Baadhi ya wakina Mama wanaojihusisha na uchekechaji wa mchanga wa madini mji wa Mererani |
Baadhi ya wakina Mama wanaojihusisha na uchekechaji wa mchanga wa madini ya Tanzanite mji wa Mererani wakitoa kero wanazokumbana nazo baada ya kufungwa Kwa baadhi ya migodi ya wachimbaji wadogo |
Na: Mwandishi wetu, Mererani
maipacarusha20@gmail.com
Wanawake ambao wanafanya kazi ya kuchekecha michanga katika Machimbo ya Tanzanite Mererani na ambao wanafanya biashara za Madini juzi wameandamana kumuomba Rais Samia Suluhu kuingilia kati mgogoro wa kufungwa baadhi ya migodi ya wachimbaji wadogo.
Wanawake hao wameeleza kufungwa kwa njia za migodi hiyo, ikiwepo mgodi wa Saniniu Laizer ambao hadi sasa unashikilia rekodi ya kutoa Madini makubwa lakini pia kulipa kodi kubwa kwa serikali umewasababishia umasikini na kushindwa kumudu familia zao.
Sambamba na njia ya mgodi huo, pia migodi mingine ya wachimbaji wadogo imefungwa na baadhi kulazimishwa kuingia ubia na Franone ili waweze kuendelea kuchimba Madini.
Helena Daud mchekechaji wa madini anasema kufungwa Kwa migodi ya wachimbaji wadogo kumepelekea kuwa na hali ngumu zaidi kwao kwani Kwa Sasa wanapata udongo Kwa shida wanaweza kushinda kutwa wanachekecha na wasipate chochote Cha kurudi nacho nyumbani Hali inayofanya maisha kuwa magumu kila kukicha.
Naye Ummy Rajabu Chandu mchekechaji wa madini anaungana mwenzake Kwa kusema kuwa kufungwa Kwa migodi wa wachimbaji wadogo kumeathiri uchumi na ajira za akina mama wa mji wa Mererani.
Akizungumzia athari hizo mfanyabiashara wa Madini Mererani Herieth Evarist Mushi anasema wameshindwa kuwapeleka watoto shule baada ya mji wa Mererani kufa kwani watu hawana ajira na wamekosa madini kutokana na Madini yote kuhodhiwa na Kampuni ya Franone ambayo imekodishiwa eneo la Kitalu C.
Alisema kwa kupeleka shughuli zote za uuzaji wa madini ndani ya Ukuta Mererani umbali wa kilomita 9 ambapo gharama za usafiri kwenda na kurudi ni shilingi 6000 Kwa pikipiki Kila siku kumeongeza ugumu wa maisha yao.
Lightness Daniel ,Mkazi wa Mererani anasema kuchukuliwa njia za madini Kwa wachimbaji wadogo kutapelekea kukosekana kwa ajira Kwa watu wengi kwani migodi ya wachimbaji wadogo ambayo imefungwa ndio hutoa fursa ya ajira nyingi kwa vijana na kuwapa udongo wanawake.
Amesema udongo ambao walikuwa wakipata ndio huchekecha na kujipatia madini ambayo huyauza na kujipatia kipato Cha kuendesha maisha yao.
Wanawake hao wanamuomba RAIS Samia kuingilia kati Mgogoro huo kwani Wizara imeshindwa kutoa Suluhu ya migodi iliyofungwa.
"Lakini pia tunamuomba Rais aruhusu Biashara ya madini kufanyika katika mji wa Mererani na pia wale waliofungiwa waachiliwe kwani huwarahisishia kujipatia kipato na ajira za uhakika"alisema
Liana Mlay, mfanyabiashara anayetembeza bidhaa za nyumbani Kwa kutumia mkokoteni anasema ameishi mji huo Kwa miaka 30 Sasa lakini Kwa kipindi Cha Mika minne Sasa Hali imekuwa ngumu sana kwani hata Bidhaa muhimu anazouza za chakula huweza kupitia siku asiuze Kwa sababu ya kufa Kwa Biashara za madini mjini Mererani.
Ritha Steven Siliwimba , brocker wa madini Anasema Saniniu Laizer alikuwa akitoa msaada wa mchanga na fedha kwa akina Mama wengi wa Mererani lakini Toka njia yake kuvamiwa anashindwa kutoa udongo wa kutosha unaopelekea wanapata shida.
Ritha alisema Kampuni ya Franone haitoi ajira Kwa wazawa wa Mererani na hivyo kusababisha ukosefu mkubwa wa ajira Kwa wakazi wa mji huo na kupelekea uchumi wa watu hao kuzorota
Gladness Godfrey Mungi anasema njia za madini zimekatwa na kwenda Kwa Mwekezaji wa Kitalu C Franone na hivyo kupelekea kukosekana Kwa ajira za kudumu kwa wakazi wa Mererani kwani yeye Franone hajaajiri wakazi wa Mererani.
Wakizungumzia mgogoro wa Mererani , Waziri wa Madini Anthony Mavunde na Mkuu wa mkoa Manyara Queen Sendiga wametaka busara kutumika kumaliza migogoro ya Mererani.
Waziri Mavunde alisema Serikali haitaki kuona Mererani inakuwa na vurugu lakini pia Kuna wachimbaji wanahujumiana.
Alisema Wizara yake pia imekamilisha zoezi la kupiga picha eneo lote ya Migodi ya Tanzanite ndani ya Ukuta na nje ili kuona akiba ya Madini iliyopo.
"Baada ya taarifa kutoka tutawapa lakini maono yangu Mimi ipo siku Mererani itakuwa haina mgogoro hata mmoja "alisema
Kwa Upande wake Mkuu mkoa Manyara, Sendiga pia ametaka busara kutumika Mererani ili kumaliza migogoro.
"Kila mtu lazima akubali kupoteza kitu ili kutatua migogoro hapa Mererani"alisema
Katika Machimbo hayo mgogoro mkubwa ni sheria ya uchimbaji Madini ya Vito ambayo inataka mchimbaji kuchimba Madini katika eneo lake la lesseni tu kwenda chini.
Hata hivyo wachimbaji wanapinga sheria hiyo kwani Madini ya Tanzanite wanachamba kwa kufuata miamba ya Madini na mingi inaelekea kitalu C ambacho amepewa Mwekezaji mmoja tu Kampuni ya Franone .
Katika Machimbo ya Mererani kuna zaidi ya migodi 400 katika kitalu A,B,D lakini kitalu C Kuna Mwekezaji mmoja tu .
No comments:
Post a Comment