Tanzania, Guinea Bissau kufanya utafiti wa zao la korosho - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Saturday 22 June 2024

Tanzania, Guinea Bissau kufanya utafiti wa zao la korosho

 




Na Selemani Msuya, DSM

maipacarusha20@gmail.com 


NCHI ya Tanzania na Guinea Bissau zimekubaliana kushirikiana katika utafiti wa zao la korosho, ili kuhakikisha wanaongeza uzalishaji na kuinua uchumi wa wakulima.


Makubaliano hayo yamefikiwa na viongozi wa nchi hizo Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania na Rais wa Guinea Bissau, Umaro Embalo aliyepo nchini kwenye ziara ya kikazi ya siku tatu, Ikulu jijini Dae es Salaam.


Poa viongozi hao wamejadiliana namna ya kushirikiana katika sekta ya elimu, biashara, uwekezaji, ulinzi na usalama na nyinginezo.


Akizungumza na waandishi wa habari Rais Samia Suluhu amesema Tanzania na Guinea Bissau ni moja ya nchi zinazolima kwa wingi zao la korosho, hivyo wamekubaliana kushirikiana kwenye utafiti ambao utaleta tija kwenye zao hilo.


"Tumejadiliana kwa kina kuhusu  ushirikiano wetu ambao ulianza tangu wakati wa Hayati Mwalimu Julius Nyerere, ila tumeamua kuweka mkazo katika kuhakikisha tunafanya utafiti wa zao la korosho na biashara ili kukuza uchumi wetu," amesema.


Pia tumekubaliana kusukuma ajenda ya kukubaliana bei nzuri imepanga kushirikiana katika kukuza biashara hasa ya zao la korosho na kuongeza tafiti za kukuza uzalishaji wa zao hilo ili kuliongezea thamani.


Aidha Rais Samia amesema nchi hizo mbili zimepanga pia kushirikiana katika ukuzaji wa amani na usalama barani Afrika, ukuzaji wa biashara na uwekezaji, elimu, afya pamoja na uchumi wa buluu.


Rais Samia amesema eneo lingine ni maeneo huru ya uwekezaji ambapo baada ya kumaliza leo Rais Embalo ataangalia maeneo yetu ambayo ni EPZA na Reli ya Kisasa ya SGR ili kuona mfano halisi jinsi miundombinu inavyounganisha nchi zetu hizi mbili. 


Rais Samia amesema wamekubaliana kushirikiana na nchi zingine za Afrika katika kuhakikisha bidhaa za kilimo za Tanzania na Guinea Bissau zinapata bei nzuri kwa kutengeneza umoja katika soko la dunia. 


Aidha amesema bara la Afrika lipo mbioni kuhakikisha eneo huru la biashara linafunguka lengo likiwa ni kukuza zaidi kiwango cha biashara kati ya nchi za Afrika.


“ Kuanzishwa kwa eneo hili pia kutachochea ukuaji wa viwanda, uongezaji wa thamani wa mazao yetu na kuleta ajira kwa vijana hivyo tumesema eneo hili huru la biashara tunalitumia ipasavyo,” amesema


Kwa upande mwingine Rais Samia amesema Tanzania na Guinea Bissau zina maeneo makubwa ya Pwani hivyo watashirikana kwenye masuala ya uchumi wa buluu ikiwemo uvuvi, utalii kwenye fukwe na usafirishaji baharini.


“Tumekubaliana kuendelea kushirikiana katika masuala ya tishio la ugaidi pamoja na biashara haramu ya dawa za kulevya” amesema


Akizungumza katika mkutano huo wa waandishi wa habari, Rais wa Guinea Bissau, Umaro Embalo’ amesema Tanzania na nchi yake zikifanya kazi kwa pamoja zinaweza kuwa na amani ya kudumu na ustahimilivu wa kisiasa pamoja na kuwaletea maendeleo wananchi.


Aidha amesema wanawakaribisha sekta binafsi nchini Guinea Bissau kuwekeza kwani nchi hiyo ni lango muhimu la kuingia nchi zingine za Magharibi hasa kupitia eneo huru la biashara Afrika.


Rais Embalo amesema nchi hizo zinapaswa kutumia fursa walizonazo kuchochea maendeleo kwa haraka.

Pia Rais huyo amemualika Rais Samia kutembelea nchini Guinea Bissau, mwaliko ambao Rais Samia ameukubali.

No comments: