondoa adha wanayopata wananchi katika barabara hiyo.

“Tupo eneo la tukio mitambo tayari imefika na kazi iliyopo mbele yetu ni kuhakikisha tunarekebisha maeneo yote korofi ili huduma za usafiri kati ya Ifakara, Mng’eta, Chita na Mlimba zinarejea kwa kipindi kifupi baada ya mvua iliyonyesha wiki hii kuharibu miundombinu ya barabara na magari kushindwa kupitika hada kipande cha kutoka Mng’eta kwenda Mlimba.amesema Mhandisi Malya.

Kutokana na kukatika kwa barabara hiyo madareva wa malori wanaosafiri mchele wa mpunga wanalazimika kubeba viroba walivyojaza pumba kama njia ya kuchukua tahadhari pale wanapokwama kumimina chini ili kunasua gari eneo husika.


No comments: